SIMBA ipo zake Algeria kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika Kundi A dhidi ya CS Constantine utakaochezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Chahid Hamlaoui uliopo Mji wa Constantine.
Katika mechi tano za mwisho, Simba imeshinda zote ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola huku nyingine ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo (3-0), Mashujaa (1-0), KMC (4-0) na Pamba (1-0).
Mbali na Simba kuwa na safu kali ya ushambuliaji, imeonyesha pia kuwa na ngome imara ambayo imeiwezesha kutoruhusu bao katika mechi zote hizo.
Timu hiyo imeruhusu bao moja tu katika mashindano ya kimataifa msimu huu na ilikuwa dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya kwenye kuwania kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba ilipata ushindi wa mabao 3-1 nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kutinga makundi kibabe baada ya ugenini kutoka 0-0.
Kwa upande wa wapinzani wao, takwimu zinaonyesha katika michezo mitano iliyopita ya mashindano yote (nyumbani na ugenini), ukiwamo mmoja wa Kombe la Shirikisho, CS Constantine ambayo inaoongoza msimamo wa Ligi Kuu Algeria imeruhusu mabao matatu na kufunga matano, ina wastani wa 0.6 wa kuruhusu mabao na kufunga ni bao moja kwenye kila mchezo.
Katika michezo hiyo mitano iliyopita, CS Constantine imeshinda mitatu ambapo mmoja ni wa Shirikisho dhidi ya CS Sfaxien kwa bao 1-0 huku mingine ikiwa dhidi ya Olympique Akbou (2-1) na USM Alger (1-0) kwenye ligi yao ya ndani, yote ni kwa tofauti ya bao moja tu. Hivyo inaonyesha sio timu yenye uwezo mkubwa wa kufunga.
Ndani ya michezo yake mitano ya mwisho wikiwa nyumbani tu, CS Constantine imeruhusu bao katika michezo minne, ni mchezo mmoja tu ambao nyavu zao hazikugushwa ambao ni dhidi ya USM Alger.
Wakati CS Constantine ikionekana kuwa ni timu inayofungika kulingana na takwimu za michezo yao mitano iliyopita, Simba inaonekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji ambayo imefunga mabao 10 katika michezo yake mitano iliyopita, ina wastani wa kufunga mabao mawili kwa kila mechi.
Lakini pia rekodi zinaonyesha Simba wamekuwa wagumu kuruhusu bao iwanapocheza ugenini katika michuano ya kimataifa kwa siku za hivi karibuni kitu ambacho kinaweza kuwasaidia mbele ya CS Constantine.
Rekodi za mechi tano za mwisho katika michuano ya kimataifa ikiwa ugenini, zinaonyesha timu hiyo licha ya kuwa wagumu kwenye kuruhusu mabao, lakini bado haina matokeo mazuri ya ushindi ikishindwa hata kufunga bao.
Simba katika mechi tano za mwisho za kimataifa ugenini zikiwamo nne Ligi ya Mabingwa Afrika na moja Shirikisho, imeruhusu mabao matatu, haijafunga bao lolote kwa matokeo ya; Al Ahly 2-0 Simba, ASEC Mimosas 0-0 Simba, Wydad 1-0 Simba, Jwaneng Galaxy 0-0 Simba na Al Ahli Tripoli 0-0 Simba.
Akizungumzia mchezo huo, kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids alisema wanatarajia mchezo mgumu na wenye ushindani lakini ana imani kubwa ya kufanya vizuri licha ya kuwa ugenini.
“Tunatambua kucheza ugenini ni tofauti na nyumbani lakini tupo hapa kwa ajili ya kufanya kila ambacho tutaweza ili kupata pointi ambazo zitatuweka kwenye mazingira mazuri, tutatumia siku chache zilizosalia kuendelea kuufanyia kazi mpango wetu,” alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini na kuongeza.
“Tulipata muda wa kuwasoma wapinzani wetu, tunajua ubora walionao lakini muhimu zaidi nguvu zetu tumeweka katika maandalizi yetu na mpango ambao naamini unaweza kufanya kazi.”
Pia kocha wa zamani wa Simba, Abdelhak Benchikha ambaye hivi sasa anainoa JS Kabylie ya Algeria, amesema Constantine ni timu yenye njaa ya ushindi.
“Wanajua kuutafuta ushindi lakini Simba kama itacheza kikubwa kama alivyowaona ikicheza na Al Ahly Tripoli anaamini itafanya vizuri japo wanatakiwa kuwa na nidhamu ya mchezo.”
Wakati kikosi cha Simba jana kikielekea Algeria, mlinda mlango wa timu hiyo, Aishi Manula alishindwa kuendelea na safari baada ya kupata changamoto ya kiafya.
Taarifa iliyotolewa na Simba, ilisema: “Mlinda mlango Aishi Manula ameshindwa kuendelea na safari baada ya kupata hitilafu ya kiafya dakika chache kabla ya kuanza safari ya kuelekea nchini Algeria tukiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.”
Baada ya Manula kubaki Dar, Simba imesafiri na makipa wawili ambao ni Moussa Camara na Ally Salim.
Nyota wengine ni mabeki Che Malone Fondoh, Karabou Chamoue, Abdulrazack Hamza, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Valentine Nouma na Kelvin Kijili.
Viungo ni Mzamiru Yassin, Debora Fernandes, Fabrice Ngoma, Ladaki Chasambi, Augustine Okejepha, Omary Omary, Edwin Balua, Kibu Denis, Jean Charles Ahoua na Awesu Awesu.
Washambuliaji ni Leonel Ateba na Steven Mukwala.