Watu wenye ulemavu nchini wapaza sauti vikwazo vinavyowazuia nafasi za uongozi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Vyama vya siasa, taasisi za Serikali na jamii zimetakiwa kuondoa vikwazo vinavyowazuia watu wenye ulemavu kushiriki katika nafasi za uongozi na maamuzi ya kisiasa.

Wito huo umetolewa Desemba 2024 na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulika na masuala ya watu wenye ulemavu kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu inayoadhimishwa Desemba 3 kila mwaka.

Mashirika hayo ni Taasisi ya Vijana Wenye Ulemavu Tanzania (YoWDO), Chama cha Watu Wenye Ualbino (TAS) na DOLASED.

Mkurugenzi wa YoWDO, Rajab Mpilipili, amesema lengo ni kuhakikisha mazingira ya kisiasa yanawakilisha sauti za kila mtu.

“Mashirika ya watu wenye ulemavu tunatoa rai kwa jamii ya Tanzania na Serikali yetu kuweka jitihada za dhati kwa kutoa fursa za uongozi kwa watu wenye ulemavu ili waweze kushiriki na kuongoza kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa,” amesema Mpilipili.

Amezitaja baadhi ya changamoto zinazokwamisha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika uongozi kuwa ni mazingira yasiyo fikivu, ubaguzi na unyanyapaa, mtazamo hasi, watu wenye ulemavu kutojiamini kwa kudhubutu kushiriki katika michakato mbalimbali ya uongozi, mazingira ya kisera, kisheria na kikatiba yasiyotoa nafasi moja kwa moja kwa watu wenye ulemavu kujiwakilisha wenyewe.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la DOLASED, Wakili Gideon Mandesi, ametoa rai kwa waajiri wa umma na binafsi kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni zilizopo ili kutoa fursa za ajira na kazi kwa watu wenye ulemavu.

Kwa mujibu wa Wakili Mandesi, mashirika hayo kwa pamoja yameanzisha jukwaa la kidigitali lijulikanalo kama YoWDO Connect Portal litakalowawezesha waajiri kufahamu watu wenye ulemavu wenye vigezo, sifa na ujuzi wa kuajirika wanapopatikana.

“Idadi kubwa ya watu wenye ulemavu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wana vigezo, sifa na uwezo wa kuishi na kufanya kazi zenye staha hivyo, tunatoa rai kwa mashirika ya umma na binafsi kujisajili katika jukwaa hili kwa ajili ya kuwapata watu wenye ulemavu wenye vigezo na sifa za kuajirika,” amesema Wakili Mandesi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa TAS, Abdallah Bocheka, amesema ni muhimu kulinda na kuimarisha haki za watu wenye ulemavu kwa kuhakikisha kuwa mauaji, manyanyaso na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino yanakomeshwa nchini.

“Tunalaani vitendo vya kinyama visivyo na utu na vinavyokiuka haki za msingi za binadamu na kusababisha mateso makubwa kwa jamii ya watu wenye ualbino. Ukatili dhidi ya watu wenye ualbino bado unatishia usalama na utu wao, kuna haja ya kuendesha kampeni za uelimishaji jamii na kupata suluhisho linalotokana na ushirikiano wa jamii ili kuhakikisha usalama wa watu wote wenye ulemavu,” amesema Bocheka.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema; ‘Kuongeza uongozi wa watu wenye ulemavu kwa mustakabali jumuishi na endelevu’.

Related Posts