Baba asimulia mwenyekiti UVCCM alivyouawa

Mbeya. Adalas Mwijagege, baba mzazi wa Michael Kalinga ali, mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Tawi la Machinjioni, Chunya mkoani Mbeya amesema anaviachia vyombo vya dola kubaini waliohusika na mauaji ya mwanaye.

Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumanne, Desemba 3, 2024 na mwili wa kijana huyo umekutwa katika Kata ya Mkola.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa amesema wamepata taarifa za mauaji ya Kalinga na wanaendelea kuzifanyia kazi.

Wakati tukio hilo likitajwa mwendelezo wa matukio wa wanasiasa, wafanyabiashara na wanaharakati kutekwa, kuuawa na au kupatikana wakiwa wamejeruhiwa, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga amesema kifo hicho hakihusiani na masuala ya kisiasa, bali ni mauaji kama yalivyo mengineyo.

Amesema kufuatia tukio hilo polisi wanamshikilia mtu mmoja ambaye alikuwa na marehemu kabla ya kufikwa na mauaji kwa ajili ya mahojiano na kuwa vyombo vya ulinzi na usala vipo kazini na wahusika watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali.

“Kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa hatukupokea kero wala malalamiko yoyote, hata marehemu hatujapata kesi yake ya mgogoro na yeyote. Alikuwa mchoma nyama na mwimba kwaya kanisani kwake, hivyo wanaohusisha mauaji hayo na siasa si sahihi, ni mauaji kama yalivyo mengineyo na tunaendelea na uchunguzi” amesema Batenga.

Mwijagege ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha TLM Kata ya Makongorosi amesema, mwanaye alikuwa mjasiriamali wa kuchoma nyama katika Mji wa Makongorosi, eneo maarufu la Pub ya MJ.

Amesema jana Jumatatu saa 3:00 usiku kijana huyo alipigiwa simu na watu wasiojulikana ambao walimweleza wanauza mbuzi na aliwaaga wafanyakazi wake na kuondoka na binti mmoja (jina limehifadhiwa) kwa pikipiki yake.

“Aliwasha pikipiki na kumpakia binti huyo na kuelekea eneo aliloelekezwa.”

Mwijagege amesema walipofika kwenye eneo la Mianzini kuna pori la miti mirefu, kijana huyo alijisikia haja ndogo, aliposimama kujisaidia ndipo walipo jitokeza watu wasiojulikana na kumshambulia kwa vitu vyenye ncha kali na kusababisha umauti.

“Kwa maelezo ya binti aliyekuwa na marehemu, watu hao walikuwa wawili walioziba macho na kuwa wakiwa kwenye purukushani, kijana huyo alipiga mayowe ya kuomba msaada,” amesema Mwijagege.

Amesema binti huyo ambaye pia alipiga kelele, amesema walimkamata na kumfunga kamba kisha kwenda kumtupa jirani na mji Makongorosi pembezoni mwa barabara.

Amesema baada ya kufanikiwa kujitoa kwenye Kamba, binti huyo alikwenda kutoa taarifa za tukio hilo kwa wafanyakazi wa marehemu ambao walikwenda kutoa taarifa polisi. Binti huyo aliwaongoza hadi eneo la tukio ambapo mwili ulichukuliwa na umehifadhiwa Hosptali ya Wilaya.

Kuhusu maisha ya mwanaye, baba huyo amesema alikuwa ni kijana asiye na makuu, mpenda watu katika jamii hususani kwenye nafasi ya mwenyekiti wa UVCCM aliweza kufanya vizuri kukipigania chama.

“Kimsingi nimeumia sana, naona akili zangu zinahama na kurejea kwa jinsi walivyomtenda vibaya kijana wangu, kama walikuwa wana shida ya pesa, pikipiki na simu wangechukua lakini si uhai wake,” amesema.

Mwijagege amesema marehemu ameacha mke na watoto watatu akiwepo wa miezi mitatu, jambo ambalo kama familia limewapa kitendawili.

Diwani wa Makongorosi, Kassim Yohana amesema mbali na mauaji ya kijana huyo, hilo ni tukio la tatu kwa mwaka huu la watu kuuawa kwa kushambuliwa na watu wasiojulikana.

“Tunaomba Jeshi la Polisi liongeze nguvu kwenye kata ya Makongorosi kwani hali imekuwa mbaya, kuna matukio ya mauaji ya kutisha ambayo yanahusisha vijana wadogo, ambao ni nguvu kazi kwa Taifa,” amesema.

Katibu Mwenezi CCM Kata ya Makongorosi, Zakayo Kapama amesema taarifa hizo zimezua taharuki kutokana na maisha ya marehemu ndani ya chama na kwenye jamii aliyoishi nayo.

Amesema kwa sasa wameliachia Jeshi la Polisi kufanya kazi yake na mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumatano Desemba 4, 2024 katika makaburi ya Mkola.

Related Posts