Na Mwandishi Wetu
Tanzania imeweka rekodi ya Mkutano wa Pili wa Wahasibu Wakuu wa Serikali Barani Afrika kwa kuwa na washiriki zaidi ya 2000 kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika ikiwa ni idadi kubwa kuwahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wahasibu Wakuu wa Serikali Afrika -AAAG.
Mkutano huo ulioanza Desemba 2, 2024, ukibeba kauli mbiu ya “Kujenga Imani ya Umma katika Mifumo ya Usimamizi wa Fedha za Umma kwa Ukuaji Endelevu” uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AIC), umepokelewa kipekee huku ukikusanya Wahasibu, Wakaguzi wa Ndani na Wataalam wa kada zenye uhusiano wa karibu na uhasibu kama; Wakaguzi wa Hesabu, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA.
Aidha kupitia mkutano huo, washiriki walipata fursa ya kupata ufahamu kutoka kwa wataalam wa sekta ya umma kuhusu mwelekeo wa kisasa, changamoto, na ubunifu katika usimamizi wa fedha za umma.
Mada mbalimbali zilijadiliwa, kuanzia mabadiliko ya kidijitali katika ufanisi wa sekta ya umma hadi kupambana na mtiririko haramu wa fedha, huku ikitolewa fursa bora za kujifunza ambazo zinaweza kutumika moja kwa moja katika majukumu ya kila siku ya wahasibu na wataalamu wa fedha.
Akizungumza wakati wa Kufunga Mkutano huo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, aliwaasa wahasibu kusimamia taaluma yao kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma, na kujiongezea ujuzi ili kuendana na mabadiliko ya
teknolojia.
“Nataka niwaombe wahasibu mtambue kuwa taaluma yenu ni muhimu hata chochote kinachotokea katika sehemu zenu za kazi mtalaumia, hivyo mzuie hasara zinazoweza kutokea” amesema Dkt. Biteko.
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, aliwataka wahasibu wote Barani Afrika, kuwa waaminifu na kuzisaidia nchi zao katika kuhakikisha zinapata maendeleo.
Alisema kuwa kazi zozote zinazofanywa hususani za miradi ya maendeleo katika nchi za Bara la Afrika zinawahusisha wahasibu hivyo, wazingatie maadili ya taaluma zao na miongozo inayotolewa katika nchi zao ili kuhakikisha malengo yanayopangwa yanafanikiwa.