YANGA na Simba wikiendi hii zitakuwa Algeria kucheza mechi zao za pili hatua ya makundi dhidi ya miongoni mwa vigogo wa nchi hiyo katika michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Wataanza Yanga kucheza dhidi ya MC Alger ambao ni mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1976. Timu hizo zinakutana katika mchezo wa Kundi A unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Ali La Pointe uliopo Mji wa Douéra.
Awali mchezo huo ulipangwa kuchezwa Uwanja wa 5 July 1962 uliopo Algiers lakini wenyeji wamepeleka maombi yao Caf wakitaka wabadilishe uwanja, ombi ambalo linafanyiwa kazi na lolote linaweza kutokea.
Kesho yake kwa maana ya Desemba 8, Simba itapambana na CS Constantine kwenye Uwanja wa Chahid Hamlaoui uliopo Mji wa Constantine ukiwa ni mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika Kundi A.
Tutajuana hukohuko ni kauli ambayo unaweza kuitumikia ukiangalia namna timu ambazo Simba na Yanga zinakwenda kukutana nazo si za kawaida ukiangalia pia ligi yao ipo juu kulinganisha na yetu.
Ukiwaangalia wapinzani wa Yanga, MC Alger, wapo vizuri katika ligi yao wakishika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Algeria baada ya kucheza mechi 10 na kukusanya pointi 17 zilizotokana na kushinda mechi nne, sare 5 na kupoteza mbili huku ikifunga mabao 11 na kuruhusu manane.
Yanga wao wanashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara wakikusanya pointi 27 baada ya kucheza mechi 11, wameshinda tisa na kupoteza mbili huku timu hiyo ikifunga mabao 16 na kuruhusu manne.
Kwa takwimu hizo, Yanga inaonekana kuwa vizuri katika kufunga mabao na kulinda, huku pia ipo vizuri kwenye ukusanyaji wa pointi kulinganisha na wapinzani wao MC Alger.
Hata hivyo, ugumu uliopo katika Ligi Kuu ya Algeria maarufu Ligue 1, unaweza MC Alger kuwa na matokeo ya aina hiyo.
Katika viwango vya ubora wa Caf, Ligi Kuu Algeria yenye timu kama MC Alger, CS Constantine, USM Alger, ES Setif, CR Belouizdad, JS Kabylie na JS Soura, inashika nafasi ya pili, huku Ligi Kuu Bara ikiwa ya sita.
Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuondoka leo Jumanne kuelekea Algeria lakini tayari imetanguliza watu wao wawili kwenda kuweka mambo sawa.
Taarifa za ndani zinasema tayari Hafidhi Saleh ambaye ni mratibu wa timu amewasili Algeria akiwa na Mkurugenzi wa Mashindano wa klabu hiyo, Ibrahim Mohamed.
Mwanaspoti limepata taarifa kuwa kilichowatanguliza viongozi hao ni sababu kuu tatu ambazo Yanga iliziangalia kwa jicho la tatu.
“Kule ni ugenini hivyo viongozi waliokwenda watakuwa na kazi ya kufanya maandalizi yote ya wapi timu itafikia na mambo mengine kama usafiri na kadhalika.
“Sababu ya pili wamepata taarifa kuwa mechi inaweza kuhamishwa uwanja, hivyo wamefika kupata uhakika na kujua timu itafika wapi kama uwanja utabadilishwa,” kilisema chanzo.
Hata hivyo, uamuzi wa MC Alger kutaka kubadilisha uwanja unaweza usiwasumbue sana Yanga kwani wapinzani wao wana marufuku ya mechi nne za Caf nyumbani kucheza bila ya mashabiki.
MC Alger imetakiwa kucheza mechi nne za nyumbani za michuano ya Caf bila ya mashabiki kutokana na utovu wa nidhamu waliouonyesha mashabiki wao katika mchezo wa mwisho wa kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo msimu huu katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir.
Rais wa MC Alger, Mohamed Hakim amesema klabu hiyo imepeleka barua Caf juu ya kubadilisha uwanja huku wakitarajia ombi lao kukubaliwa.
“Barua yetu imepokelewa na Caf na upo uwezekano mechi yetu dhidi ya Yanga ikahamishiwa kuchezwa uwanja wetu wa Ali la Pointe, zipo sababu za msingi sisi kuwasilisha ombi hilo, tunataka mechi hii iwe na mvuto pande zote, watu wafurahie mpira zaidi,” alisema Hakim juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari nchini Algeria.
MC Alger ilianzia hatua ya awali kwa kuiondosha Watanga kutoka Liberia kwa jumla ya mabao 4-0 kisha ikaichapa US Monastir ya Tunisia jumla ya mabao 2-1, ikafuzu makundi.
Yanga hatua za awali ilifunga mabao 17 katika mechi nne ikianza kuichapa Vital’O kutoka Burundi jumla ya mabao 10-0 kisha CBE SA ya Ethiopia 7-0.
Mechi za kwanza makundi, Yanga nyumbani imefungwa 2-0 na Al Hilal, wakati MC Alger ugenini ikitoka 0-0 dhidi ya TP Mazembe.
Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka kesho Jumatano kwenda Algeria katika mchezo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi dhidi ya CS Constantine, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akieleza wazi anawatambua vyema wapinzani hao.
Akizungumzia mchezo huo, Fadlu alisema Constantine ni timu nzuri na yenye wachezaji wazuri ingawa jopo la benchi lao la ufundi lilianza kuwafuatia kwa ukaribu na kugundua wana muunganiko mzuri, kuanzia katikati ya kiwanja hadi ushambuliaji.
“Ni timu nzuri ndio maana hata ukiangalia mchezo wao wa kwanza walipata pia ushindi tena ugenini, hii inaonyesha wazi sio rahisi kwetu na tunapaswa kujipanga vizuri ili kuendeleza rekodi nzuri ambayo tumeanza nayo nyumbani,” alisema.
Kocha huyo alisema licha ya timu hiyo kucheza kwa muunganiko, ila kuna wachezaji ambao wanatambua ubora wao huku akiweka wazi miongoni mwao ni kiungo nyota wa kikosi hicho, Brahim Dib na mshambuliaji, Zakaria Benchaa wote raia wa Algeria.
“Tunapaswa kucheza katika ubora wa kiwango kizuri katika mchezo huo, kila mmoja yupo tayari kwa changamoto hiyo ugenini na jambo bora ni kuona wachezaji wote wako katika morali ya hali ya juu, sio rahisi ila inawezekana kwa umoja uliopo,” alibainisha Fadlu.
Timu hizo zinakutana huku Simba ikiwa na rekodi bora tofauti na wapinzani wao katika michezo ya Ligi waliyocheza hadi sasa, ambapo kikosi hicho cha Msimbazi kimekuwa tishio katika ushambuliaji na uzuiaji ukilinganisha na CS Constantine.
Constantine inayonolewa na Kocha Mkuu, Kheireddine Madoui imecheza michezo 10 ya Ligi ya Algeria ‘Ligue 1’, kabla ya ule wa jana dhidi ya Biskra ambapo imeshinda mitano, sare mitatu na kupoteza miwili ikiongoza msimamo kwa pointi 18.
Katika michezo hiyo 10, Constantine imekuwa haina safu nzuri ya ushambuliaji na uzuiaji kwani hadi sasa tayari imefunga mabao 11 na kuruhusu manane, ikiwa haina uwiano mzuri wa kuzuia na kushambulia jambo linaloweza kuipa faida zaidi Simba.
Katika mabao hayo 10, nyota wa timu hiyo, Brahim Dib ndiye anayeongoza akiwa amefunga matano huku matatu kati ya hayo ‘Hat-Trick’ akifunga kwenye mchezo ambao kikosi hicho kilishinda mabao 3-2, dhidi ya JS Kabylie Oktoba 12, 2024.
Katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, Brahim Dib amefunga mabao mawili ambapo moja lilikuwa ni la hatua za awali huku lingine akifunga mechi ya kwanza ya makundi ambapo kikosi hicho kilishinda ugenini 1-0, dhidi ya CS Sfaxien.
Kwa upande wa mshambuliaji, Zakaria Benchaa ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kufuzu hatua ya makundi kwani amefunga mabao manne katika michezo minne aliyocheza, ingawa hadi sasa hajafunga bao lolote kwenye Ligi Kuu ya Algeria.
Katika mabao 11 ambayo Constantine imeyafunga, sita imefunga kipindi cha kwanza huku matano ikifunga cha pili, huku kwa upande wa Simba iliyocheza michezo 11, ikiwa nafasi ya pili na pointi 28 kwenye Ligi Kuu Bara, imefunga 22 na kuruhusu matatu.
Katika mabao hayo 22 ambayo Simba imeyafunga haina tofauti sana na wapinzani wao Constantine kwani imekuwa na mgawanyiko mzuri, kwa sababu kati ya hayo 12, imefunga kipindi cha kwanza huku mengine 10, ikiyafunga kipindi cha pili cha mchezo.
Wakati Constantine ikimtegemea zaidi Brahim Dib, kwa upande wa Simba inamtegemea kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua ambaye ndiye aliyeipa pia pointi tatu katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam alipofunga bao pekee kwa penalti katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Bravos.
Kama haitoshi, nyota huyo ndiye tegemeo katika kikosi cha Fadlu kwa sababu hata katika Ligi Kuu Bara amekuwa ni tishio, kwani kwenye mabao hayo 22, ambayo Simba imefunga tayari amechangia tisa, akifunga matano na kuchangia manne ‘asisti’.
Simba ipo hatua ya makundi baada ya kuitoa Al Ahli Tripoli ya Libya kwa jumla ya mabao 3-1, baada ya kutoka suluhu mechi ya kwanza ugenini, kisha kushinda 3-1 ikiwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kwa upande wa Constantine ilianzia hatua za awali kwa kuitoa Police FC ya Rwanda kwa jumla ya mabao 4-1, kisha kukutana na Nsoatreman FC ya Ghana na kuitoa pia kwa jumla ya mabao 3-0, kufuatia kushinda ugenini 2-0, kisha nyumbani bao 1-0.
Katika mechi zao za kwanza hatua ya makundi, zote zimepata ushindi wa 1-0, wakati SImba ikishinda nyumbani, Constantine iliichapa CS Sfaxien ugenini.