Arusha. Mahakama ya Rufani, imetengua adhabu ya kifo aliyokuwa amehukumiwa Cheni Vareli, baada ya kukutwa na hatia ya kumuua mama yake mzazi, Leah Masangaa, kutokana na dosari za kisheria. Uamuzi huyo umefikiwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo walioketi Dodoma, waliosikiliza rufaa hiyo ya jinai namba 269 ya mwaka 2021, baada ya kukubaliana na sababu moja ya rufaa kuwa Jaji aliyesikiliza shauri hilo awali, hakusaini ushahidi wa kila shahidi aliyetoa ushahidi kwenye kesi hiyo.
Aidha kutokana na dosari nyingine zilizopo kwenye kesi hiyo, Mahakama hiyo imesema kesi hiyo haiwezi kusikilizwa upya kwani itatoa mwanya kwa upande wa mashtaka kuziba dosari zilizopo ambazo zilisababisha tofauti kati ya ushahidi na hati ya mashtaka. Cheni alidaiwa kumuua mama yake mzazi Juni 24, 2017, katika Kijiji cha Mapinduzi, wilayani Bahi, Dodoma baada ya kumuomba mama yake fedha Sh5,000 na mama yake kumjibu hana,jambo lililopolekea kumtolea maneno machafu, kumpiga hadi kumuua mama yake.
Hukumu hiyo iliyomuachia huru Cheni imetolewa Disemba 4, 2024 na jopo la majaji hao ambao ni Shaban Lila, Zainab Muruke na Gerson Mdemu.
Awali Cheni alihukumiwa adhabu hiyo Machi 18, 2022 na Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Ilivyokuwa Katika kuthibitisha kesi yake, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi watano pamoja na vielelezo viwili huku kwenye utetezi, Cheni akiwa shahidi pekee.
Ilidaiwa siku ya tukio, Cheni aliyekuwa akiishi na mama yake (marehemu), saa 11 jioni, alimuomba mama yake sh 5,000 ambapo mama yake alimjibu hana pesa.
Ilidaiwa kuwa Cheni alikasirika na kumtolea maneno machafu mama yake ambapo kwa mujibu wa shahidi wa kwanza, Mahajile Vareli (kaka yake mkubwa), alidai kuwa ilikuwa kawaida ya Cheni kugombana na mama yao.
Alidai kuwa baada ya ugomvi huo aliondoka na alipokuwa umbali wa karibu mita 100, alisikia kelele kutoka nyumba ya mama yake na kuamua kurudi ambapo alimkuta Cheni akimshushia kipigo mama yao hadi akafariki.
Alidai baada ya kutenda kosa hilo alikimbia, hivyo yeye akalazimika kupiga kelele kuomba msaada ambapo watu walikusanyika eneo hilo.
Shahidi wa pili ambaye ni Kiongozi wa Kanisa, Blandina Mdemwa, alidai kuwa Cheni alikimbilia kwake na kukiri kumuua mama yake mzazi hivyo kumuomba kuendesha misa ya mwisho kwa kutumia maji ya baraka.
Blandina alidai kuwa aliona suruali na viatu vya mrufani vikiwa na damu na kuwa baada ya hapo alienda na vijana wawili eneo la tukio ambapo walimkuta shahidi wa kwanza na mwili wa marehemu ukiwa kwenye dimbwi la damu.
Blandina alidai kumpigia simu kiongozi wa mtaa huo, ambaye kwenye kesi hiyo alikuwa shahidi wa tatu, Forogo Matonya kumweleza kuhusu tukio hilo kisha Cheni akakamatwa na taarifa zikatolewa Kituo cha Polisi Kigwe.
Ilidaiwa Juni 25, 2017 polisi kutoka Bahi walifika na shahidi wa nne, Dk Kassimu Kolowa, ambaye aliufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, ambaye alithibitisha kuwa marehemu alikufa kutokana na majeraha makubwa kichwani.
Baada ya kusikilizwa kesi hiyo, Jaji na wazee wa baraza walihitimisha kuwa Cheni ana hatia baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka yoyote hivyo kumtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Rufaa Katika rufaa hiyo Cheni aliwakilishwa na Wakili Leonard Haule huku upande wa jamhuri ukiwakilishwa na mawakili ambapo mrufani huyo aliwasilisha sababu nne za rufaa.
Katika uamuzi wa majaji hao walieleza kuwa sababu zitakazoonekana wazi katika hukumu hiyo ni sababu ya tatu na nne ambazo ni Jaji aliyesikiliza kesi hiyo alikosea kisheria kumtia hatiani mrufani kwa kutojali kabisa tofauti ya wazi kati ya shtaka na ushahidi na Jaji kukosea kisheria na kumtia hatiani mrufani kwa kosa kubwa lisilofuata utaratibu.
Wakili Leonard katika kuunga mkono hoja ya nne alidai Jaji hakuambatanisha sahihi yake mwishoni mwa ushahidi wa kila shahidi wa upande wa mashtaka pamoja na ushahidi wa utetezi wa mshtakiwa alioandika.
Wakili huyo alidai kwa kutoweka sahihi kwenye ushahidi wote wa mashahidi,usahihi na ukweli juu ya ushahidi wote wa mashahidi unatiliwa mashaka na kudhoofisha mwenendo wa kesi.
Wakili huyo katika kuunga mkono kesi yake alinukuu kesi iliyowahi kutolewa uamuzi na Mahakama ya Rufaa na kuiomba Mahakama kubatilisha mwenendo wa kesi, kufuta hatia, kutengua adhabu na kumwachia huru mrufani, kwa sababu kusikilizwa tena hakuwezi kuamriwa.
Wakili huyo alidai kesi hiyo haiwezi kusikilizwa kwani shtaka linatofautia na ushahidi wa upande wa mashtaka kuhusu mahali ambapo kosa hilo lilitendeka kwani ukurasa wa 30 unaonyesha kosa hilo lilifanyika Kijiji cha Mapinduzi.
Alidai shahidi wa kwanza hadi wa tatu walithibitisha kuwa wanaishi Kijiji cha Kigwe, Wilaya ya Bahi, ambako kosa hilo lilitendeka na kusisitiza kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha shitaka hilo, hivyo watakapopewa nafasi ya kusikilizwa tena, watajaza mapengo hayo.
Sababu ya pili ni kuwa Mahakama Kuu ilitoa hukumu kutokana na ushahidi wa shahidi wa kwanza ambaye ushahidi wake haukuwa wa kuaminika kwani kwa nyakati mbili alieleza marehemu alikatwa na vitu viwili tofauti ikiwemo panga.
Alidai katika ukurasa wa 42 ambapo shahidi wa kwanza alidai alikuwepo katika eneo la tukio, shahidi wa tatu alidai kuwa shahidi huyo wa kwanza hakuwepo eneo la tukio na badala yake alimsikia marehemu akipiga kelele.
Wakili Patricia Mkina, alikiri kosa la Jaji ya kutosaini baada ya kila ushahidi wa shahidi aliouandika na kupendekeza shauri hilo lifutwe na kuamuriwa kusikilizwa tena kwa sababu upande wa mashtaka hautajaza mapengo kama inavyodaiwa na wakili wa mrufani.
Uamuzi Baada ya kusikiliza hoja za pande zote majaji hao walieleza kuwa wanafikiri sababu hiyo ya nne inaweza kutupilia mbali rufaa hiyo na kuwa lalamiko kuu lililotolewa na wakili wa mrufani na kukubaliwa na wakili wa serikali ni ni kwamba, Jaji wa mahakama hiyo hakusaini ushahidi wa kila shahidi aliorekodi.
Jaji Muruke amesema wanakubaliana na wakili Leonard kwamba kuanzia ukurasa wa 40 hadi 59 wa kumbukumbu ya rufaa, Jaji aliyesikiliza kesi hakusaini baada ya kurekodi ushahidi wa mashahidi watano wa jamhuri na ushahidi wa utetezi wa Cheni.
“ Uhalisi wa ushahidi wa mashahidi hao pamoja na ukweli wa mwenendo wa kesi katika mahakama hiyo unatia shaka, tunaona kuwa kutokutajwa kunadhoofisha mwenendo mzima wa mahakama na hivyo ni ubatili na si tu uhalali wa ushahidi wa mashahidi bali ukweli wa rekodi yeyenye ya mahakama inatia shaka,”amesema.
Jaji Muruke amesema suala la kutoweka saini baada ya kurekodi ushahidi wa mashahidi lilizingatiwa na Mahakama katika kesi ya Yohana Mussa Makubi na mwingine dhidi ya jamhuri katika rufaa ya Jinai namba 556/ 2015.
“Kwa kukosekana kwa saini ya mtu aliyeandika ushahidi huo, haiwezi kusemwa kwa uhakika kwamba kilichomo kwenye rekodi ni maelezo ya kweli ya ushahidi wa shahidi, mwenendo mzima wa kesi uliorekodiwa baada ya usikilizwaji wa awali unavunjwa kwa sababu sio halisi”ameongeza
Jaji huyo alifafanua kuwa hiyo haitoi uhakika kwamba kesi hiyo ni ya kweli na ni dhahidi kuwa dosari hiyo haiwezi kutibiwa na kifungu cha 388 cha Sheria ya Mwenendo ya Makosa ya Jinai hivyo wanaona dosari hiyo imeharibu mwenendo mzima.
Kuhusu kusikilizwa upya kwa kesi hiyo, baada ya kuchunguza suala hilo kwa kina wanakubaliana na wakili wa mrufani kuwa kuna makosa katika kesi ya mashtaka ambayo ni msingi wa kesi hiyo ilikuwa na tofauti kubwa na ushahidi uliotolewa.
Amesema shahidi wa kwanza hadi wa tatu wa mashtaka walieleza eneo lililotokea tukio ni Kijiji cha Kigwe huku shtaka likieleza tukio limetokea Kijiji cha Mapinduzi.
Jaji Muruke amesema hawaoni ni sawa kwa manufaa ya haki kuamuru kusikilizwa upya kwa sababu ya makosa ya ushahidi wa upande wa mashtaka uliopo kwenye kumbukumbu ya rufaa na kuwa amri ya kusikilizwa upya itafungua njia kwa upande wa mashtaka kuziba mapengo yaliyopo.
Jaji Muruke amesema kwa matokeo na sababu hizo wanaruhusu rufaa kwa msingi wa nne wa sababu ya kukata rufaa, kufuta hukumu na kuamuru Cheni kuachiliwa huru.