Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33), anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili likiwamo la kujipatia Sh5.1 bilioni kwa njia ya udanganyifu, amehoji sababu za upande wa mashtaka kushindwa kukamilisha upelelezi wa shauri hilo kwa wakati.
Mshtakiwa anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Saccos ya Jatu kwa madai kuwa, fedha hizo ‘atazipanda’ kwenye kilimo cha mazao ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.
Gasaya ametoa maelezo hayo leo Jumanne, Desemba 3, 2024, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mshtakiwa ametoa malalamiko hayo, baada ya Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele kuieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, hivyo upande wa mashtaka wanaomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Akiwa amevalia kaunda suti rangi ya kijivu iliyokolea huku mkono wa kulia akiwa ameshikilia ‘diary’ rangi ya chungwa na chini akiwa ametupia kiatu cheusi, alinyoosha mkono juu kuashiria kuwa anaomba Mahakama impe nafasi ya kuongea na alipopewa nafasi hiyo alianza kudai kuwa, upande wa mashtaka umekuwa ukirudia maelezo yale yale kila mara na sehemu ya maelezo yake ilikuwa kama ifuatavyo.
Mshtakiwa: “Mheshimiwa hakimu kikao cha mwisho, ulitoa maelekezo kwa upande wa mashtaka waje na majibu juu ya upelelezi wa kesi hii.
Sasa nashangaa wanarudia maelezo yale yale kuwa upelelezi wa kesi hii haujakamilika. Mheshimiwa hakimu, huu ni mwaka wa pili sasa… upelelezi wa kesi yangu bado haujakamilka.”
Hakimu: “Mara ya mwisho sikutoa maelezo yoyote, bali niliwataka wakamilishe upelelezi kwa wakati.”
Mshtakiwa: “Sasa Mheshimiwa hakimu, upelelezi wa kesi hii utakamilishwa lini?”
Hakimu: “Mahakama yangu imefungwa mikono, haiwezi kufanya chochote kwa kuwa kesi ni ya uhujumu uchumi na Mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza, isipokuwa kwa kibali maalumu. Hivyo sasa, naelekeza upande wa mashtaka wajitahidi kukamilisha upelelezi kwa wakati.”
Hakimu Mhini baada ya kueleza hayo, aliahirisha kesi hito hadi Desemba 16, 2024 kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili kutokuwa na dhamana.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.
Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa, Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, kwa njia ya udanganyifu alijipatia Sh5.139 bilioni kutoka Saccos ya Jatu.
Shtaka la pili ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 jijini Dar es salaam.
Mshtakiwa anadaiwa kujihusisha na muamala wa Sh5.139 bilioni kutoka katika akaunti ya Jatu Saccos iliyopo Benki ya MNB tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC iliyopo katika benki hiyo.