Dk Nchimbi awaonya wanaCCM udalali kwa wasaka uongozi

Njombe. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho kujiepusha kuwa madalali wa watu wanaosaka nafasi za uongozi.

Dk Nchimbi amesema kama kuna kitu kinachoweza kukidhoofisha chama hicho tawala ni viongozi kukubali kuwa madalali wa wagombea.

“Mtu anayetaka kukufanya uwe dalali tafsiri yake ameshakupima, amegundua unanunulika, anakudharau na ameamua kukutumia,” amesema Dk Nchimbi leo Ijumaa Aprili 19, 2024 akizungumza na viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya tawi hadi Mkoa wa Njombe akiwa ziarani.

Dk Nchimbi ameambatana na wajumbe wa Sekretarieti ya CCM katika ziara ya mikoa sita.

Ametoa mfano akisema utakuta kiongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya tawi, kata, wilaya na mkoa anakuwa na jina la mgombea mfukoni kwa sababu tu katengenezewa utaratibu wa fedha, anajaribu kuwa dalali wa mgombea.

“Wapo watu kwenye uongozi wanapewa rushwa ili kuitisha vikao vya kamati ya maadili kuwashughulikia wanaojua watagombea nao, wanakupunguza kasi. Nasema kataeni kwa nguvu zenu zote kuwa madalali wa kisiasa,” amesema.

Dk Nchimbi amewataka WanaCCM kujenga umoja ndani ya chama hicho kwa nguvu zao zote na kueleza mambo mazuri yanayotekelezwa na Serikali.

Amesema hatua hiyo itawezesha kupunguza uongo unaosambazwa na baadhi ya watu wanaozunguka katika maeneo mbalimbali wakisema Serikali haijafanya lolote.

Pia amesisitiza maadili na uadilifu kwa watoto kuanzia ngazi ya familia ili kuwa na vizazi bora.

“Lazima tujielekeze kwenye malezi bora ya watoto ili kupata vijana wenye maadili katika nchi yetu,” amesema.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amewataka wananchi kuyapuuza maandamano ya amani yaliyoandaliwa na Chadema akitoa maagizo kwa viongozi wa jumuiya za chama hicho kuwahamasisha wananchi kuchukua mikopo ya asilimia 10.

Makalla akizungumza katika mkutano wa ndani wa viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho mkoani Njombe, alitoa kauli hiyo alipoeleza kuhusu uamuzi wa Serikali kurejesha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Aprili 16, 2024 akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tamisemi kwa 2024/25 Waziri wa wizara hiyo, Mohamed Mchengerwa alitangaza kurejea kwa mikopo kuanzia Julai mosi 2024.

Makalla amesema Serikali imetoa fursa ya watu kupata mikopo ya asilimia 10, lakini Chadema inahamasisha washiriki wa maandamano ya amani yatakayoanza Aprili 22, 2024, yakipinga hali ngumu ya maisha.

“Yaani kuna neema ya vijana kupata mikopo wenzetu wanahamasisha maandamano,” amesema.

Alhamisi Aprili 18, 2024 Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alitangaza kuanza kwa maandamano Aprili 22 hadi 30, 2024 katika mikoa yote yakiongozwa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe na makamu wake Bara Tundu Lissu.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa azimio la chama hicho la Mtwara lililotaka kufanyika maandamano ya amani nchini ili kufikisha ujumbe wa kilio cha ugumu wa maisha na madai ya upatikanaji wa Katiba mpya itakayowezesha kupatikana Tume Huru ya Uchaguzi.

Makalla amewataka Watanzania na wana-CCM kupima chama chenye dhamana ya kuongoza na chama kisicho na dhamana.

Amesema CCM ina dhamana lakini wao hawana, ndiyo maana wanadhani kuwezesha vijana ni kuandamana.

Makalla amesema wakati Chadema wakilalamika hali ya umasikini, chama hicho tawala kinakwenda kutoa fursa kwa wananchi kuwawezesha kiuchumi ili kujikwamua na umasikini.

“Wana-CCM wakati hawa (Chadema), wakihamasisha maandamano, ninyi hamasisheni vijana wetu, mamalishe na watu wenye ulemavu wakachukue mikopo,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi Digital kuhusu kauli ya Makalla, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amewataka Watanzania kutokisikiliza CCM badala yake wajikite katika maandamano ya Aprili 22.

“Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waiulize CCM tangu tuanze maandamano Januari hadi sasa haijataka Serikali kupeleka bungeni wala Baraza la Mawaziri mpango wa dharura wa kupunguza gharama za maisha kwa wananchi.

“Kama kweli CCM inawajali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu mbona haijasukuma Serikali kuhakikisha kufanya marekebisho ya kisheria na kikatiba ya kuwezesha kuwepo kwa uchaguzi huru na haki,” amesema Mnyika.

Mnyika amewataka Watanzania kujiandaa na maandamano hayo.

Related Posts