Wanafunzi wa kike TPC wafaidika na juhudi za kiwanda cha sukari

Na Safina Sarwatt, Kilimanjaro

Wanafunzi 68 wa kike katika Shule ya Sekondari ya TPC mkoani Kilimanjaro wamepata afueni kubwa baada ya kiwanda cha sukari cha TPC kukamilisha ujenzi wa bweni jipya. Hatua hii imetatua changamoto ya kutembea umbali wa kilomita 20 kwenda na kurudi shuleni kila siku, hali iliyokuwa ikihatarisha usalama wao na kuathiri masomo.

Bweni hilo jipya, lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 68, limegharimu Shilingi milioni 147 na linatarajiwa kuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto za usafiri kwa wanafunzi wa kike, ambao hapo awali walilazimika kusafiri kupitia mashamba makubwa ya miwa huku wakikumbana na hatari mbalimbali.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Sukari TPC anayeshughulikia masuala ya utawala, Jaffari Ally, alisema kuwa kiwanda hicho kimekuwa kikitenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya shule zinazozunguka kiwanda hicho kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii (CSR).

“Mazingira yalikuwa hatarishi kwa watoto wa kike. Kutembea umbali wa kilometa 20 kila siku kulikuwa kunawaweka hatarini kwa sababu ya uchovu, vishawishi, na hata ukatili wa kijinsia. Bweni hili litasaidia wanafunzi kujikita zaidi katika masomo yao bila hofu ya safari ndefu,” anasema Ally.

Anafafanua zaidi kuwa, shule za sekondari za TPC na Chewe zilianzishwa kutokana na mahitaji makubwa ya elimu katika eneo hilo.

Hata hivyo, changamoto ya usafiri iliendelea kuwa kikwazo kwa watoto wengi wa kike, ambapo juhudi za awali za kukodisha mabasi ziligonga mwamba kutokana na wazazi wengi kushindwa kuchangia gharama za usafiri.

“FTK iliamua kuwekeza katika ujenzi wa bweni hili ili kuwezesha watoto wa kike kusoma katika mazingira salama. Tunafurahi kuona juhudi hizi zikileta mabadiliko makubwa,” aliongeza Ally, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Foundation for Community Transformation in Kilimanjaro (FTK).

Maktaba mpya ya kisasa

Mbali na ujenzi wa bweni hilo, kiwanda cha TPC pia kimefadhili ujenzi wa maktaba ya kisasa yenye maabara ya kompyuta, kwa gharama ya Shilingi milioni 126. Maktaba hiyo inaweza kuhudumia wanafunzi 48 kwa wakati mmoja.

“Maktaba hii itakuwa na vifaa vya kisasa, lakini bado tunahitaji TZS milioni 25 kukamilisha mahitaji yote ya thamani. Tunatoa wito kwa wadau mbalimbali kuungana nasi kufanikisha hili,” alisema Ally.

Wanafunzi waelezea mabadiliko

Gladines Kimaro, mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, alieleza jinsi changamoto za awali zilivyokuwa zikitatiza masomo yao.

“Kuchelewa kufika shule kulituathiri sana. Wakati mwingine tulikosa vipindi vya asubuhi au kurubuniwa njiani na madereva wa bodaboda. Bweni hili limetupa matumaini mapya na tunaahidi kufanya vizuri zaidi katika masomo yetu,” alisema Kimaro.

Aliongeza kuwa kutembea umbali mrefu kulisababisha baadhi ya wanafunzi, hasa wa kike, kukatisha masomo kutokana na uchovu na vishawishi njiani.

Faida kwa shule

Mkuu wa shule ya sekondari ya TPC, Mwalimu Salehe Shaban, alisisitiza kuwa ujenzi wa bweni hilo ni hatua muhimu katika kuinua viwango vya ufaulu shuleni hapo.

“Kabla ya bweni, kiwango cha utoro kilikuwa juu, hasa kwa watoto wa kike. Tulikuwa tukikuta wengine wamejificha maporini kwa hofu ya kuadhibiwa kwa kuchelewa shuleni. Sasa tuna matumaini makubwa ya kuboresha ufaulu,” alisema Mwalimu Shaban.

Bweni hilo linatarajiwa si tu kusaidia kuboresha elimu, bali pia kuhakikisha usalama na maendeleo endelevu kwa watoto wa kike katika shule hiyo.

Hatua za kiwanda cha TPC kujenga miundombinu ya elimu zimepongezwa kama mfano bora wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, zikiwa na lengo la kusaidia maendeleo ya kitaaluma na kijamii kwa wanafunzi wa kike.

Related Posts