Asimulia mwanaye alivyonusurika kuuawa kwa kuchinjwa na mumewe

Shinyanga. Siku moja baada ya Mkazi wa Kijiji Cha Mwamagunguli, Kata ya Kolandoto mkoani Shinyanga, Peter Makoye (45) kukutwa amefariki dunia kwa kujinyonga baada ya kujaribu kumuua mwanaye (6), mke wa marehemu, Elizabeth Mwigulu ameelezea tukio hilo lilivyotokea.

Mtoto huyo kwa sasa anauguza jeraha lililosababishwa na shambulio hilo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (Mwawaza).

Mwananchi Digital imefika pia katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (Mwawaza) anakopatiwa matibabau mtoto huyo na kukutana na mama yake mzazi ambaye anamuuguza, huku jitihada za madaktari zikiendelea kuhakikisha afya yake inaimarika.

Elizabeth amesema anaamini mmewe alichukua uamuzi wa kujitoa uhai baada ya kuhisi amemuua mtoto wake kwa kumchinja.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Desemba 3, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema uchunguzi wa awali umebaini uamuzi wa mwanaume huyo umechangiwa na ugomvi wa shamba na mkewe.

Hata Elizabeth amedai mgogoro wa shamba ulioibuka baina yao ndio sababu ya matukio hayo.

“Mwanangu amekatwa shingo na baba yake, ilikuwa baada ya baba kuuza shamba tulilotaka kufanya kiwanja cha kujenga, tulichonunua Kagongwa mwezi wa nane mwaka huu, aliuza pamoja na mabati 40 tuliyokuwa tumeshayanunua,” amedai Elizabeth.

Amesema baada ya mmewe kuuza kiwanja hicho na mabati hayo bila ridhaa yake, ndipo mgogoro ukaibuka baina yao.

Mama huyo anasema alitoa taarifa kwa wazazi wa mumewe ili kupata suluhu na mwezi wa tisa aliitwa na baba yake (baba wa marehemu) mkoani Mwanza.

“Sikujua alichoelezwa huko ila baadaye aliaga kwao kwamba amepata kazi Nzega. Nikawaambia ukweni kuwa kawadanganya kwa sababu siku chache tu alirudi Shinyanga, alikuwa nyumbani Kolandoto,” amesimulia Elizabeth.

Amesema jana Jumatatu Desemba 2, 2024, saa 9 usiku aliamka kwenda chooni, wakati anarejea ndipo alipomuona mumewe akiwa amesimama mlangoni, akamhoji kwa nini wakwe zake wanamtetea kuliko yeye mtoto wao.

“Akaanza kunikimbiza hadi kwenye mahindi ,nikamzidi mbio akarudi ndani huku akinitaka na mimi nirudi. Nikamwambia nitarudi kukishakucha. Niliporudi nyumbani nikakuta mtoto amekatwa na kisu shingoni, kisha kamtoa chumbani akamweka kwenye makochi na yeye kajinyonga,” anasimulia.

Huku akitokwa machozi, mama huyo amesema baada ya kukuta kitinda mimba wake kati ya watoto wao watatu amejeruhiwa shingoni, alimchukua haraka na kumuwahisha Hospitali ya Kolandoto kisha kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Daktari aliyemtibu mtoto huyo, Dk Dotto Matinde akizungumzia kwa niaba ya Ofisa Habari wa hospitali hiyo, George Maganga, amesema walimpokea mtoto huyo akiwa na jeraha shingoni lililokuwa linavuja damu nyingi.

Dk Matinde amesema baada ya uchunguzi wa awali wa jeraha la mtoto huyo aliyeonekana kupoteza fahamu kutokana na kupoteza damu nyingi, walibaini limesababishwa na kukatwa na kitu chenye ncha kali.

“Na tukampeleka moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji kwa ajili ya kudhibiti damu iliyokuwa inavuja, tulifanikiwa na mgonjwa sasa hivi yuko wodini anaendelea vizuri, ameamka kutoka kwenye dawa za usingizi,” amesema Dk Matinde.

Kuhusu mwili wa marehemu, Kamanda Magomi amesema umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kabla ya kukabidhiwa kwa ndugu kwa maziko.

“Mwili wa marehemu bado unafanyiwa uchunguzi na baada ya taarifa za uchunguzi kukamilika utakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya shughuli za mazishi,” amesema Kamanda Magomi.

Related Posts