Wabunge waiangusha serikali Ufaransa – DW – 05.12.2024

Wabunge wanaoelemea mrengo mkali wa kulia na wa kushoto waliungana kuunga mkono hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Michel Barnier, kwa wingi wa kura 331. 

Sasa waziri mkuu huyo anapaswa kukabidhi barua ya kujiuzulu pamoja na serikali yake kwa Rais Emmanuel Macron, hatua inaoifanya serikali yake iliyodumu kwa miezi mitatu kuwa miongoni mwa zile zilizokaa madarakani mwa muda mfupi zaidi tangu mwaka 1958.

Vyama vya mirengo ya kulia na kushoto vimemuadhibu Barnier kwa kutumia kwake madaraka yake maalum ya kikatiba kutekeleza sehemu ya bajeti ambayo haiungwi mkono na umma bila ya kupata idhini ya bunge, ambako serikali yake haina wingi wa kutosha. Rasimu ya bajeti hiyo ilikuwa inataka euro bilioni 60 ili kuziba nakisi. 

Soma zaidi: Serikali ya Ufaransa yakabiliwa na kitisho cha kuangushwa

Kabla ya kura kupigwa, Barnier aliwaambia wabunge kwamba nakisi iliyopo isingeliweza kuondoka kwa hoja ya kumuondowa yeye madarakani, na kwamba serikali yoyote itakayokuja baada yake itakumbwa na tatizo hilo hilo.

Mara ya kwanza serikali kuangushwa

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali kuangushwa kwa kura ya kutokuwa na imani bungeni tangu mwaka 1962. Hatua hii, wachambuzi wanasema, ilichangiwa sana na uamuzi wa Macron kuitisha uchaguzi wa mapema mwezi Juni mwaka huu, ambapo matokeo yake yalikuwa ni bunge lililopasuka likiwa na wabunge wengi kutoka upinzani. 

Ufaransa, Michel Barnier
Bunge la Ufaransa kwenye kikao cha kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Michel Barnier.Picha: Lafargue Raphael/abaca/IMAGO

Kutokana na kuporomoka kwa serikali hii, sasa Ufaransa inaelekea kuumaliza mwaka huu bila serikali madhubuti wala bajeti ya mwaka 2025, ingawa katiba inaruhusu kuchukuliwa hatua maalum ambazo zitaepusha kufungwa kabisa kwa shughuli za serikali kama ilivyo kwa Marekani.

Soma zaidi: Barnier aanza kukabiliana na vizingiti vya kuunda serikali Ufaransa

Kwa upande mwengine, mpasuko wa kisiasa wa Ufaransa utaudhoofisha zaidi Umoja wa Ulaya, ambao tayari unakabiliana na kuporomoka kwa serikali ya mseto nchini Ujerumani, wiki chache kabla ya rais mteule wa Marekani, Donald Trump, kurejea Ikulu ya White House mwezi ujao.

Athari kwa Ukraine

Waziri wa ulinzi anayemaliza muda wake, Sebastian Lecornu, ameonya pia kwamba mpasuko huo unaweza kuathiri msaada wa Ufaransa kwa Ukraine.

Marine Le Pen
Marine Le Pen, kiongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ufaransa.Picha: STEPHANE DE SAKUTIN/AFP

Chama kinachoelemea mrengo mkali wa kushoto, LFI, kimemtaka Rais Macron mwenyewe kujiuzulu.

Soma zaidi: Macron aongeza juhudi za kuvunja mkwamo wa kisiasa

Kiongozi wa mreno mkali wa kulia, Marine Le Pen, ambaye kwa miaka kadhaa amekuwa akikijenga chama chake cha National Rally kama serikali inayosubiri kuapishwa, amesema ingawa hashinikizi kujiuzulu kwa Macron, lakini shinikizo dhidi yake litazidi kukuwa na hatimaye mwenyewe atapaswa kuchukuwa uamuzi huo.

Ikulu ya Elysee imesema Rais Macron atahutubia taifa hivi leo, huku vyanzo vitatu tafauti vikiliambia shirika la habari la Reuters kwamba huenda rais huyo akateuwa waziri mkuu mpya haraka kabla ya Jumamosi.

Related Posts