Namibia yapata Rais wa kwanza mwanamke – DW – 04.12.2024

Ushindi huo unamfanya Nandi-Ndaitwah kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika taifa hilo la Kusini Magharibi mwa Afrika. Matokeo yaliyotangazwa Jumanne na tume ya taifa ya uchaguzi ya Namibia yanaonesha kuwa makamu wa Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah ameshinda katika uchaguzi huo kwa kupata asilimia 58 ya kura zilizopigwa baada ya zaidi ya asilimia 91 ya kura kuhesabiwa.

Mpinzani mkubwa wa makamu huyo wa rais, Panduleni Itula wa chama cha IPC ameshika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro hicho kwa kupata asilimia 25 ya kura.  Hata hivyo Itula alishaulalamikia uchaguzi huo kutokana na na dosari zilizojitokeza.

Soma zaidi: Ucheleweshaji wa kura Namibia wazusha hasira

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi ya Namibia, chama tawala cha SWAPO kimefanikiwa pia kupata wingi wa viti bungeni na kuendeleza utawala wake wa miaka 34 tangu nchi hiyo ilipopata Uhuru mwaka 1990. Chama hicho kimekuwa kikikosolewa kwa ukuaji duni wa uchumi, kushindwa kufanya uwekezaji katika huduma za jamii na sekta ya afya pamoja na tatizo la rushwa.

Netumbo Nandi-Ndaitwah anakabiliwa na changamoto za uchumi na ukosefu wa ajira

Mshindi wa nafasi ya Rais kupitia SWAPO Nandi-Ndaitwah mwenye miaka 72 amesema kuwa baada ya ushindi atajikita kupambana na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kuwekeza zaidi katika nishati ya kijani, na miundo mbinu katika muhula wake wa miaka mitano ya uongozi. 

Akifafanua namna ya kukabiliana na baadhi ya changamoto wakati wa kampeni zake aliahidi kutengeneza nafasi zaidi za ajira kwa kuvutia uwekezaji kwa kutumia diplomasia ya uchumi.  

Uchaguzi wa Namibia, 2024
Uchaguzi wa Namibia 2024Picha: Jasko Rust/DW

Uchaguzi huo uliofanyika Jumatano iliyopita uligubikwa na upungufu wa karatasi za kupigia kuwa na changamoto nyingine zilizosababisha muda wa kupiga kura uongezwe hadi Jumamosi. Tume ya taifa ya uchaguzi ya Namibia ilikiri mapungufu hayo na mengine katika kuratibu uchaguzi huo likiwemo la kupata moto kupita kiasi kwa vishkwambi vilivyotumiwa kuwaandikisha wapiga kura.

Vyama vya upinzani vilidai kuwa kurefushwa huko kwa muda ni kinyume cha sheria na vimeahidi kuungana kutaka uchaguzi huo ubatilishwe.

Karibu wananchi milioni 1.5 kati ya raia karibu milioni tatu wa nchi hiyo walijiandikisha kushiriki kupiga kura katika uchaguzi wa wiki iliyopita.

 

Related Posts