TAAMULI HURU: Upinzani umeshinda uchaguzi wa serikali za mitaa

Leo safu yangu haitajikita kwenye hoja za kisheria, nitajikita kwenye matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa ya kuyadurusu kwa jicho tunduizi, hivyo kuwaonyesha umdhaniye ndiye, siye na usiyemdhania ndiye. Mshindi wa jumla ni CCM, hivyo chereko chereko za ushindi ni kwa CCM, aliyeshindwa jumla ni upinzani, wamebaki wanalialia kuhusu figisu na faulo walizochezewa.

Sasa uchaguzi wa serikali za mitaa umekwisha, japo CCM ndiye mshindi wa jumla, upinzani umeshindwa jumla, ukweli ni kuwa CCM ndio imeshindwa kwa sababu imepoteza na upinzani ndio umeshinda kwa kutumia kigezo cha kizungu kinachoitwa “gainers and losers”, waliopata na waliopoteza, CCM ndio wamepoteza, upinzani ndio wamepata.

Tuanze na kanuni ya asiyekubali kushindwa sio mshindani, sote tunakubaliana uchaguzi umekwisha, sasa ni wakati wa kujenga nchi na nashauri tuutumie udhaifu na upungufu ya uchaguzi huu wa serikali za mitaa kama shamba darasa la uchaguzi mkuu, 2025.

Kwa kadiri miaka inavyokwenda, fani mbalimbali pia zinazidi kuboreka, miongoni mwa fani hizo, ni ya uandishi wa habari, kwa kuongezeka fani ya uandishi wa tawimu (data journalism) ambapo mwandishi anakusanya data na kuzichakata, kisha anabaini habari kutokana na data hizo.

Ukifuatilia matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa kwa juujuu, inaonekana CCM ndio wameshinda na wapinzani wameshindwa, lakini tukizikusanya data za matokeo ya uchaguzi huu na kuzichakata, utabaini CCM, japo ni washindi wa jumla, lakini ndio wameshindwa, na wapinzani ambao kweli wameshindwa, lakini wapinzani ndiyo wameshinda kwa kuipokonya CCM nafasi ambazo CCM ilikuwa inazishikilia.

Kuna msemo wa kizungu usemao, “numbers don’t lie”, yaani namba haziongopi au hazidanganyi, 1+ 1 = 2, hivi ndivyo ilivyo mpaka mwisho wa dunia. Hivyo naomba niwapitishe kwenye matokeo kuwaonyesha CCM imeshinda nini, imeshindwa nini, na wapinzani wameshinda nini na wameshindwa nini, na kitu muhimu zaidi, ni kuwaeleza matokeo haya yana maana gani kwa uchaguzi wa mwaka 2025.

Kwanza, nafasi za mwenyekiti wa kijiji:

CCM imeshinda vijiji 12,150 sawa na asilimia 99.01, wapinzani wameshinda nafasi vijiji 121 sawa na asilimia 0.09. Tukilinganisha na matokeo ya 2019, CCM imepoteza vijiji 121 ilivyokuwa inavishikilia, hivyo wapinzani wameshinda vijiji 121.

Pili, nafasi za mwenyekiti wa mtaa:

CCM imeshinda mitaa 4,213 sawa na asilimia 98.83, wapinzani wameshinda mitaa 50 sawa na asilimia 1.17. Tukilinganisha na matokeo ya 2019, CCM imepoteza mitaa 50 ilivyokuwa inaishikilia, hivyo wapinzani wameshinda mitaa 50.

Tatu, nafasi za mwenyekiti wa kitongoji:

CCM imeshinda vitongoji 62,728 sawa na asilimia 98.26, wapinzani wameshinda vitongoji 2,000 sawa na asilimia 1.74. Tukilinganisha na matokeo ya mwaka 2019, CCM imepoteza vitongoji 2,000 ilivyokuwa inaishikilia, hivyo wapinzani wameshinda vitongoji hivyo 2,000.

Nne, nafasi za wajumbe wa halmashauri ya Kijiji: CCM imeshinda nafasi 229,075 sawa na asilimia 99.31, wapinzani wameshinda nafasi 1,580 sawa na asilimia 0.69. Tukilinganisha na matokeo ya mwaka 2019, CCM imepoteza wajumbe 1,580, hivyo wapinzani wameshinda wajumbe 1,580.

Tano, nafasi za wajumbe wa kamati ya mtaa: CCM imeshinda nafasi 21,148 sawa na asilimia 99.30, wapinzani wameshinda nafasi 150 sawa na asilimia 0.70. Tukilinganisha na matokeo ya mwaka 2019, CCM imepoteza wajumbe 150, hivyo wapinzani wameshinda wajumbe 150.

Ushindi wa jumla wa CCM ni nafasi 329,314 na kupoteza nafasi 3,901 ambazo zimenyakuliwa na upinzani, hivyo kwenye gainers na losers (waliopata na waliopoteza), CCM ndio wamepoteza na upinzani ndio wamepata ukilinganisha na uchaguzi wa 2019. Kila aliyesimamishwa na CCM alishinda, hii inamaanisha, ikitolewa elimu ya kutosha ya uraia, ule mtindo wa Watanzania kuchagua kwa mazoea tu utapungua.

Watu watajengewa uwezo wa kuchagua kwa kufanya kitu kinachoitwa informed decisions, hivyo uchaguzi mkuu wa 2025, wapinzani wakisimamisha wagombea wazuri kuliko wagombea wa CCM kwenye ubunge na udiwani, Watanzania watawachagua, hivyo kupata tena Bunge lenye kambi ya upinzani itakayoisimamia serikali kikamilifu.

Natoa pongezi kwa CCM kwa ushindi mkubwa wa nafasi 329,314 kilioupata katika uchaguzi huu, kwa sababu ina kila sababu ya kushinda. CCM sio tu ni chama cha siasa, ni chama dola. Mwenyekiti wa CCM ndiye Rais wa nchi, mkuu wa nchi, mkuu wa serikali na Amiri Jeshi Mkuu, tunafanya uchaguzi kwenye uwanja tenge, uchaguzi wa Tanzania ni sawa na kugombea kisu cha makali kuwili, huku mgombea mmoja ameshika kwenye mpini, anashindana na wagombea wanaoshika kwenye makali, unategemea nini?

Upinzania ndio unaostahili pongezi za dhati, kuwapokonya CCM nafasi 3,901 ambazo CCM ilikuwa inazishikilia kabla, na sasa zimeshikwa na upinzani. Kushinda ni kushinda tu, kuna raha yake, na kushindwa pia ni kushindwa, kuna maumivu yake, hongereni CCM na wapinzani kwa kushinda, wote mmeshinda, na poleni CCM na wapinzani kwa mlichopoteza, wote mmeshinda na mmeshindwa.

Ushindi huu kwa upinzani unamaanisha, CCM inaweza kushindwa!. Hili ni muhimu sana, inamaanisha wapinzani wakijizatiti kusimamisha wagombea wazuri kila kata, kila jimbo, wanayo fursa 2025.

Nashauri tuutumie upungufu tuliouona kwenye uchaguzi huu kama shamba darasa la chaguzi zijazo, japo ukuaji wa demokrasia ni mchakato, hivyo naendelea kusisitiza, CCM na serikali yake, ina wajibu wa kulea vyama vya upinzani ili vikue na kujenga demokrasia ya kweli. Watanzania ni wamoja na tunajenga nyumba moja, hakuna sababu ya kugombea fito, uchaguzi umekwisha, sasa kazi ni moja, kujenga nchi.

Related Posts