Chikola akwepa presha ya ufungaji Bara

LICHA ya kuwa kwenye kiwango bora na kasi kubwa ya kutupia mabao, winga wa Tabora United, Offen Chikola amesema hana malengo ya kujiweka kwenye vita ya kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwani kipaumbele chake ni kuisaidia timu kufanya vizuri katika mechi.

Chikola aliyejizolea umaarufu hivi karibuni baada ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Yanga, ameshatupia kambani mabao manne msimu huu katika mechi 13 za Tabora United inayoshika nafasi ya tano ikiwa imevuna alama 21.

Winga huyo wa zamani wa Ndanda, Fountain Gate na Geita Gold aliliambia Mwanaspoti kuwa hajipi presha kwa sasa, lakini hajiondoi kwenye vita hiyo kwani lolote linaweza kutokea na nafasi bado iko wazi kwa kila mchezaji atakayetumia vyema nafasi anazopata uwanjani.

“Siku zote nacheza kwa ajili ya timu, iwe nimefunga au sijafunga, lakini kama mshambuliaji ni lazima uwe na namba nzuri. Ukiangalia pale kwenye kuwania kiatu njia bado iko wazi japo ni mapema sana. Mimi siwekei mawazo hayo nafikiria zaidi kuipambania timu yangu,” alisema Chikola.

“Lakini kwa kila nafasi nitakayopata nitahakikisha naitumia vizuri kwa kufunga, kutoa pasi nzuri za mabao na kukaba ili kuhakikisha timu inamaliza katika nafasi nzuri. Hayo mabao binafsi tutayajua tukifika huko mwishoni mwa msimu.”

Akizungumzia ubora wa kikosi msimu huu, alipongeza viongozi wa klabu kufanya usajili mzuri wa wachezaji nyota wa kimataifa na wenye uzoefu mkubwa ambao wanaisaidia timu na wachezaji wazawa kufanya vyema.

“Ukiangalia timu yetu imekamilika makipa wazuri, mabeki wa kati bora na wazoefu mpaka safu ya mbele kina Makambo (Haritier) na Yacouba (Songne) wameshacheza mashindano makubwa. Usajili mzuri umeleta mafanikio haya kwa sababu mpira ukishaweza hapo basi kupata matokeo siyo kitu kigumu,” alisema Chikola.

Related Posts