Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
SERIKALI imeeleza dhamira yake ya kuhakikisha wakandarasi na wazabuni wa ndani wanajengewa uwezo ili kuongeza fursa za ajira na kuchangia maendeleo ya kiuchumi.
Hayo yalisemwa Desemba 4, 2024, jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, wakati akifungua mkutano ulioandaliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA).
Mwandumbya alisema lengo la mkutano huo ni kupokea changamoto kutoka kwa wazabuni wanaoshiriki katika miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, pamoja na kuweka mikakati ya kuzitatua.
“Changamoto za kimfumo na kimuundo zinaathiri uwezo wa wazabuni wa ndani kushindana na kufikia viwango vya kimataifa. Serikali imeboresha sheria ya ununuzi wa umma ili kutoa nafasi kwa Watanzania kushiriki kikamilifu,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwandumbya, maboresho ya sheria ya ununuzi wa umma yaliyofanywa mwaka 2023 yameongeza fursa kwa kampuni za ndani kushiriki katika miradi mikubwa, huku zikijenga mitaji yao na kupata ajira zaidi.
Upendeleo kwa wazabuni wa ndani
Kamishna wa Maendeleo ya Sera za Ununuzi wa Umma, Fredrick Mwakibinga, alisema Serikali imeweka upendeleo maalum kwa kampuni za ndani ili kuhakikisha hazinyimwi nafasi na kampuni za kigeni.
“Hii ni hatua muhimu ya kuwawezesha wazabuni wa ndani kushiriki katika miradi ya maendeleo na kuongeza uwezo wa kiuchumi. Mikutano kama huu inatoa nafasi ya kubaini changamoto na kutafuta suluhisho,” alisema Mwakibinga.
Hata hivyo, alitaja changamoto kama ukosefu wa mitaji na uelewa mdogo wa taratibu kama vikwazo vinavyoathiri ushiriki wa wazabuni wa ndani.
Mkutano huo umeelezwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha miongozo ya ununuzi wa umma na kuhakikisha Watanzania wanapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika miradi inayofadhiliwa na taasisi za kimataifa kama Benki ya Dunia.