Nondo asimulia alivyotekwa, kuteswa | Mwananchi

Dar es Salaam.  Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ACT-Wazalendo, Abdul Nondo amesimulia mwanzo mwisho tukio la kutekwa kwake, huku akisema bado ana hofu kuhusu maisha yake kutokana na vitisho alivyopewa.

Amesema hofu inaongezeka zaidi kwa namna tukio hilo lilivyotokea, akisema kama waliweza kumteka hadharani, basi watu hao wamemuambia hawashindwi kumchukua tena mahali popote endapo akifungua mdomo wake kueleza kilichojiri baada ya kumshikilia.

Nondo ambaye amelezwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam akipatiwa matibabu kutokana na majeraha ya kipigo, ameeleza hayo jana Jumatatu, Desemba 2, 2024 wakati akihojiwa na Kituo cha Redio cha Kimataifa cha DW.

Mwanasiasa huyo alitekwa alfajiri ya Desemba mosi, 2024 katika kituo cha mabasi cha Magufuli, jijini Dar es Salaam, akitokea mkoani Kigoma alikokuwa akishiriki  shughuli za chama hasa kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27,2024.

Baada ya tukio hilo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini David Misime alisema kuna mtu mmoja mwanamume amekamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa wakitumia gari nyeupe lenye usajili wa namba T 249 CMV Land Cruiser.

Baadaye usiku Jeshi la Polisi lilitangaza Nondo kapatikana eneo la fukwe la Coco Kinondoni baada ya kutekelezwa na wasiomfahamu.

Awali, wadau mbalimbali kikiwamo chama chake walipaza sauti wakitaka Nondo aachiwe huru.

Akizungumza kwa shida kutokana na maumivu yanayomkabili, Nondo anasema alikuwa anatokea Kigoma na alifika Dar es Salaam, saa 10 alfajiri wakati akitoka nje ya kituo hicho kutafuta usafiri, wakatokea vijana sita, waliomvamia na kumtaka kutopiga kelele.

“Waliniambia nitulie, awali nilihisi ni vibaka, lakini jambo lilikuwa ‘serious’ zaidi baada ya kuona gari nyeupe HardTop likasogezwa na milango ya nyumba ilifunguliwa ili niingie ndani.

“Nilipiga kelele kuingia katika gari, kuhakikisha siingii, nilikuwa naomba msaada kwa watu waliokuwapo nikawaambia nisaidieni naitwa Abdul Nondo, maana kulikuwa na watu wa boda, wasafiri waliokuwa wanafika kutoka safarini  na wengine kwenda mikoani,” anasema Nondo.

Nondo anasema tukio la kutekwa kwake lilikuwa la ghafla, kwa kuwa hakuwa na wazo kama kuna watu wanamfuatilia ili akamatwe. Anasema ukatamaji ule haukuwa wa kawaida kwa sababu waliotekeleza tukio hilo hawakujitambulisha.

“Nilichosikia walikuwa wakilaumu pingu ziko wapi, baada kuzikosa pingu walinifunga kamba kwenye mikono tena kwa nguvu sana mikono ikiwekwa nyuma na usoni walinifunga kitambaa,” anadai.

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT- Wazalendo Abdul Nondo akiwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kutokana na kuumizwa kwa kipigo na watu wanaodaiwa kumteka.

Katika purukushani za Nondo kuchukuliwa inaelezwa kuwa begi lake lilindondoka pamoja na pingu.

Nondo anasema baada ya kuchukuliwa gari lilikwenda kwa kasi kisha kuingia sehemu na kuegeshwa na kumshusha mwanasiasa huyo, kwa kumuweka pembeni ya kibaraza na kuanza kumshushia kipigo cha magongo, kwenye unyayo, mabega na maungio ya miguu, magoti, mapaja na kumnining’iniza juu chini.

“Walikuwa wananiambia mimi si cha mdomo sasa tunakuua wewe… walikuwa wananitukana matusi makubwa pia. Baada ya kipigo wakaniingiza kwenye gari, kabla ya kunishusha tena na kunipiga, baada ya mateso waliwasha gari kwenda umbali mrefu, walinishusha na kunipakiza kwenye gari jingine.”

“Baada ya umbali mrefu nikashushwa, nikaambiwa shuka na kuanza kutembea, lakini wakati natembea nilihisi kukanyaga kokote na uwepo wa upepo wa bahari na mawimbi nikajua hawa watu,” anasema Nondo.

Nondo ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TNSP) anasema:“Nikasema hawa watu wanakwenda kunitupa baharini, maana walinifunga na kamba na macho wanakwenda kunitupa baharini tena kwenye kina kwa hiyo nitakosa msaada, nitakufa.”

Anaendelea kusimulia kuwa walivyompeleka hadi katika eneo hilo wakamuamulu akae asigeuke kwani watampiga risasi.

“Sikugeuka, wakachukua kama kisu, wakanikata kamba walionifunga kwenye mikono. Wakaniambia ukitoka hapa nenda moja kwa moja nyumbani usipitie sehemu yoyote, wala kuahadithia, tusisikie sauti kwenye chombo cha habari chochote, hatutaki kusikia makelele nenda nyumbani ukatulie, ukiendelea tutakukamata mara ya pili,” anadai Nondo.

Licha ya kuwa na maumivu mwilini Nondo anasema alijitahidi kutembea ingawa kwa shida ili kutafuta msaada ndipo alipoona barabara ya lami.

“Nikawa najikongoja hadi barabarani kuomba msaada, nikafanikiwa kupata bodaboda aliyewaambia wenzake watatu walionihoji ili kutengeneza uaminifu kisha kukubali kunibeba.

Boda akaniambia nakupeleka nyumbani kwako nikamwambia haiwezekani kwa mazingira nahitaji msaada wa matibabu hivyo anipeleke ofisi za chama, maana sikuwa na simu,” anadai.

Nondo anasema tukio hilo lilimuogepesha kwa sababu kwa nyakati tofauti alikuwa anaambiwa atauawa. Anasema tukio la awali ilikuwa matukio ya utekaji hayakukithiri, lakini la hivi sasa limetokea kukiwa na matukio ya mfululizo ya utekaji, ndio maana alikuwa na hofu kubwa.

“Bado nina hofu na maisha yangu kwa tukio lililonipa kutokana na vitisho nilivyovipata,” anasisitiza Nondo.

Machi 2018 Nondo akiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na kutekelezwa wilayani Mufindi mkoani Iringa.

‘Hali ya Nondo inaendelea vizuri’

Naibu Katibu wa Habari, Mawasiliano kwa Umma wa ACT-Wazalendo, Shangwe Ayo ameliambia Mwananchi kuwa hali ya Nondo inaendelea kuimarika kutokana na matibabu anayoendelea kuyapata Aga Khan.

Katika hatua nyingine, Shirika la Vijana Tanzania Youth Association (TYA) limelaani mfululizo na mwenendo wa matukio ya utekaji au ukamataji usiofata sheria na taratibu za ukamataji nchini.

TYVA inasema imeshuhudia matukio mfululizo ya vijana kutekwa, kuumizwa na kukamatwa kiholela kunakosababisha hofu na taharuki kwa jamii kutoka Januari hadi sasa, pamoja matukio ya hivi karibuni ya vijana kutekwa au kukamatwa kiholela.

“Matukio ya utekaji au ukamataji usiofata sheria na taratibu za ukamataji yanayozidi kushamiri nchini hasa kwa kundi la vijana wanaopaza sauti kuhusu utawala bora na usawa wa kidemokrasia nchini,” anasema Peter Masoi ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya taasisi hiyo.

Masoi anasema matukio ya utekaji au ukamataji usiofata sheria na taratibu za ukamataji yanayozidi kushamiri nchini tukiamini yana lengo na nia ovu ya kujaza Watanzania na vijana hofu kwenye kusimania utawala bora, usawa wa kidemokrasia na uhuru wa kushiriki katika michakato ya kisiasa.

Related Posts