Musoma. Imeelezwa kuwa, asilimia 90 ya wakazi wa Mkoa wa Mara wanatumia nishati isiyokuwa safi na salama kwa kupikia.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Desemba 3, 2024 mjini Musoma na Mkuu wa Mkoa huo, Evans Mtambi alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari juu ya mradi wa uuzwaji wa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama kupitia mradi unaotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).
Mtambi amesema matumizi ya nishati chafu yanahusisha kuni na mkaa hali inayochangia uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti.
“Katika asilimia hizo, asilimia 85 wanatumia kuni na asilimia tano wanatumia mkaa, kwa kweli mkoa wetu ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa matumizi makubwa ya nishati isiyokuwa salama,” amesema.
Amesema hali hiyo inasababisha uzalishaji wa kemikali ambazo sio rafiki kwa afya ya binadamu na mazingira kwa jumla.
“Kama mtakumbuka, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mkakati maalumu wa kitaifa wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, mkakati unaolenga ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe tayari wanatumia nishati safi na salama ya kupikia,” amesema Mtambi.
Amesema mradi huo utahusu uuzwaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya Sh20,000 badala ya Sh45,000 lengo likiwa ni kutaka wananchi wengi watumie gesi.
Deusdedith Malulu kutoka Rea kitengo cha Nishati Jadidifu, amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza Januari mwakani.
“Huu mradi unalenga kuwafikia wakazi wote kuanzia ngazi ya vitongoji, kila mtu atafikiwa na upo utaratibu maalumu uliowekwa ikiwa ni pamoja na utambuzi kwa kutumia kitambulisho au namba ya kitambulisho cha Taifa, namba moja itatumika kupata jiko moja tu,” amesema.
Baadhi ya wakazi wa Musoma wamesema miradi hiyo ni mizuri huku wakitoa angalizo kwa wasimamizi kuhakikisha hakuna upendeleo wakati wa utekelezaji.
“Mfano hayo majiko isije ikatokea kipaumbele kikatolewa kwa wale wenye uwezo ambao wana weza kununua majiko kwa bei ya sokoni na kuwaacha wasiojiweza ambao nadhani ndio walengwa halisi,” amesema Upendo Jamhuri.
Juma Omollo amesema mradi wa mkopo kwa ajili ya vituo vya mafuta unapaswa kuwanufaisha wakazi wa vijijini badala ya wawekezaji kutoka mijini na kwenda kuwekeza vijijini.