Wadau nishati safi wataka sera kuwabana waingiza vifaa visivyo na ubora

Dar es Salaam. Wadau wa Nishati Safi ya kupikia nchini Tanzania, wameitaka Serikali kutunga sera ili kuwabana wanaoingiza vifaa visivyo na ubora kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kupikia.

Uwepo wa sera hiyo utadhibiti uingizwaji wa vifaa vikiwemo majiko ya gesi, umeme, mipira ya kusukumia gesi, stovu pamoja na mitungi.

Wameyasema hayo jana Jumatano Desemba 4, 2024 wakati wa mkutano wa kujadili sera katika sekta nishati ulioandaliwa na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) na kuwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi na Serikali.

Dhumuni la mkutano huo ni kuangalia namna gani jamii inaweza kushirikishwa kikamilifu katika mpango huu wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034 wawe wanatumia nishati safi.

Meneja wa UNCDF, Imanuel Muro amesema kutokana na umuhimu wake kuna kila sababu ya Serikali kutunga sera hiyo ya uingizaji wa vifaa kwaajili ya wananchi.

Amesema Serikali ina taasisi zake kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo kazi yake ni kudhibiti ubora wa bidhaa mbalimbali zinazoingizwa nchini, hivyo lisimamie kwa umakini uingizwaji huo.

“Ni vyema udhibiti huu ukawepo ili kudhibiti wafanyabiashara wasiokuwa wazalendo ambao wanaweza kuweka vifaa feki sokoni na kuathiri watumiaji,” amesema.

Aidha Muro ameenda mbali zaidi akisema hata ikiwezekana, ili kuongeza uelewa wa nishati safi, Serikali iingize katika mitaala suala hilo ili wanafunzi wafahamu tangu wakiwa shuleni umuhimu wa mpango huo.

Akichangia katika mazungumzo hayo, Andres Mendes, mdau wa nishati safi kutoka Kenya amesema kuna haja ya kupeana taarifa mbalimbali kuhusiana na kila hatua ya mpango huo wa nishati safi wa kidunia ili wananchi waweze kuwa na uelewa wa mpango huo.

Amesema ikiwa hakutakuwa na taarifa na maelezo ya kutosha kuhusu umuhimu wa nishati safi, utekelezaji wake utakuwa hafifu.

Katarina Aloyce anayefanya kazi ya utafiti mbalimbali, amesema kuna haja ya kupunguza gharama kwa kila kitu kinachohusiana na matumizi ya nishati safi ili kila Mtanzania aweze kumudu gharama.

Akitoa mfano, amesema kuwa kwa kuwa Serikali imepeleka umeme vijijini, na inahamasisha matumizi ya nishati safi, sasa hatua hiyo itakuwa na tija kwa kupunguza gharama kwa vifaa wezeshi vya matumizi ya nishati safi ikiwemo nishati ya umeme.

Mpango huo wa UNCDF unafanya kazi ya kuhabarisha na kuibua mijadala namna ya kutekeleza mpango wa nishati safi umefadhiliwa na Umoja wa Ulaya, Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), UNCDF, Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (Unido) na CoockFund.

Hata hivyo Serikali imekuwa ikisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia Rais Samia Suluhu Hassan ili kutoathiri afya na mazingira kutokana na matumizi ya nishati zisizo safi kama kuni na mkaa.

Related Posts