Wanaharakati Wahimiza Vyama vya Siasa Kuwapa Nafasi Wanawake, Vijana na Walemavu Kugombea Uongozi

VYAMA vya siasa vimetakiwa kuwaamini wanawake,vijana wa jinsia zote,sambamba na walemavu kwa kuwapatia nafasi ya kusimama katika nafasi za kugombea uongozi ili wapate nafasi ya kuchaguliwa na kuongoza.

Tamko hilo limetolewa leo Disemba 04,2024 na Afisa TGNP idara ya ujenzi na nguvu za pamoja Anna Sangai katika semina za jinsia na Maendeleo zinazofanyika kila Jumatano ambapo waliangazia kuhusiana na mchakato mzima wa uchaguzi wa serikali za vijiji na mitaa katika kipengele cha ushiriki wa uchaguzi huo ambapo waligusia kundi la wanaume,wanawake,vijana wa kike na wakiume pamoja na kundi lenye mahitaji maalumu.

Amesema katika suala la uongozi mwanamke ni kama mwanaume anafikra za uongozi kwa sababu ungozi ni busara si misuli hivyo mwanamke akipatiwa nafasi ya kuongoza anaweza kutekeleza majukumu yake kama ambavyo mwanaume angefanya.

“Wanawake wengi walihamasika na wakachukua fomu,Kama unavyofahamu Tanzania huwezi kupata nafasi yeyote lazima upitie kwenye chama cha siasa,kule Kuna changamoto hasa katika kundi la wanawake,watu wenye ulemavu pamoja na vijana wakike na wakiume wamekuwa bado hawaaminiki”Amesema.

Aidha Sangai ameeleza kuwa hata katika hatua za kampeni wakati wa kunadi sera kumekuwa na kasumba ambayo imezoeleka ambapo mwenyekiti wa chama ikitokea mgombea ni mwanamke amekuwa akitoa mtu kwa ajili ya kumsemea jambo ambalo si sawa kwani mwanamke naye anapaswa aaminike.

Kwa Upande wake, Mwanaharakati kutoka kata ya Majohe-Ukonga Jijini Dar es Salaam Bw.Joseph Safari amesema kwa asimilia kubwa ameshuhudia wanawake wakishiriki katika zoezi la kuchagua pekee na sio katika kugombea nafasi za uongozi.

Aidha Safari ameshauri kuwa serikali ikichukua hatua ya kuvihamasisha vyama vya siasa kuunda demokrasia ambayo itakuwa ni ya usawa wa kijinsia kutachagiza mageuzi makubwa na kupatikana wanawake viongozi.

“Serikali ichukue hatua kwa vyama siasa ambavyo vinaonesha bado kuwakandamiza wanawake juu ya mifumo dume ikiwemo rushwa ya ngono,rushwa ya fedha”Amesema.

Sambamba na hayo Safari ameeleza kuwa ili kuwafanya wanawake kuendelea kuhamasika ni pale wanapowaona wenzao wanapata nafasi hizo bila kuhusishwa kwa swala la rushwa.

Nae, Mwanaharakati Levlin Ngugi ameshauri wanawake ambao wanatamani kuwa viongozi kujinoa kabla ya kwenda kushiriki zoezi la kugombea uongozi kwani hakuna chama ambacho kipo taayari kumpatia mtu nafasi ambaye atashindwa.










Related Posts