Tanga. Chama cha Jiolojia Tanzania (TGS) kimeitaka Serikali kuharakisha uanzishwaji wa bodi ya usajili wa wataalamu wa jiolojia wa Tanzania, kikisisitiza umuhimu wake katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ya sekta ya madini yaliyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya 2030 ya Tanzania.
Wito huu umetolewa na Rais wa TGS, Dk Elisante Mshiu, kwenye mkutano wao wa mwaka unaofanyika jijini Tanga kwa siku tatu ambapo amesema kutokuwepo kwa bodi hiyo kunadhoofisha uwezo wa Tanzania kufaidika kikamilifu na utaalamu wa jiolojia uliopo nchini.
“Uanzishwaji wa bodi hii utakuwa hatua kubwa, ikitoa fursa ya kuwasajili wataalamu wa jiolojia wa Tanzania kwenye ngazi ya kimataifa,” amesema Dk Mshiu wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Dk Mshiu amebainisha kuwa licha ya Tanzania kuwa na takribani wataalamu wa jiolojia 4,000, ni wanne tu wanaotambuliwa kimataifa.
Pengo hili kubwa linasababisha nchi kutegemea kwa kiasi kikubwa utaalamu wa kigeni unaogharimu fedha nyingi.
Amesema kuwa nchi zote zinazofanya vizuri katika sekta ya madini zina bodi za usajili za wataalamu wa jiolojia zinazofanya kazi ipasavyo ili kudhibiti na kukuza sekta hiyo.
Waziri wa Madini, Antony Mavunde, aliyewakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Msafiri Mdibo, aliwahakikishia washiriki wa mkutano kuwa serikali imejipanga kuharakisha uanzishwaji wa bodi hiyo.
“Serikali inatambua nafasi muhimu ya bodi hii katika kusimamia na kutekeleza miongozo ya kimaadili ili kudumisha kasi ya maendeleo ya sekta ya madini kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya 2030,” amesema Mdibo kwa niaba ya Mavunde.
Kupitia mkutano huo amewahakikishia wanachama wa TGS kuwa mchakato huo uko katika hatua za mwisho.
Mdibo amesema ukuaji mkubwa wa sekta ya madini, ambapo mapato ya taifa yameongezeka kwa asilimia 360 kutoka Sh161 bilioni mwaka 2015/16 hadi Sh 753 bilioni mwaka 2023/24.
Aidha, ajira za moja kwa moja kwenye sekta hiyo zimefikia 16,000, huku Watanzania wakichukua nafasi nyingi za juu zilizokuwa zikishikiliwa na wataalamu wa kigeni.
“Mkazo katika usimamizi wa kimaadili ni muhimu ili kuhakikisha madini yanachangia maendeleo endelevu ya kiuchumi,” ameongeza Mavunde, akiwakumbusha washiriki kuwa madini ni rasilimali isiyoweza kujirudia na lazima yachimbwe kwa uwajibikaji ili
Amesisitiza pia umuhimu wa kuoanisha uchimbaji wa madini na suluhisho la nishati safi, jambo ambalo ni kipaumbele kwa wizara wakati mahitaji ya kimataifa ya mabadiliko ya nishati yanapozidi kuongezeka.