Wasomi hao wanahimiza kuwepo kwa sera kuhusiana na uharibifu na upotevu wa uotoasili kwa msingi wa matokeo ya utafiti, na sio kwa ajili ya kulinda maslahi ya wenye viwanda na shughuli zingine za binadamu ambazo zimesababisha kasi ya mabadiliko ya tabianchi.
Kongamano hilo ambalo limewaleta pamoja wasomi na wadau watendaji katika suala zima la bioanuwai kutoka zaidi ya mataifa 50 ya Afrika na ya Magharibi linalenga kutilia mkazo kwa uhusika wa wasomi na watafiti katika kutatua changamoto mbalimbali zinazotishia uhai wa binadamu, wanyama na uotoasili kwa jumla.
Soma pia:Greenpeace yachukizwa na makubaliano ya COP29
Wasomi hao ikiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu wanabadilishana taarifa na maarifa kutoka nchi zao baada ya kutambua kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo maongezeko ya joto na mvua zinakumba nchi zote.
Kwa mfano kisa cha mafuriko na maporomoko ya udongo kilichotokea Hanang Tanzania kinalinganishwa na kile kilichotokea Uganda wiki iliyopita ambapo zaidi ya watu 28 walipoteza maisha yao.
Wito watolewa juu ya kufidia waathiriwa
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wanaohudhuria kongamano hilo wanahimiza masuala ya fidia yazingatiwe kwa ajili ya waathirika kutokana na hasara na maafa walimotumbukia.
“Jamii waathirika zinarudi nyuma kimaendeleo kwa hiyo wanastahili kufidiwa. Maongezeko haya ya joto na mvua ni kutokana na shughuli za binadamu.”
Lakini suala hilo la fidia zimeibua mjadala mkubwa kwamba nani anastahili kutoa fidia hiyo. Kulingana na wasomi kutoka Afrika Magharibi, nchi za Afrika zinatatizwa na mabadiliko ya tabianchi kutokana na shughuli za mataifa yenye viwanda. Kwa msingi huo mataifa hayo ndiyo yanatakiwa si tu kufidia lakini pia kufadhili juhudi za kuokoa bioanuwai Afrika. Profesa Chris Izinyon kutoka Nigeria ametoa angalizo hilo.
”Mataifa ya Magharibi ndiyo yanasababisha uharibifu mkubwa wa bioanuwai kwa hiyo si hiari ila uwajibifu kwao kufadhili miradi ya kulinda bioanuwai.”
Naye mwanafunzi wa shahada ya uzamivu chou kikuu cha Dar es Salaam Upendo Lyimo ameongezea hivi kuhusu suala hilo.
”Ufadhili bila sera si sawa, na ndiyo maana tathmini ya uharibifu ilingane na fidia.”
Washiriki wameorodhesha athari za uharibifu wa bioanuwai wkitaja zile za moja kwa moja kwa maisha ya binadamu kama vile kupungua kwa viwango vya uzalishaji wa chakula kutosheleza mahitaji ya idadi ya watu inayongezeka kwa kasi.
Wanapendekeza kwamba ili kuwa na jamii stahimilivu dhidi ya makali ya mabadiliko ya tabianchi, njia asilia za kulinda mazingira zizigatiwe hasa watu barani Afrika.
Soma pia: Rasimu mpya ya ufadhili wa tabianchi yazusha mgawanyiko
Wanafunzi Gift Kyando na Elizabeth Kidumla wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamechangia mawazo haya.
“Njia asilia ndizo njia za uhakika katika kulinda bioanuwai. Tujitokeze na mbinu za kimaumbile kama vile kuwatumia nyuki kuchevusha mimea kwa kiwango cha juu.”
Wenyeji wa kongamano hilo la siku tatu ni Chuo Kikuu cha Makerere ambacho kimeratibu mawasilisho kutoka kwa mataifa yote yaliyowakilishwa na yanatarajiwa kuwa na mengi ya kujifunza na kubadilishana uzoefu na maarifa.