Klabu za Simba, Yanga na Azam zimepata fursa ya kucheza mechi za kirafiki na klabu za Ligi Kuu ya Russia, pamoja na kuweka kambi katika kipindi cha mapumziko ya ligi.
Fursa hiyo imepatikana kutokana na ziara ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro nchini humo na alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Michezo wa nchi hiyo, Mikhail Degtyarev, Desemba 3, 2024.
Pamoja na fursa hiyo, Ndumbaro amependekeza kuwapo na ushirikiano wa kubadilishana utaalamu katika ngazi ya klabu pamoja na kuwa na michezo ya mara kwa mara ya kirafiki baina ya klabu za ligi mbalimbali za nchi hizo mbili.
Aidha, Waziri Ndumbaro ametembelea ofisi za Bodi ya Ligi Kuu ya Urusi na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mwendeshaji Mkuu wa bodi hiyo, Evgeniy Melezhikov na wamekubaliana kuanzisha ushirikiano baina ya timu za taifa na kuwa na mechi za kirafiki.