Profesa Janabi: Chembe za plastiki zinaweza kuathiri ubora wa mbegu za kiume

Dar es Salaam. Chembechembe za plastiki na kemikali inayotumika kutengeneza bidhaa hiyo, zinatajwa kuathiri afya ya uzazi, ikiwemo ubora na idadi ya mbegu za kiume.

Kemikali inayotajwa ni BPA (Bisphenol A) inayotumika kutengeneza plastiki ambazo mara nyingi hutumika kama vyombo vya chakula, vinywaji, vifaa vya matumizi ya kila siku, vifaa vya matibabu na umeme.

Pia hutumika kwa utengenezaji wa vifaa kama vile chupa za maji, vyombo vya kuhifadhia chakula, vikombe vya watoto, na kwenye makopo ya chakula na vinywaji ambayo hupakwa ndani ili kuzuia kutu na kuharibu chakula.

BPA inatajwa  kusababisha madhara yakiwamo ya athari kwa mfumo wa homoni na kuongeza hatari ya matatizo ya uzazi, ya moyo na mishipa na kuathiri maendeleo ya ubongo, hasa kwa watoto wachanga.

Pia tafiti zinaonyesha inaweza kuongeza hatari ya saratani kama vile za matiti na tezi dume.

Hivyo inashauriwa kutumia vyombo vya plastiki visivyo na BPA na kuepuka kuweka chakula cha moto kwenye vyombo vya plastiki, huku ikishauriwa kuvibadilisha vyombo hivyo na vya kioo au chuma cha pua inapowezekana.

Mshauri wa masuala ya afya ambaye pia ni Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi, kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ya Instagram na X,  ameandika akitaja sababu ya kupungua kwa ubora na idadi ya mbegu za kiume ni pamoja na matumizi ya plastiki zenye BPA.

Profesa Janabi amezungumzia mazingira ya kisasa na namna yalivyojaa hatari zilizofichwa zinazoathiri afya ya uzazi.

Amesema bidhaa nyingi hutoa chembechembe za plastiki ndogo, zenye kemikali zinazoweza kuathiri uzazi, kuongeza hatari ya saratani na kuvuruga usawa wa homoni.

“Uvutio wa kemikali kama BPA kwenye plastiki unaweza kupunguza idadi ya mbegu za kiume na uwezo wake wa kusafiri… amesema.

Ametaja msongo wa mawazo wa muda mrefu, ukosefu wa mazoezi na usingizi duni pia vinavuruga viwango vya ‘testosterone’ (homoni ya kiume) na usawa wa homoni unaohitajika kwa uzazi.

Profesa Janabi ambaye ni mbobezi wa magonjwa ya moyo ameainisha mambo ambayo mwanamume anatakiwa kuyafanya kuboresha afya ya mbegu za kiume kwa ujumla.

“Achana na plastiki, chagua bidhaa zisizo sumu, plastiki hasa zile zilizo na BPA na ‘phthalates’ hutoa kemikali hatari zinazovuruga mfumo wa homoni mwilini mwako. Kemikali hizi huiga homoni na kuvuruga mfumo wako wa uzazi na afya yako kwa ujumla.

“Tumia vyombo vya kioo au chuma cha pua, angalia lebo za ‘BPA-free’  (zisizo na kemikali hiyo) kwenye vitu vya kila siku kama risiti, makopo na chupa za maji,” amesema.

Ameshauri kuchagua bidhaa za utunzaji wa mwili na usafi, zenye lebo zisizo na harufu au zisizo na sumu ili kupunguza athari za kemikali mwilini.

Kwa upande wa vyakula amesema ni muhimu kufuata ulaji wa vile vya asili vyenye virutubisho vingi kupambana na uvimbe.

“Kile unachokula kinaathiri moja kwa moja afya yako ya uzazi. Mlo wenye sukari nyingi, mafuta yaliyochakatwa na vyakula vilivyosindikwa huongeza msongo wa oksidishaji na uvimbe, kuharibu mbegu na kusababisha kutofanya kazi vizuri kwa homoni,” amesema.

Profesa Janabi amesema ni muhimu kulenga ulaji wa mboga za rangi tofauti, mboga za majani na matunda yenye vioksidishaji kama ‘berries’ ili kupunguza uharibifu wa chembe huru.

“Jumuisha mafuta yenye afya kama parachichi, karanga, mbegu na vyakula vya omega 3 kama samaki (salmoni) ili kuongeza uzalishaji wa homoni. Ondoa au punguza vyakula vilivyosindikwa, sukari na wanga uliosafishwa ili kuweka sukari ya damu katika hali thabiti na kupunguza uvimbe,” amesema.

Pia anashauri ni muhimu kuweka kipaumbele katika usingizi, kutembea na usimamizi wa msongo wa mawazo ili kusaidia afya ya homoni.

Profesa Janabi amesema msongo wa mawazo wa muda mrefu, usingizi mbaya na maisha yasiyo ya kimwili vinaathiri viwango vya homoni za uzazi na kufanya kuwa vigumu kudumisha uzazi bora.

Akizungumza na Mwananchi Agosti mwaka huu, Mkuu wa kitengo cha upandikizaji mimba (IVF) Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Matilda Ngarina alitaja mambo ya kufuata na kuepukwa ili mwanamume awe na mbegu zilizo bora.

Alisema lazima ajue vitu vingapi vinaweza kuharibu ubora, akitaja wapo ambao huzaliwa wakiwa tayari na changamoto ya mbegu, ikiwemo shida za homoni, mfumo na wengine kupata athari baadaye na kuharibu ubora wa mbegu zinazozalishwa.

“Inategemea unakula nini, unakunywa nini, unafanya kazi gani na tabia ya ngono zembe pia nayo inaathiri ubora wa mbegu.

“Ukifanya ngono zembe ukawa na maambukizi inaathiri ubora wa mbegu, ukinywa pombe nyingi, sigara, kukaa muda mrefu sehemu yenye joto inaathiri ubora wa mbegu,” alisema.

Alitaja kutokula vyakula vyenye ubora, ikiwemo mboga za majani, matunda na protini kwa wingi kuwa huathiri ubora wa mbegu.

Kwa mujibu wa Dk Ngarina, katika mshindo mmoja mwanamume anatakiwa kutoa mbegu zaidi ya milioni 30.

Kuhusu ubora wa mbegu, anasema huhusisha jinsi inavyotembea kwenda kutafuta yai, ambayo kawaida huogelea kwa kasi kwenda mbele, iwe na kichwa, shingo na mkia.

Mbegu isiyo bora anasema hubaki ikichezacheza palepale badala ya kusonga mbele.

Dk Ngarina anasema ili kubaini ubora wa mbegu, hutakiwa zaidi ya asilimia 60 ziwe na safari zinazoeleweka.

Related Posts