Arusha. Chama cha Madaktari wa Wanyama Tanzania (TVA), kimeiomba Serikali kuajiri madaktari wapya wa wanyama ili kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa hatarishi, hasa yale ya milipuko na yanayosambaa kimataifa.
Akizungumza leo Jumanne Desemba 3, 2024 katika kongamano la 42 la wanachama wa TVA lililohudhuriwa na wajumbe 2,000 kutoka Tanzania na nchi za Jumuiya ya Madola, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Esron Karimuribo amesema upungufu wa madaktari wa wanyama unaathiri juhudi za kujitosheleza kwa mazao ya mifugo na fursa za kushiriki soko la kimataifa, kulingana na vigezo vya Shirika la Biashara Duniani (WTO) na Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH).
Profesa Karimuribo amesema nchi ina madaktari wa wanyama 1,300 pekee, huku kukiwa na pengo la madaktari 258 katika mikoa, wilaya, wizara, taasisi za wanyamapori na mashamba ya majeshi.
“Mikoa ya mipakani kama Kagera, Mwanza, Mara na Kigoma haina madaktari wa wanyama wa mikoa, hali hiyo inadhoofisha juhudi za kudhibiti wa magonjwa ya wanyama,” amesema.
Ameongeza kuwa, kuzibwa kwa pengo hilo kwa kushirikiana na sekta binafsi, kutaisaidia Tanzania kutokomeza magonjwa ya wanyama, kuimarisha uzalishaji na kuhakikisha usalama wa biashara ya mazao ya mifugo ndani na nje ya nchi.
Waziri wa Mifugo, Abdallah Ulega aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kongamano hilo, ameahidi kufikisha maombi ya TVA kwa Rais.
“Nimemwakilisha Rais Samia hapa, nitamjulisha kuhusu ombi lenu, kama ambavyo Serikali inaajiri watumishi wa sekta nyingine,” amesema Waziri Ulega.
Pia, amesisitiza umuhimu wa wataalamu wa ndani kushirikiana na wenzao kutoka Jumuiya ya Madola kubadilishana uzoefu na utafiti.
Akisoma hotuba ya Rais Samia, Ulega amesema Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya mifugo kutoka Sh47 bilioni hadi kufikia Sh460 bilioni na imetenga Sh28.1 bilioni kwa ajili ya kampeni ya chanjo dhidi ya magonjwa yanayowaathiri ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku wa kienyeji.
Amesema kampeni hiyo itajumuisha chanjo za muda mfupi kwa mifugo milioni 1.9 ya ng’ombe, mbuzi, kondoo milioni 2.9 na kuku milioni 40 na fedha zingine zitatumika kwa ajili ya ajira za wataalamu wa muda, 3,540.
Awali, akizungumza katika kongamano hilo, Katibu Msaidizi wa TVA, Caroline Eliona amesema kauli mbiu ya kongamano hilo isemayo: “Tokomeza magonjwa ya mifugo ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuimarisha biashara ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi,” inalenga kuisaidia Tanzania kufikia utoshelevu wa mazao salama ya mifugo na kuchangamkia fursa za masoko ya kimataifa.
Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inaonyesha mahitaji ya nyama nchini ni tani milioni 290, huku uzalishaji ukiwa asilimia 30 pekee.
Mahitaji hayo yanatarajiwa kuongezeka hadi tani milioni 480 ifikapo mwaka 2030 kutokana na ongezeko la idadi ya watu, hali inayoonyesha umuhimu wa kudhibiti magonjwa ya mifugo.