Dodoma. Hatimaye Serikali imesikia kilio cha wabunge kuhusu wanyama wakali na waharibifu, kwa kutoa kibali cha kuwapunguza wanyama hao kwenye baadhi ya maeneo.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Desemba 3, 2024, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana wakati akifungua semina ya maofisa wanyamapori jijini Dodoma.
Dk Chana amesema ametoa kibali cha kupunguza wanyama wakali katika baadhi ya maeneo na kuwa amefanya hivyo baada ya kupata ushauri kutoka Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (Tawa).
“Tutapunguza mamba, kiboko na tembo, mwenyekiti aliniambia acha mheshimiwa waziri tutakupelekea kwenye proper formula (utaratibu maalum), Taifa lipate hela kuliko kupunguza kama wanyama wakali,”amesema.
Amesema wanyama aina ya tembo watapunguzwa kwa kutumia utaratibu maalumu na kuwa wenzao wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri) wanafanya sensa na wako uwandani kuhesabu wanyama.
“Sasa tumekuja baadhi ya maeneo yenu kupunguza hao wanyama. Nimeelekeza tunapofika hakikisha mkuu wa wilaya na mbunge wanataarifa hao ndio wasemaji wetu kwamba utekelezaji wa Ilani (ya uchaguzi) unafanyika,”amesema Dk Chana.
Hata hivyo, amesema ni lazima watengewe fedha katika halmashauri zao kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yao.
Amehoji inakuwaje maofisa hao, wanashindwa kushawishi baraza la madiwani katika halmashauri zao kutengewa fedha za mafuta kwa ajili ya shughuli zao.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Stanslaus Nyongo amesema wahifadhi hao na wizara yake inayodhima ya kuhakikisha kero na vilio vya wananchi vinashughulikiwa kwa wakati.
Amesema changamoto inayowakabili ni kulipa kifuta jasho na fidia kwa wakati, tatizo linalosababishwa na wahifadhi hao kushindwa kufikisha taarifa za watu walioathirika na wanyama hao kwa wakati wizarani.
Amesema kuna siku Dk Chana alimtuma kumwakilisha kwenye ziara ya Makamu wa Rais mkoani Tabora ambapo alikutana na madai ya fidia kwa tukio alilolitolea maelekezo Mei.
Bila kufafanua zaidi amesema alipigiwa simu na mbunge kuwa tembo wamevamia jimboni kwake na yeye alimuunganisha na mhifadhi katika halmashauri husika.
Amesema alimpa maelekezo taarifa za tukio hilo ziende wizarani kwa haraka lakini hakufanya hivyo.
“Kati ya Septemba na Oktoba niko katika mkutano wa hadhara ikaibuka madai hayajalipwa. Nikakumbuka jambo hilo nililipokea mimi mwenyewe,”amesema.
Amesema alipowasiliana na wasaidizi wake juu ya utekelezaji wa jambo hilo wakamweleza kuwa taarifa hazijafika wizarani licha ya kuelezeka zifike kwa haraka.
Nyongo amesema alipotafutwa mhifadhi aliyepewa maelekezo hakupatikana. Amesema amekutana na changamoto ya ucheleweshaji wa taarifa hiyo katika maeneo mengi na kuyataja baadhi kuwa ni Masasi na Kilwa.
Mkurugenzi wa Wanyamapori, Dk Alexander Alexander Lobora, amesema migongano kati ya binadamu na wanyamapori imekuwa ikiongezeka kutokana shughuli za kibinadamu kufanyika karibu na maeneo ya hifadhi na shoroba za wanyama.
Amesema changamoto hiyo imeathiri halmashauri zaidi ya 42 kati halmashauri 91 zenye changamoto hiyo.
Dk Lobora amesema changamoto hiyo imekuwa ikiathiri uchumi wa mtu mmoja, Taifa na kusababisha taharuki kwa wananchi wanapoingia pindi wanyama wanapoingia katika maeneo yao.
Amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwamo kuandaa na kutekeleza mikakati pamoja na kufanya doria za kudhibiti wanyama kwenda kwenye maeneo ya wananchi.
Dk Lobora amesema pamoja na mikakati hiyo Serikali imeendelea kutekeleza Kanuni ya Kifuta Jasho na Machozi ya Mwaka 2021 na marekebisho yake ya mwaka 2024 ambayo yameoongeza kidogo kiwango kifuta jasho.
Amesema Serikali imeendelea kutoa kifuta jasho na machozi na katika mwaka 2023/24 wametoa kwa wananchi 14,959 kutoka halmashauri 53.
Dk Lobora amesema wananchi hao walilipwa wanyama wakali na waharibifu walilipwa Sh3.1 bilioni.
Amesema tangu Julai mwaka huu, wamelipa Sh2.5 bilioni ambazo ni madai yaliyocheleshwa kulipwa katika kipindi cha nyuma.
Juni 30, mwaka 2022, uharibifu na mauaji yanayosababishwa na uvamizi wa tembo nchini yaliwaibua wabunge 13 wakitaka Serikali ieleze mikakati inayochkua kuwanusuru na watu na tatizo hilo.
Pia, mbunge wa Kerwa (CCM) Innocent Bilakwate ambaye wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2023/24, aliomba Serikali kuwapatia tembo uzazi wa mpango ili kupunguza kasi ya kuzaliana.
Mbunge huyo alisema hakuna namna nyingine kama Serikali inashindwa kuwavuna tembo ambao wamekuwa ni hatari kwa maisha ya wanadamu.
Aprili 30, 2024 suala hilo lilikuja kivingine kupitia mbunge wa Mbarali (CCM) Bahati Ndingo ambaye aliwasilisha hoja bungeni kuhusu tembo kuingia katika makazi ya watu na kusababisha shughuli za kiuchumi na kijamii kusimama kwa zaidi ya miezi mitatu.
Ndingo alitaka Serikali kuweka mikakati ya ziada ya kukabiliana na tembo wanaovamia maeneo ya makazi ikiwa ni pamoja na kuwavuna.