NYAKATI ngumu wakati mwingine zinaweza zikabadili tatizo na kugeuka fursa, ndivyo anavyosimulia mshambuliaji wa Kagera Sugar, Tariq Seif anayeshuhudia kupitia kudharauka alipata nafasi ya kucheza Yanga msimu wa 2019/20.
Unataka kujua ilikuaje? Anasimulia msimu wa 2018/19 akiwa Biashara United, hakuwa chaguo la kwanza, hivyo kuna wakati mwingine alikuwa akipewa nafasi ya kucheza, alisindikizwa na neno nenda na wewe kajaribu, kitu kilichokuwa kinautafuta moyo wake kuona pamoja na bidii anayofanya mazoezini haonekani kama ana kitu cha kuisaidia timu.
Kutoonekana muhimu kikosini kulimfanya apate hasira ya kupambana kuhakikisha kocha anamkubali, mechi ya Mei 10, 2019 timu hiyo ilicheza dhidi ya Yanga, Uwanja wa Karume mjini Musoma, ilibadili maisha yake na kupandisha thamani.
Biashara United ilishinda bao 1-0 dhidi ya Yanga, lililofungwa na Tariq akaonekana na viongozi wa Wanajangwani, msimu uliofuatia akasajiliwa.
“Maisha yana changamoto nyingi sana, kama moyo unakuwa mwepesi unaweza ukajikuta unashindwa kuendelea, lakini ukizigeuza changamoto na kuwa fursa njia ya kufanikiwa ipo wazi.
“Kutoka Biashara United ambako nilikuwa naonekana siyo kitu hadi kusajiliwa Yanga, iliongeza thamani ya kazi yangu, ikanifunza kutokata tamaa katika maisha yangu ya upambanaji,” anasema Tariq ambaye msimu uliopita bao lake alilofunga dhidi ya Azam kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi liliingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo za msimu.
Muonekano wa Tariq kwa sasa ni wa kirasta, tofauti na awali ambapo alikuwa anasokota dredi, analielezea kilichomshawishi ni imani ya marasta, utu wao, upendo na kumanisha kila wanalolifanya, tofauti na asilimia ya watu wengi ambao wamejaa unafiki.
Ingawa pamoja na muonekano huo wa kirasta alionao, hujabadilisha kitu chochote kuhusu imani yake ya kislamu, anaswali kama kawaida, lakini msisitizo wake anapenda marasta wamenyooka na mambo.
“Mfano mzuri ni Bob Marley aina ya nyimbo zake ni za kuleta amani, upendo na kupinga vitendo vinavyokinzana na utu, licha ya nguli huyo wa rege kutokuwepo duniani, ila ujumbe wake unaishi katika mioyo ya watu,” anasema Tariq ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao matano, akiwa na Geita Gold.
Anasema kitu alichokuwa anakipenda kukifanya kama asingetoboa katika soka ni ubondia na huwa akipata muda anapenda kwenda kufanya mazoezi hayo katika gym za mabondia mbalimbali.
“Nina watoto watatu Mudhihir (9),Razack (7) na Zaynab ambaye bado ni mdogo,lakini natamani niwapeleke shule za michezo hata mmoja wao akiwa bondia, nitafurahia zaidi.
Anaongeza”Zamani nilikuwa na ndoto za kuwa bondia, ila nilipoona katika soka nafanya vizuri nikaachana na ndoto hiyo, ingawa nikipata muda huwa nafanya mazoezi ya aina hiyo pia napenda Kareti na taikondo.”
Anasema haujawa msimu mzuri kwake, kwanza hapati nafasi kubwa ya kucheza na anamiliki bao moja alilofunga dhidi ya Mashujaa dakika ya 9, kitu kinachomuweka katika dimbwi la mawazo, kama mshambuliaji anatambulika kwa mabao na siyo kitu kingine.
“Japokuwa nafahamu bado nina nafasi ya kuendelea kupambana nisije nikamaliza msimu bila kitu, soka ni kazi yangu ninapoona vitu haviendi sawa lazima sitakuwa sawa,” anasema.
Msimu wa 2019/20 alijiunga na Yanga ambapo alicheza msimu mmoja, anasema kilimuondoa “Baada ya mkataba kumalizika walitaka kunisainisha miaka miwili, lakini hawakutaka kunipa dau la usajili badala yake walitaka waniongezee mshahara kidogo, kwangu ikawa ngumu.
Anaongeza”Mchezo wa soka ni wa muda mfupi, tuna familia ambazo zinatuhitaji kama unakuwa hufanyi vitu vitakavyokusaidia baadaye inakuwa ni changamoto, wakati huo Yanga inataka kunisainisha bila pesa ila nitakuwa napewa mshahara kulikuwepo na timu ambazo zilikuwa tayari kutoa dau la usajili ndio maana niliondoka.”
Anasema kupitia soka amefanikisha kufanya vitu mbalimbali vya maendeleo, ikiwemo na kufanya baadhi ya miradi inayomuingizia pesa.
Anaulizwa hutamani tena kwenda kucheza nje? Anajibu “Msimu huu ilikuwa nicheze Zanaco FC ya Zambia, kuna kitu kilinikwamisha ikabidi nisaini Kagera Sugar, hicho kitu kikikaa sawa, muda wowote naweza nikaondoka.”
Anasema kwa kiwango alichokionyesha beki Kelvin Yondani, akicheza Simba (2006-2012), Yanga (2012-2020) na Taifa Stars, akicheza kikosi cha kwanza panga pangua,anastahili kupewa maua yake, akikiri jambo liloshindwa kufanyika na wachezaji wanaokuja nyuma yake.
Anaongeza”Ukiachana na wachezaji wa zamani ambao tunasimuliwa, Yondani amekuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wengi, kutunza kiwango si jambo jepesi, inahitajika nidhamu, kujitambua na kupenda unachokifanya, aliletewa watu katika nafasi yake bado aliwakalisha benchi, hadi sasa anacheza kwa kiwango kilekile.
“Ukiachana na Yondani ninamkubali Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’ lakini ana kazi ya kumeneji kiwango chake, ili aweze kucheza kwa muda mrefu, kwani umri wake unamruhusu kufanya hayo.”
Anasema kutokana na sayansi na teknolojia, kila anachokifanya mchezaji kinakuwa wazi kama kiwango chake kinakuwa kizuri ni rahisi kutajirika.
“Tunashukuru Ligi Kuu inaonyeshwa, hivyo ni rahisi kuonekana sehemu mbalimbali duniani, ndio maana nasema sisi tunapaswa kupambana kama tunahitaji kufaidi matunda ya vipaji vyetu,”anasema.
Timu alizowahi kuzichezea ni Geita Gold (2023/24),Mbeya City (2022/23), Polisi Tanzania (2020/ 2021, 2021 /22), Yanga (2019/20), Biashara United (2018/19) na Stand United (2017/18).