MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa namna mshtakiwa Kambi Zuberi Seif, alivyokamatwa akitoroka kwenda nchini Kenya kupitia mpaka wa Horohoro, uliopo mkoani Tanga.
Kambi aliye mmiliki wa kituo cha Cambiasso Sport Academy kilichopo Tuangoma Kigamboni, anadaiwa kukamatwa Horohoro na maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya( DCEA), baada ya kuweka mtego na zuio katika mipaka ya Tanzania na katika viwanja vyote vya ndege vilivyopo nchini kutokana na kupata taarifa kuwa mtuhumiwa huyo anataka kutoroka nchini.
Kambi na wenzake watano, wanakabiliwa na mashtaka nane yakiwemeo ya kuongoza genge na kusafirisha dawa za kulevya aina ya herone zenye uzito wa kilo 34.89 pamoja na kutakatisha fedha.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 43/2023 ni aliyekuwa kocha wa makipa wa timu ya Simba Sport Club, Muharami Sultani(40) maarufu kama Shilton; Maulid Mzungu(54) maarufu Mbonde, mkazi wa Kisemvule ambaye ni dalali wa viwanja na muuza nazi.
Wengine ni Said Matwiko mkazi Magole; John Andrew maarufu Chipanda(40) mkazi wa Kitunda ambaye kazi yake ilikuwa ni kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka Cambiasso Sport Academy pamoja na Sarah Joseph, ambaye ni mke wa Matwiko.
Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi.
Hayo yameelezwa leo na jopo la mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga akisaidiana na Judith Kyamba na Roida Mwakamele, wakati akiwasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo yaani Commital Proceedings kwa kupokezana.
Mwanga amesema maelezo hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, baada ya upelelezi wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 71 ya mwaka 2022 kukamilika.
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo(Committal Proceeding).
Kabla ya kuwasomea maelezo hayo, wakili Mwanga aliwakumbusha mashtaka yao washtakiwa hao kwa kuwasomea upya hati ya mashtaka.
Baada ya hapo, alianza kuwasomea maelezo ya shahidi mmoja baada ya mwingine.
Akisoma maelezo ya shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo, Mkaguzi wa Polisi kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini( DCEA) Hassan Msangi amedai, Oktoba 26, 2022 majira ya usiku, wakiwa katika doria walipata taarifa kutoka kwa msiri Kambi anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya na katika harakati za kuhamisha dawa hizo, anazipeleka huko Kivule katika nyumba ya John Adrew na Said Matwiko.
“Tulikuwa na gari mbili, hivyo tulijigawa wengine walienda katika nyumba ya John na mimi nilienda kwenye Matwiko na kwenda kufanya upekuzi katika nyumba hizo na kuwakamata watuhumiwa hao” amedai Msangi.
Amedai katika nyumba ya Matwiko walikuta boksi mbili za mbao, ambapo moja lilikuwa maandishi ya kiruni na ndani yake lilikuwa na pakiti 12, lingine likiwa na mifuko ya vitambaa sita, ambayo ndani yake kuna dawa za kulevya aina ya Heroini.
Vile vile katika nyumba ya Matwiko walikuta mifuko nane ya nailoni ambayo ndani yake ilikuwa na Heroni.
Baada ya upakuzi huo, waliorodhesha vitu hivyo katika hati ya ukamataji na kisha kumkamata Mwatwiko na mke wake Sara Joseph na kisha kuwapeleka Polisi.
Pia kwa mshtakiwa John walikuta heroine na katika maelezo yake alidai kuwa alipewa na Kambi na kwamba anatarajia kutoroka.
Baada ya taarifa hizo, maofisa ya DCEA wakishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi waliweka zuio na mtego katika mipaka na viwanja vya ndege vyote.
Pia maofisa hao walienda kufanya upekuzi katika nyumba ya Kambi Zuberi iliyopo mtaa wa Chisinza eneo la Oysterbay katika nyumba ya Kavishe.
Maofisa hao walipofika nyumbani kwa Kambi hawakumkuta bali walimkuta mdogo wake aitwaye Sabrina Zuber Seif na huku chumba cha Kambi kiliwa kimefungwa.
Maofisa hao wa DCEA walilazimika kuvunja kitasa cha mlango na kufanya upekuzi katika chumba hicho ambapo walikuta fedha taslimu Sh 9milioni na funguo ya gari aina ya Fortune.
Walipewa taarifa kuwa Kambi ameondoka nyumbani hapo baada ya kusikia washirika wake ambao ni Chipanda, Said na Maulid wamekamatwa.
Jinsi Kambi alivyokamatwa
Oktoba 30, 2022, usiku maofisa kutoka DCEA na vyombo vingine vya ulinzi walienda mpaka wa Horohoro uliopo Tanga, ambapo walipewa taarifa za Zuberi kutoroka kwenda nchini Kenya kupitia mpaka huo.
“Waliweka kambi eneo hilo na usiku wa Oktoba 31, 2022 Kambi alikamatwa na akiwa na dola za kimarekani 500 pamoja na fedha taslimu Sh 41,000, simu 4 za mkononi pamoja na hati ya kusafiria na kisha kumrejesha Dar es Salaam” amedai Msangi.
Novemba Mosi, 2022 Kambi alifikishwa Dar na kupelekwa DCEA na alipumzika kwa masaa 3 na kisha alianza kuhojiwa kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.
Katika mahojiano yake, Kambi amekiri kifanya biashara hiyo na pia alikiri kiwatambua washirika wake na kwamba alianza biashara ya kuuaza dawa mwaka 2009, ambapo alikuwa anauza rejareja na kwamba alikuwa ananunua kwa Hafidh na Kelvin Soka.
Amedai kuwa dawa hizo zilikuwa zikitoka Afghanistan kupitia Bahari ya Hindi na kupokelewa na Ali Yusuph.
Amedai baada ya kupokea alikuwa akimpa mtu aliyemtaja kwa jina la Kulangwa na Muharami na Muharami alikuwa akimpa John, huku akiongeza kwamba alipokea pakiti 80 kutoka Afganistan, ambapo alimpa mshtakiwa John.
“Pia Zuberi alitufahamisha kuwa laini zake za simu alisajiliwa na watu wengine kwa madai kuwa yeye hana kitambulisho cha taifa( Nida) kwa kuwepa kujilikana katika biashara hiyo, lakini tulivyomfanyia upekuzi tulimkuta na kitambulisho chake cha taifa,” ilidai wakili wa Serikali wakati akisoma maelezo ya shahidi.
Hata hivyo, katika uchunguzi wa nyaraka mbalimbaki ziizokutwa kwa Kambi, ilibainika kuwa ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Safia Group Campanies Limited na anamiliki magari matano aina ya TATA ambayo yalitokana na biashara haramu ya dawa za kulevya.
Muharami alikamatwa Bweni majira ya asubuhi baada ya kumaliza kufanya mazoezi.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa Muharami alikamatwa baada ya maofisa wa Mamlaka hiyo kwenda katika eneo ambalo alikuwa anafanya mazoezi na kumkuta Seleman Matola, ambapo aliwaeleza kuwa wameshamaliza kufanya mazoezi, hivyo aliwambia waende sehemu ya kuegeshea magari labda wanaweza kumuona.
Matola aliongozana na maofisa hao hadi kwenye maegesho ya magari na kumkuta Muharami akiwa katika gari yake aina ya Hyundai Santa na kujitambulisha kisha kuanza upekuzi katika gari na chumba cha mazoezi.
Baada ya hapo walienda kwake Kigamboni na kufanya upekuzi na katika maelezo yake, akiri kuwafanya washirika wenzake na pia alikiri kufanya biashara ya dawa za kulevya.
Muharami alidai kuwa amekuwa akichukua dawa za kulevya na kumpekekea kaka yake, aitwaye Maulid aliyopo Mkuranga.
“Oktoba 27, 2022 Mkaguzi wa Polisi, Brown kutoka DCEA akiongozana na askari wengine waliongozana hadi katika nyumba ya Maulid iliyopo Mkuranga ambapo walipofika, Muharami alimtaka kaka yake atoe ndoo nyeupe yenye mfumo wa bluu ambayo alimpa eneo la Mbagala Sabsaba” alidai wakili wakati akisoma maelezo.
Alidia Maulid alienda ndani ya nyumba yake na kuchukua funguo na kisha kwenda katika nyumba nyingine ambayo hakuna mtu anayeishi na kufungua mlango na kisha kuingia ndani na kisha kuelekea chumbani na kuchukua ndoo hiyo ambayo ilikuwa imewekwa kwenye kona ikiwa imefunikiwa kwa juu na kipande cha bati.
Ndani ya ndoo hiyo kulikuwa na mifuko midogo iliyokuwa imefungwa kwa vitambaa na ndani yake ilikuwa na heroin.
Katika maelezo hayo, Muharami alikiri kupokea Pakiti 73, ambapo pakiti 25 alimpa John na Maulidi na pakiti nane alienda kuficha kwa Maulidi.
Miongoni mwa mashtaka hayo ni kuongoza genge la uhalifu shtaka linalowakabiliwa watu wote ambapo Inadaiwa tarehe tofauti kati ya mwaka 2016 na Novemba 4, 2022 maeneo tofauti na ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride.
Shtaka la pili inadaiwa kuwa Oktoba 27, 2022 katika eneo la Kivule wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 27.10.
Vile vile, Novemba 4, 2023 washtakiwa, Zuberi, Zungu na Mtwiko katika eneo la Kamegele wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa Kilo 7.79.
Katika shtaka la nne, tano, sita na saba ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili mshtakiwa Kambi inadaiwa kuwa Aprili 15, 2021 katika wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam alinunua magari manne aina ya TATA yenye jina la Safia Group of Companies LTD huku akijua mali hizo zilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Katika shtaka la nane inadaiwa kuwa Aprili 24,2021 mshtakiwa Kambi alinunua gari aina ya TATA yenye jina Safia Group of Companies LTD akijua mali hiyo ilipatikana kwa kosa la kuongoza genge la uhalifu.