Ramovic, Fadlu katika mtihani wa mabao

Dar es Salaam. Licha ya kuwa Yanga na Simba wana vibarua tofauti na vigumu vya kufanya katika michezo yao ya pili ya kimataifa wakiwa ugenini nchini Algeria, takwimu zinaonyesha wapinzani wao, MC Alger na CS Constantine ni timu zenye tabia ya kuruhusu mabao.

Jambo hilo linabaki kuwa mtihani kwa Kocha wa Yanga, Sead Ramovic na Fadlu Davids wa Simba kuhakikisha wanaziimarisha safu zao za ushambuliaji ili kutumia nafasi kupata matokeo mazuri.

Katika michezo hiyo ya kimataifa, Yanga watakuwa wa kwanza kutupa karata yao kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi A kwa kukabiliana na MC Alger, Uwanja wa 5 Juliet huku wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa mabao 2-0 mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Simba wao watacheza siku inayofuata, Jumapili upande wa Kombe la Shirikisho Afrika Kundi A dhidi ya CS Constantine kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui, ni umbali wa kilomita 456 kutoka mjini Algiers hadi Constantine ambako wawakilishi wengine wa Tanzania watatupa karata yao.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Yanga kukabiliana na MC Alger katika michuano ya kimataifa, mara ya kwanza ilikuwa 2017 ambapo ilipoteza michezo yote miwili dhidi miamba hiyo ya soka la Algeria, walianza kwa kupoteza kwa bao 1-0 kabla ya kufungwa ugenini mabao 4-0 na kutupwa nje ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa jumla ya mabao 4-1.

Yanga imeenda Algeria ikiwa na mastaa wake ambao walikosekana katika michezo kadhaa iliyopita kutokana na majeraha kama vile, Khalid Aucho na Clement Mzize, jambo ambalo linaweza kuwaweka katika mazingira mazuri ya kupigania pointi tatu wakiwa ugenini baada ya kupoteza nyumbani.

Takwimu zinaonyesha wapinzani wa Yanga, MC Alger wameruhusu mabao matatu katika michezo mitano iliyopita na mabao hayo wameruhusu katika mchezo mmoja dhidi ya CR Belouizdad, hivyo Kocha wa Yanga, Sead Ramović anaweza kuanzia hapa.

MC Alger ambao katika michezo mitano iliyopita ikiwemo za nyumbani na ugenini, wameshinda mmoja tu na kutoa suluhu mitatu, inaonyesha kuwa safu butu ya ushambuliaji kutokana na kufunga kwao mabao mawili ndani ya michezo hiyo. MC Alger inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 17 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Algeria nyuma ya CS Constantine yenye pointi 19. 

Kwa kuangalia mechi zao tano za nyumbani tu, wameruhusu mabao manne na kufunga matatu hivyo ni dhahiri kuwa kama Ramovic atachanga vyema karata zake anaweza kufanya vizuri kwenye mchezo huo wa tatu kwake tangu kurithi mikoba ya Miguel Gamondi ambaye aliifanya Yanga kuvuka hatua hii ya makundi msimu uliopita na kuishia robo fainali.

Yanga ambao walipoteza mechi tatu mfululizo dhidi ya Azam (1-0), Tabora United (3-1) na Al Hilal (2-0), wataingia katika mchezo huu wakiwa na morali ya ushindi kufuatia matokeo mazuri waliyoyapata katika mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Namungo kwa mabao 2-0.

Licha ya mapungufu kadhaa ambayo yalionekana kujitokeza, Ramovic anaamini mabadiliko makubwa yataonekana dhidi ya MC Alger licha ya kwamba watakuwa ugenini, yote hiyo ni kutokana na ubora wa wachezaji alionao.

“Tumekuwa na wakati mzuri wa maandalizi ambayo tunafanya hatua kwa hatua, niseme wazi kwamba hatuna cha kuhofia, hii ni nafasi ya kubadili mwanzo wetu mbaya, tunahitaji ushindi na nimezungumza na wachezaji wangu kwa ajili ya kuwajenga mmoja baada ya mwingine naona wapo na hali nzuri kuelekea mchezo,” alisema kocha huyo.

Katika michezo mitano iliyopita, Yanga ikiwa ugenini Ligi ya Mabingwa Afrika, imeshinda miwili dhidi ya Vital’O ya Burundi kwa mabao 4-0 na Ethiopia Nigd Bank kwa bao 1-0, imetoa sare mbili dhidi ya Mamelod Sundowns (0-0 dakika 90) na Medeama (1-1).

Yanga imepoteza mchezo mmoja tu kati ya mitano iliyopita ikiwa ugenini katika Ligi ya Mabingwa ambapo ni dhidi ya Al Ahly ya Misri kwa bao 1-0. Kwa michezo mitano iliyopita katika ligi, Yanga haijapoteza mchezo hata mmoja ikiwa ugenini, ilizifunga KenGold (1-0), Simba (1-0), Coastal Union (1-0) Singida BS (1-0) na Namungo (2-0).

Kwa upande wa wapinzani wa Simba, takwimu zinaonyesha katika michezo mitano iliyopita ya mashindano yote (nyumbani na ugenini), ikiwemo mmoja wa Kombe la Shirikisho,CS Constantine ambao wanaoongoza msimamo wa Ligi Kuu Algeria wameruhusu mabao matatu na kufunga matano, wanawastani wa kuruhusu mabao wa 0.6 na kufunga ni bao moja kwenye kila mchezo.

Katika michezo hiyo mitano iliyopita, CS Constantine wameshinda mitatu, mmoja ni wa Shirikisho dhidi ya CS Sfaxien kwa bao 1-0 huku mingine ikiwa dhidi ya Olympique Akbou (2-1) na USM Alger (1-0) kwenye ligi yao ya ndani. Hivyo inaonyesha sio timu yenye uwezo mkubwa wa kufunga.

Ndani ya michezo yao mitano ya mwisho nyumbani tu, CS Constantine wameruhusu bao katika michezo minne, ni mchezo mmoja tu ambao nyavu zao hazikugushwa, dhidi ya USM Alger.

Wakati CS Constantine  ikionekana kuwa ni timu inayofungika kulingana na takwimu za michezo yao mitano iliyopita, Simba inaonekana kuwa na safu kali ya ushambuliaji ambayo imefunga mabao 10 katika michezo yake mitano iliyopita, wana wastani wa kufunga mabao mawili.

Tofauti na CS Constantine ambao wamepoteza na kutoa sare mara moja moja, Simba yenyewe imeshinda michezo mitano mfululizo, ikiwemo mmoja wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola ni minne ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo (3-0), Mashujaa (1-0), KMC (4-0) na Pamba (1-0).

Mbali na Simba kuwa na safu kali ya ushambuliaji, imeonyesha kuwa na ngome imara ambayo imewafanya ndani ya michezo hiyo kutoruhusu bao, msimu huu Simba imeruhusu bao moja tu katika mashindano ya kimataifa na ilikuwa dhidi dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya wakati wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1 Uwanja wa Benjamini Mkapa na kutinga makundi kibabe.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema wanatarajiwa mchezo mgumu na wenye ushindani lakini anaimani kubwa ya kufanya vizuri licha ya kuwa ugenini.

“Tunatambua kucheza ugenini ni tofauti na nyumbani lakini tupo hapa kwa ajili ya kufanya kile ambacho tutaweza ili kupata pointi ambazo zitatuweka kwenye mazingira mazuri,” alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini na kuongeza.

“Tulipata muda wa kuwasoma wapinzani wetu, tunajua ubora walionao.”

Hata hivyo, kocha wa zamani wa Simba, Abdelhak Benchikha ambaye hivi sasa anainoa JS Kabylie ya Algeria, ameanza kwa kusema: “CS Constantine wanajua kuutafuta ushindi lakini Simba kama itacheza kikubwa kama ilivyofanya dhidi ya Al Ahli Tripoli naamini watafanya vizuri japo wanatakiwa kuwa na nidhamu ya mchezo.”

Kuhusu MC Alger, Benchikha alisema: “MC Alger inacheza soka la mashambulizi ya kushtukiza, Yanga wanatakiwa kujipanga sana na hilo kwani ushindi wao umekuwa ukitokana na mashambulizi ya aina hiyo.”

Related Posts