Abiria SGR wasota Soga saa nne, TRC yatoa sababu

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania (TRC), limesema kilichokwamisha safari ya treni ya umeme iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma ni hitilafu ya umeme.

Abiria waliokuwa wakisafiri na treni hiyo walijikuta wakisota Stesheni ya Soga mkoani Pwani, kwa saa nne kisha wakaendelea na safari.

Treni hiyo ilitakiwa kuondoka Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam, jana Jumatano Desemba 4, 2024 saa 12:55 jioni lakini iliondoka 1:10 usiku na ilipofika stesheni ya Soga kuanzia saa 2:45 usiku ilisimama.

Treni hiyo ilikaa hapo pasipo abiria kuelezwa nini tatizo lililowafanya kusimama hapo. Ilipofika saa 6:48 usiku wa leo Alhamisi, Desemba 5, 2024 walianza safari na kufika Dodoma saa 11 alfajiri.

Miongoni mwa abiria waliokuwamo kwenye treni hiyo, walikuwa wakilalama kutokana na kutopewa taarifa sahihi ya nini kinaendelea.

“Tumesimama hapa kwa muda sasa, hakuna taarifa yoyote mpaka sasa juu ya nini kinaendelea. Tumekunywa chai hadi zimeisha na wengine tuna watoto hatujui nini kinaendelea hapa,” alisikika mmoja wa abiria abiria hao.

Kwa mujibu wa ratiba ya treni hiyo, ilikuwa itoke Dar es Salaam jana Jumatano, saa 12:55 jioni na kufika Dodoma saa 5:01 usiku, lakini kutokana na changamoto hiyo wamejikuta abiria wakifika alfajiri ya leo Alhamisi.

Mapema asubuhi ya jana Jumatano, abiria waliokuwa wakitoka Dodoma kwenda Dar es Salaam nao walikwama kwa dakika kadhaa kwa kile kilichoelezwa ni hitilafu ya umeme kwenye gridi ya Taifa, hivyo kuathiri upatikanaji wa umeme kwenye mikoa inayohudumiwa na gridi hiyo.

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika taarifa yake lilieleza kumetokea hitilafu kwenye gridi ya Taifa na tayari tatizo hilo limepatiwa ufumbuzi na huduma kurejea.

Leo Alhamisi, Mwananchi limezungumza na Ofisa Habari wa TRC, Fredy Mwanjala kujua changamoto gani ilijitokeza kwa treni hiyo, ambapo amesema ilitokea hitilafu ya umeme.

Mwanjala amesema kukwama kwa treni hiyo ni muendelezo wa changamoto za hitilafu ya umeme zilizotokea kwenye gridi.

“Umeme sawa ulirudi, lakini ipo hivi unaweza kurudi, ukarudi kwa nguvu sana, hata majumbani huwa inatokea ikitegemea na vifaa vyako umevilinda kwa kiasi gani.

“Ndicho kilitokea kwenye treni yetu ya umeme, hadi saa 6:48 usiku huduma ikarejea, ” amesema.

Amesema, hitilafu hizi ni za dharura, ambazo zinaweza kutokea kwenye usafiri wowote.

“Sema mentality (mtazamo) kwa baadhi ya watu wasiopenda maendeleo wanaotaka kuiona SGR inafeli na kufeli ilishatengenezwa kwamba ikitokea changamoto kama hizi wao ndio wanafurahia.

“Hata sisi (TRC) hatupendi changamoto hizo, na zinapotokea hakuna anayelala, mfano jana, tulikuwa na Mkurugenzi (Masanja Kadogosa) hadi saa 8 usiku tunapambana mambo yaende, hivyo Watanzania waelewe hizi ni dharura kama ambavyo vitatokea kwenye usafiri mwingine,” amesema Mwanjala.

Amesema dharura inapotokea, haitoi taarifa, hivyo hata kwao inapotokea zinakuwa nje ya uwezo wa mafundi, hivyo kuanza kupambana ili kurudisha huduma katika hali ya kawaida.

Mmoja wa abiria aliyezungumza na Mwananchi, ameshauri uongozi wa TRC kuhakikisha unaboresha mawasiliano kwa kutoa taarifa kwa abiria pindi kunapotokea dharura badala ya kukaa kimya kama wafanyavyo sasa.

Amesema kitendo cha wafanyakazi kukaa kimya bila kueleza abiria kitu kinachoendelea kunatengeneza mazingira ya hofu na taharuki.

Pia, huduma ndani ya treni ikiwemo vyakula ni tatizo linapotokea dharura kwa kuwa abiria wengine husafiri na watoto na wagonjwa ambao wanahitaji huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo vyakula.

“Treni inakwama kwa zaidi ya saa tano, unapouliza mhudumu anakujibu hajui tatizo nini, wanaotoa matangazo wako kimya. Ukiagiza maji unaambiwa yameisha, kahawa hakuna sasa wanataka watu wafe kwa njaa ama nini?”

Tupo kwenye zama za Tehama lakini, huduma ndani ya SGR bado za kizamani sana,” amesema abiria huyo ambaye jana alisafiri kutoka Stesheni ya Magufuli Desemba 4, 2024 saa 1:10 usiku na kufika Stesheni ya Samia Suluhu Hassan Dodoma saa 11 alfajiri ya Desemba 5, 2024.

Abiria mwingine naye amesema: “Ila kubwa hakuna mawasiliano kabisa, yaani tumetoka Dar es Salaam tumechelewa na hawakusema lolote, tumeondoka tumefika Soga tumesimama wakatangaza hiyo shida lakini tulivyokaa pale zaidi ya saa nne, tulianza safari na kufika Ruvu tukasimama kama dakika kadhaa kisha tukaanza kurudi nyuma.

Kila mtu alishangaa, yaani kurudi tulipotoka halafu hakuna tangazo, hakuna sababu iliyosemwa tukafika karibu na Soga baada ya dakika chache tukaendelea na safari kufika Ruvu tukaambiwa tunapishana na treni nyingine ila kitendo hicho cha kurudi nyuma wala hakikuelezwa sababu.”

Related Posts