Kibaha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu wawili, mmoja akiwa ni mume anayetuhumiwa kwa kumuua mkewe na mwingine akidaiwa kuwajeruhi watu wanne kwa kutumia bunduki.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, ameeleza hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari, Desemba 5, 2024, mjini Kibaha.
Watuhumiwa hao ni Godfrey Killu, mkazi wa Kibaha, ambaye anatuhumiwa kwa kumuua mkewe aitwaye Elizabeth Sindakika.
Tukio hili linadaiwa kutokea Desemba 1, usiku, baada ya mume na mke huyo kwenda katika baa kwa ajili ya kunywa pombe.
Kamanda Morcase ameeleza kuwa wakiwa huko, Godfrey alimtaka mkewe warejee nyumbani, lakini Elizabeth alikataa hali hiyo ilisababisha ugomvi kati yao ambapo Godfrey alianza kumshambulia marehemu kwa fimbo.
“Baada ya kumshambulia, Godfrey aliona mkewe akizirai na kumkimbiza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani, Tumbi, kwa matibabu, hata hivyo, alithibitika kufariki dunia baada ya kupatiwa huduma za kwanza,” amesema Kamanda Morcase.
Muuguzi wa zamu aligundua kuwa marehemu alikuwa ameshambuliwa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na alichukua hatua ya kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ambao walifika hospitalini na kumkamata Godfrey, ambaye sasa anahojiwa huku mwili wa marehemu unaendelea kufanyiwa uchunguzi na utakabidhiwa kwa familia kwa taratibu za mazishi.
“Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa,” ameongeza Kamanda Morcase.
Katika tukio lingine, Kamanda Morcase amezungumzia tukio la kujeruhi watu wanne kwa kutumia bunduki, ambalo lilitokea Desemba 2, 2024, katika Wilaya ya Bagamoyo.
Mwekezaji mzawa, Keneth Amon anadaiwa kuwajeruhi wafugaji wanne kwa kutumia bunduki baada ya mifugo yao kuingia katika shamba lake.
“Vurugu zilitokea kati ya wafugaji na walinzi wa shamba, na baada ya Keneth kutoka nje, alijitokeza kwa bunduki na kuwajeruhi wafugaji wanne na waliwahishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu,” amesema Kamanda Morcase.
Keneth Amon anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi, na atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.