MARIAM MWINYI :MARADHI YA SARATANI YANAREJESHA NYUMA JUHUDI ZA JAMII

 Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu, na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) Mhe. Mama Mariam Mwinyi amesema maradhi ya Saratani ni hatari na yanarejesha nyuma juhudi za jamii na uchumi hata kusababisha umasikini kwa jamii kutokana na gharama kubwa za matibabu yake kwa wagonjwa wengi kutokuwa na uwezo wa kumudu matibabu.

Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 4 Disemba 2024, Ofisini kwake Ikulu ya Migombani, Mkoa wa Mjini Magharibi alipozungumza na wageni kutoka Hong Kong, Dk. Jeremy Hon, Daktari na Mtaalamu wa maradhi ya Saratani akiambatana na Bi. Angel Hon wa Taasisi ya “Belt and Road Creation Resources” waliofika kumtembelea

Aidha, Mama Mariam aliueleza ugeni huo kwamba ZMBF katika kuisaidia jamii juu ya maradhi hatari ikiwemo Saratani taasisi yake mara kadhaa imekuwa na utaratibu wa kila baada ya miezi mitatu kuweka kambi za matibabu bure Unguja na Pemba kwa Mikoa yote kuisadia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wakuu wa Mikoa kuwaalika wananchi kwaajili ya matibabu na uchunguzi wa afya zao.

Mama Mariam amemualika Dk. Jeremy Hon kuangalia uwezekano wa kuja Zanzibar kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwani Serikali tayari imekamilisha hospitali 10 za Wilaya Unguja na Pemba na moja ya Mkoa pamoja na kuweka miundombinu imara na vifaa vya kisasa vya maabara.

Halikadhalika, Mama Mariam Mwinyi amebainisha kuwa “Tumaini Initiative” umelenga kuzalisha taulo za kike zaidi ya 20,000 kwa mwaka na hadi sasa tayari ZMBF imefanikiwa kusambaza kwa wanafunzi na wasichana zaidi ya 7000 wa skuli za msingi na sekondari kwa Unguja na Pemba.

Kwa upande wao Dk. Jeremy Hon na Mrs Angel Hon wamepongeza juhudi za maendeleo na kazi nzuri inayofanywa na Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” Pia wameeleza shauku yao ya kutaka kuendeleza ushirikiano wao na Zanzibar hasa katika kubadilishana uzoefu kwenye sekta ya Afya ili kupunguza wimbi za maradhi ya Saratani yanayowasumbua wananchi wengi.

 

Related Posts