Matokeo yamtisha straika Namungo | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Namungo, Hassan Kabunda amesema hali inayopitia timu hiyo sio shwari kufuatia matokeo mabaya mfululizo ya Ligi.

Mechi tano za mwisho, Namungo imeshinda moja dhidi ya Pamba Jiji Oktoba 28 kwa bao 1-0 ikipoteza nne mbele ya Yanga 2-0, Mashujaa 1-0, KMC 1-0 na Simba 3-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kabunda alisema ni kama bahati haiko upande wao kwani wana wachezaji wazuri na kocha mzoefu Juma Mgunda.

Aliongeza kuwa matokeo hayo yanawapa wakati mgumu wachezaji na kuwakatisha tamaa licha ya kazi kubwa ya Mgunda kuwarudisha mchezoni.

“Tuna michezo 18 migumu iliyopo mbeleni, tunapitia kipindi kigumu sana cha kukosa matokeo tunaamini timu itakuwa sawa kuna muda wachezaji tunakata tamaa lakini kocha anatupa moyo,” alisema Kabunda.

Namungo iko nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi ikishinda michezo mitatu na kupoteza tisa ikiwa miongoni mwa timu mbili Ligi Kuu zilizopoteza michezo mingi.

Licha ya matokeo hayo lakini timu hiyo imeruhusu mabao 15 wastani wa kufungwa bao moja kila mechi wakiweka kambani mabao matano na washambuliaji wa Namungo wakiwa hawajatikisa nyavu za wapinzani hadi sasa.

Related Posts