WAKULIMA WASHAURIWA KUPIMA UDONGO KABLA YA KULIMA

 Na Farida Mangube, Morogoro .

Katika kuadhimisha siku ya udongo Duniani Idara ya Sayansi za Udongo na Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Taasisi ya wanaagronomia Tanzania (Tanzania Agronomy Society- TAS) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeadhimisha siku hiyo kwa kuwakutanisha wadau wa kilimo kwa lengo la kukumbushana umuhimu wa matumizi sahihi ya udongo kwa maendeleo ya kilimo na usalama wa chakula. 

Akizungumza na waandishi wa habari, Dkt. Boniface Massawe, Mkuu wa Idara ya Sayansi za udongo na Jiolojia kutoka SUA anasema kupima udongo ni hatua muhimu inayowawezesha wakulima kuelewa hali ya virutubisho vya udongo wanaoutumia.

“Udongo ni msingi wa kilimo. Bila kujua hali yake, wakulima wanaweza kujikuta wakitumia mbolea zisizofaa au kupanda mazao yasiyofaa kwa aina ya udongo waliyonayo ndio maana leo tumekuja kuwapa elimu ya umuhimu wa kupima udongo kabla ya kulima” alisema.

Katibu Mkuu Taasisi ya Wanaagronomia Tanzania (TAS) Emmanuely Zephaline amesema mwaka huu wameshirikiana na SUA katika kuadhimisha siku hiyo ili kupeleka elimu kwa jamii hasa wakulima umuhimu wa kupima udongo kabla ya kulima ili kuimarisha ustawi wa chakula kwa kupata mavuno yenye tija.

Dkt. Sibaway Mwango mratibu wa utafiti wa udongo kutoka TARI Mlingano anasema ni vyema wakulima wakapima udongo wa shamba kabla ya kulima ili kuongeza tija na kudumisha rutuba ya udongo.

Amesema matumizi ya mbolea kwa kiasi kikubwa au kidogo yanaweza kuharibu udongo na kusababisha athari za muda mrefu kwenye mazingira. 

“Kuna maeneo mengi nchini udongo umechoka kabisa kwa sababu wakulima hawajui aina ya mbolea ya kutumia au njia bora za kuhifadhi udongo,” amesema

Kwa upande wao wakulima wameiomba serikali na wadau wa kilimo kuhakikisha huduma za upimaji udongo zinapatikana kwa gharama nafuu. 

“Ni muhimu kufanikisha elimu ya upimaji udongo kufikia wakulima vijijini kwa sababu ndio walengwa wakuu wa kampeni hii,” alisema mmoja wa wakulima

Wanasema awali wamekuwa wakilima bila kufuata kanuni bora za kilimo ikiwemo kupima udongo kwa kutojua madhara yake huku lawama zote wakizielekeza kweye ubora wa mbegu wanazotumia.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), udongo wenye afya ni muhimu si tu kwa uzalishaji wa mazao bali pia kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kudumisha maisha ya viumbe hai ardhini.

Related Posts