Tumaini jipya kwa watu wenye ulemavu Tanzania

Dar es Salaam. “Ni Tumaini jipya. Ni kauli za watu wenye ulemavu nchini Tanzania baada ya kuanza kutumika kwa mipango madhubuti ukiwemo wa kitaifa wa haki na ustawi wa watu wenye ualbino (MTHUWWU).

Pia, mkakati wa Taifa wa teknolojia saidizi kwa wenye ulemavu katika kuwapa fursa na haki. Mipango hiyo imetaja nguzo kuu nne za kuwalinda, kulinda utu na ustawi wao ili kupata fursa sawa na wengine.

Nguzo hizo ni kukinga, kuzuia, usawa na kutobaguliwa sambamba na uwajibikaji. Mipango hiyo imezinduliwa jana Jumanne, Desemba 3, 2024 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko.

Wengi wao wanaamini kama itatekelezeka na si kuishia makabatini, inakwenda kuwapa tumaini jipya wakiondoka kwenye hofu ya kuuwawa, kukosa ajira, elimu, vifaa saidizi na huduma za vifaa kinga kwenye afya zao tofauti na awali ambavyo ilionekana wanafanyiwa hisani, lakini sasa ni muongozo ambao upo kimaandishi.

Meneja programu wa chama cha watu wenye ualbino Tanzania (TAS), Salehe Bukano amesema mpango huo kuwa kimaandishi, kinahofuata ni utekekezaji.

Katika mpango huo ambao kwa wenye ualbino umeanisha kuwepo kwa usawa, uwajibikaji na kutobaguana, Bukano amesema kwenye uwajibikaji ni jukumu la Serikali na taasisi nyingine kuwalinda, kuzuia na kuwakinga.

“Mfano kwenye afya, sisi wenye ualbino tunakabiriana na saratani ya ngozi, mwanzo kupata mafuta kinga ilikuwa kama hisani, mtu aamue tu na kutoa msaada, lakini sasa ipo kimaandishi,” amesema.

Mpango huo pia umeainisha haki ambazo Bukano ambaye pia ni mwanasheria amesema wenye ualbino wana haki zao, ikiwamo ya kuishi.

“Kuna watu walikuwa wakituua na kutukata viungo vyetu kwa imani za kishirikina, mpango huu umetaka watu wa usalama kuchunguza na kuwafikisha mahakama, pia wameshiriki katika mpango huu, hivyo inaonyesha ni namna gani unakwenda kutusaidia,” amesema.

Mmoja wa watu wenye ualbino, Maua Salim amesema mpango huo umewapa tumaini jipya, kwani awali changamoto walizopitia ziliwapa mateso.

“Tunaamini sasa tunakwenda kupata mazingira rafiki katika ustawi wetu na unatuondoa kwenye athari ya kubaguliwa na kunyanyapaliwa,” amesema.

Amesema jamii haipaswi kuona kuwa albino ni mkosi na badala yake watambue nao ni binadamu huku akiwasisitiza wenzake kuwa na wajibu wa kujitunza.

“Serikali imetimiza wajibu wake, lakini pia suala la usalama wetu, sisi pia tunapaswa kujilinda, sio kwa kuwa mpango umezinduliwa ndio utembee usiku, hapana,” amesema.

Kwenye mpango wa vifaa saidizi kwa wenye ulemavu, katibu wa shirikisho la watu wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata), Jonas Lubago amesema ule ucheleweshwaji wa mambo na mtu kufanya vitu kwa utashi umefikia tamati.

“Kikubwa ni mipango kufanyiwa utekelezaji, haya ndiyo yalikuwa matamanio ya wenye ulemavu,” amesema.

Mhasibu wa TAS, Abdillah Omar amesema awali vitu vingi kuwahusu wao vilifanyika kwa utashi, lakini sasa vinafanyika kimaandishi.

“Tunakwenda sasa kuwa ulemavu ni hali ya kuonekana na sio kimazingira,” amesema.

Akizindua mipango hiyo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema ulemavu usitumike kunyanyapaliwa.

“Serikali inatekeleza mipango mikakati mbalimbali ya kuwaletea maendeleo, sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama.

“Hakuna anayepanga kuwa na ulemavu, unakuja kwa kuzaliwa, maradhi au ajali na unaweza kutokea kwa mtu yoyote,” amesema Dk Biteko akieleza tathimini ya watu wenye ulemavu nchini akibainisha kaya 110,000 zinaishi na watu wenye ulemavu nchini.

Katika kukazia kwamba kundi hilo lina haki na fursa sawa, Dk Biteko anasema wenye ulemavu wengi wana uwezo mkubwa katika kazi na wapo ambao ni viongozi wakubwa.

Akieleza maagizo ya waziri mkuu, kuhusu mipango hiyo, amesema anataka wakuu wa mikoa kusimamia mpango wa wenye ualbino kuhakikisha inatekelezwa ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mafuta kinga na kuwasajili kwenye kanzi data watu wenye ulemavu.

“Katika teknolojia saidizi, waziri mkuu ameagiza kila halmashauri kutenga bajeti ya vifaa saidizi na viwanufaishe wanafunzi.

“Kuna vifaa saidizi vinanunuliwa visivyo na ubora na wenye ulemavu wanagawiwa na watu tena kwa kupiga na picha baada wiki mbili vinaharibika, hivyo basi ubora wa vifaa hivi uzingatiwe,” amesema akisisitiza Tamisemi isimamie na kuratibu kwa kila mkoa dhima na malengo yaliyokusudiwa kwa wenye ulemavu na ualbino.

Awali, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye walemavu), Ridhiwani Kikwete amesema mpango wa wenye ualbino ni wa mwaka 2024/25 hadi 2028/29 na ule wa teknolojia saidizi ni wa mwaka 24/27.

Amesema mpango huo unakwenda kuondoa unyanyapaa, kuboresha ulinzi wao na fursa na kuwa na jamii inayoheshimu haki ya watu wenye ualbino na kuendeleza haki ya maisha. Pia utashughulikia changamoto za wenye ulemavu, ikiwamo ukatili na unyanyasaji.

Related Posts