KONA YA FYATU MFYATUZI: Tujifunze ya uchaguzi mkuu kwa Botswana

Hivi karibuni Botswana, inayosifika kwa ufanisi kiuchumi na ubora na ugwiji katika demokrasia na utawala bora, kwa mara ya kwanza tangu ipate uhuru mwaka 1966, imekibwaga chama kilicholeta uhuru na kuchagua upingaji baada ya kukichoka kilicholewa maulaji hadi kikajisahau kisijue kinaweza kusahaulika kama wenzake kule Kenya, Malawi na Zambia.

Kwanza, nikiri. Nilitamani nasi tujifunze kitu hapa. Akihojiwa na redio moja ya kwa mzee Madiba, Kiboko mwana wa Duma mnene mpya wa Botswana aliniacha hoi hadi nikamtwangia simu ingawa hakupokea.

Alikuwa bize japo baadaye tulichonga mambo makubwa ambayo ni siri kubwa. Huyu dogo nilimfundisha sheria pale Chuo Kikuu cha Harvard zama zile nikifundisha kwa Joji Kichaka kabla ya kuingia Tarampu na taarabu zake za shari, nikaamua kutimua nisifanye kitu mbaya nikafungwa bure. Tuyaache.

Pili, chama twawala kililiwa na wapigakura kiasi cha kudondoka kifo cha mende au kunguni kama si chawa kisiamini. Uzuri wa siasa za kiTswana, katika uchaguzi, hakuna kuchakachua, kutishana, kukamata wapingaji wala kuwateka au kuwapoteza. Hakuna uhuni wa aina yoyote.

Ukibwagwa, kama kwa Joji Kichaka, unamtwangia mpinzani wako na kumpongeza bila mikiki wala kasheshe kama kule kwingine ambako vyata tawala, ima vinabakia ulajini kwa kuchakachua, kunyamazisha au kuwanunua baadhi ya wapingaji, kuongopea wapika kura ya kula, kutangaza matokeo ya urongo na upuuzi mwingine.

Mfano mzuri ni kule kwa akina Njomba. Felihumo kimeminywa kiasi cha kujikuta kikikumbana na maandamano ambayo hadi leo hatujui yataicha hiyo kaya kwenye hali gani. Hivyo, Botswana imepata rais wa kwanza aliyezaliwa baada ya uhuru.

Sasa tuangalie tunajifunza nini kutoka Botswana. Mosi, upingaji unaweza kuongoza kaya. Rais wa Botswana anasema waziwazi kuwa yeye ni fyatu anayetenda makosa, anayetaka kaya iwe na upingaji wa kutosha ili kumkosoa akifanya makosa akiwa mtumishi wa mafyatu na si mtumikishaji wa Mafyatu.

Pili, alitaka kuunda baraza la mawaziri kumi, wataalamu wakamkatalia, akaamua kuunda la mawaziri 18.

Tatu, Boko ni fyatu anayesema wazi kuwa sirkal yake lazima iogope mafyatu na siyo mafyatu kuiogopa, kwani sirkal yoyote inayoogopwa au kuogopesha mafyatu yake lazima iwaibie na kuwaonea. Pia, aliongeza kuwa kama sirkal ikiwaogopa wanene wake hawawezi kuwaibia njuluku kama kwenye kaya ambapo mafyatu wanaogopa sirkal.

Nne, Rais Boko anasema waziwazi kuwa sirkal yake lazima ishirikishe mafyatu na siyo kuwatenga, huku ikiwakamua na kukusanya njuluku na kuanza kuzitapanya itakavyo kwa wanene wachache kuteuana na kula kila kitu huku mafyatu wakiendelea kusota.

Tano, huyu dogo Rais Kiboko mwana wa Duma anasema wazi kuwa anataka kurejesha madaraka kwa mafyatu kwenye kile anachosema ni kuondoa uungu au to demystify power kwa Kinyakyusa. Anasema yeye ni fyatu na si muungu wala hana akili wala nguvu yoyote kuliko yeyote, bali ni mtumishi wa mafyatu. Nilipomuuliza kama anaweza kuwa mbeba maono, alicheka sana na kusema niache utani. Yeye alisema maono ya kaya yako kwenye katiba na mipango ya kaya na siyo kwenye kichwa wala moyo wa rahis.

Sita, alionya kuwa kuna uwezekano wa kupunguza marupurupu na mishahara ya wanene na matumizi mabovu ya kichoyo, roho mbaya, na uroho. Kama hayati Magu, anataka kupiga marufuku utanuaji na uzururaji wa wanene kupenda kwenda majuu bila sababu. Anasema wazi kuwa kama Watswana watahisi kuna sehemu amekosea, wasichelewe wala kuomba ruhusa kuingia mitaani.

Anasema kuwa kiongozi bora na anayejiamini, haogopi maadamano wala kukosolewa. Hahitaji kusifiwa wala kuabudiwa zaidi ya kuambiwa ukweli tena mchungu ili, kama fyatu yeyote, ajirekebishe kabla ya kuadhibiwa na mafyatu waliompa ulaji. Ameonya kuwa atakayemsifia atampuuza na kumuona kama adui anayetaka kumtia majaribuni ili baadaye wapika kura ya kula wambwage kama chata tawala.

Saba, dogo Boko ameahidi kupambana na ufisi na ufisadi kulhali. Kwani, anasema lazima sheria ipambane na mafisadi na wala rushwa, wezi, mijambazi na wengine kwenye sirkal iwe yake au ile aliyoibanjua bila huruma au kumtafuta mchawi bali kutenda haki.

Nane, aliniacha hoi aliposema kuwa atajenga uhusiano wenye siha na wapinzani wake ili kujiona kuwa kuondoka maulajini si tishio kwa yeyote. Aliongeza kuwa naye alikuwa mpingaji ambaye sasa ni munene wa kaya na ndiyo maana aliwaalika wapingaji wengi toka barani ili kuonyesha kuwa nao wanaweza kuingia kwenye maulaji. Pia, alitaka kuonyesha kuwa upingaji siyo kinyume cha sheria, bali takwa la kikatiba ambalo hakuna anayepaswa kulivunja au kulifanya kuwa hisani.

Tisa, kwenye kuapishwa kwake alikaribisha na wapingaji ili kutoa somo kuwa hakuna haja ya kuumizana kwa vile hata wapingaji wanaweza kutwaa ulaji, hasa ikizingatiwa kuwa uongozi wa mafyatu si ufalme wala mali ya família kama kwa akina M7 pale na kwingineko. Kumi na mwisho alipendekeza wanene wa Afrika wawe wanakosoana badala ya kungoja kukaripiwa na watasha kama vichanga.

Related Posts