Hitilafu ya umeme yaikwamisha treni ya SGR, huduma zarejea

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema treni zake za mwandokasi zilizokuwa zinasafiri kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma zilisimama kwa muda kutokana na hitilafu ya umeme katika mifumo ya Gridi ya Taifa.

Taarifa ya hitilafu hiyo iliyotokea leo Jumatano, Desemba 4, 2024 awali ilitolewa Shirika la Usambazaji Umeme Tanzania (Tanesco), kupitia mitandao yake ya kijamii likisema:

“Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linautaarifu umma kuhusu hitilafu iliyojitokeza katika mfumo wa Gridi ya Taifa leo, Desemba 4, 2024 saa 04:03 asubuhi, hitilafu hiyo imepelekea mikoa inayopata umeme katika Gridi ya Taifa kukosa umeme. Wataalamu wetu wanaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha hitilafu hiyo.”

Taarifa ya TRC iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Fredy Mwanjala imeeleza: “Abiria walioathirika kufuatia hitilafu hiyo ya umeme, ni wale walioanza safari yao saa 2:00 kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, abiria wa treni ya saa 3:30 kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na abiria waliotoka na treni ya saa 3:50 kutoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.

“Kufuatia jitihada zilizofanyika, umeme ulirejea saa 5:30 asubuhi na safari kurejea kama kawaida. Shirika linawaomba radhi abiria kwa usumbufu uliojitokeza.”

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts