Moshi. Glory Mallya, mtoto wa marehemu Isaack Mallya (72), aliyeuawa nyumbani kwake kijijini Umbwe Onana, Wilaya ya Moshi, Kilimanjaro na watu wasiojulikana, ameeleza aliyozungumza na baba yake siku moja kabla ya kifo chake.
Desemba 2, 2024, mwili wa Mallya ulikutwa nje ya nyumba yake ukiwa na majeraha mwilini, huku jicho moja likiwa limetobolewa.
Glory, mtoto wa tatu wa familia ya marehemu akizungumza na Mwananchi Digital jana Jumanne, Desemba 3, 2024 baada ya maziko ya baba yake, amesema walipanga mipango ya kuonana wakati wa sikukuu ya Krismasi.
Glory amesema Jumamosi iliyopita baba yake alimpigia simu kumsalimia na kumsisitiza waombeane kwa ajili ya kuonana wakati wa Krismasi.
“Aliniambia salimia kila mtu, salimia wajukuu zangu na alionekana kuwa na matumaini ya kukutana nasi mwisho wa mwaka,” amesema mtoto huyo.
Hata hivyo, anasema siku iliyofuata alipokea taarifa kutoka kwa kaka yake akimtaarifu kuhusu kifo cha baba yao.
“Amekufa kifo cha kikatili sana, hata kama alikuwa na makosa labda kuna mtu alimfanyia, lakini hakustahili kuuawa kikatili vile,” amesema Glory kwa uchungu huku akibubujikwa machozi na kuongeza:
“Ni tukio ambalo limetuumiza sana kwa sababu siku moja kabla tulizungumza naye mambo mengi kwa kirefu kuhusu mipango ya familia kuelekea Krismasi.”
Amesema ni kawaida yao kila ifikapo mwisho wa mwaka, familia nzima kukutana nyumbani kwa baba yao kusherehekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya.
Amesema lengo la baba yake kumpigia simu ilikuwa akimuuliza wamejipangaje na ndugu zake kwa ajili ya sikukuu hizo.
“Yote tuliyozungumza na baba, hayapo tena, ameuawa kinyama,” amesema Glory.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema mpaka jana jioni watu watatu walikuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za mauaji hayo.
“Bado tunachunguza chanzo cha tukio hili na tunaendelea kuwahoji watuhumiwa ili kubaini ukweli,” amesema Kamanda Maigwa.
Familia yasisitiza haki itendeke
Kaka wa marehemu, Patrick Boisafi ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, amesema familia itashirikiana na polisi kuhakikisha haki inatendeka.
“Tukio hili limetuhuzunisha sana kama ukoo. Tutaendelea kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha waliohusika wanachukuliwa hatua kali,” amesema Boisafi.
Akizungumzia mauaji hayo,Padri Antony Marunda wa Jimbo Katoliki la Moshi, amesema hali hii inaonyesha ni namna gani maadili yanavyozidi kuporomoka ndani ya jamii, kiasi cha watu kutokuwa na hofu ya Mungu.
Hivyo, amehimiza jamii kuacha matendo ya kikatili na kuishi kwa kuzingatia maadili, huku wakimtanguliza Mungu mbele kusudi wasikengeuka na ulimwengu.
“Ukatili kama huu unapaswa kukemewa kwa nguvu zote. Tunahitaji mshikamano wa viongozi wa dini na Serikali kuhakikisha tunatokomeza uovu katika jamii,” amesema Padri Marunda.
Amevihimiza vyombo vya dola kuhakikisha vinawakamata wote waliohusika na mauaji hayo na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Tunapaswa kusimama imara kama jamii na kuhakikisha matendo kama haya hayatokei tena,” amesema padre huyo.