Watu kadhaa wanahofiwa kupoteza maisha baada ya lori la mizigo aina ya Scania kugongana na Toyota Hiace inayofanya safari kati ya Kayanga wilayani Karagwe na Bukoba Mjini.
Ajali hiyo imetokea leo Jumanne, Desemba 3, 2024 katika Barabara ya Kihanga-Kyaka.
Taarifa zinasema kuwa, miili ya watu kadhaa imehifadhiwa katika Hospitali Wilaya Karagwe, huku wengine wakijeruhiwa vibaya.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Julius Laizer amethibitisha kutokea kwa ajali akisema taarifa kuhusu waliopoteza maisha na waliojeruhiwa itatolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera.
“Ni kweli, ajali imetokea ikihusisha lori na gari la abiria aina ya Toyota Hiace, utaratibu kuhusu waliopoteza maisha na majeruhi kwenda hospitali ya wilaya unaendelea kufanyika. Taarifa zaidi zitatolewa na RPC,” amesema Laizer.
Habari zaidi kutoka kwa mashuhuda zinadai kuwa, chanzo cha ajali ni lori kuparamia Hiace iliyokuwa imesimama pembezoni mwa barabara ikishusha abiria.
Endelea kufuatilia taarifa zaidi kupitia mitandao ya kijamii