Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru watu watano wakiwemo waliokuwa askari Polisi, waliyokuwa wanakabiliwa na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha na kujipatia Sh90 milioni, baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.
Uamuzi huo umetolewa jana Jumatano, Desemba 4, 2024 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu.
Hakimu Kiswaga amesema wenye jukumu la kuthibitisha mashtaka pasina kuacha shaka ni upande wa mashtaka na siyo kuegemea utetezi wa washtakiwa.
Walioachiwa huru ni waliokuwa askari kanzu watatu mwenye namba F 7149 D/Coplo Ramadhani Tarimo (42) maarufu Rasta na mkazi wa Kipawa; G 7513 D/koplo Majid Abdallah (35) mkazi wa Kunduchi na WP 6582 D/ koplo Stella Mashaka (41).
Wengine ni waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya RHG General Traders Ltd ambao ni Ashiraf Sango (31) na Emmanuel Jimmy (31), wote wakazi wa jiji hilo.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Oktoba 31, 2023 na kusomewa shtaka hilo ambao halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hadi wanaachiwa huru, washtakiwa hao wamekaa gerezani kwa siku 399, ambazo ni sawa na mwaka mmoja na mwezi mmoja na siku 4.
Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 197/2023 yenye shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha, tukio wanalodaiwa kulitenda Agosti 28, 2023 katika eneo la Kurasani, karibu na ofisi za Uhamiaji, zilizopo Wilaya ya Ilala.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja waliiba Sh90 milioni kutoka kwa Grace Donald Matage.
Inadaiwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia Grace kwa bunduki ili waweze kujipatia fedha hizo bila kikwazo.
Akichambua ushahidi, Hakimu Kiswaga amesema washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kinyume na kifungu 287B cha Kanuni ya Adhabu.
Amesema kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha likifanywa na washtakiwa wakatiwa hatiani, adhabu yake ni kifungo cha miaka isiyopungua 30 kama ilivyoelezwa na kifungu cha 287A cha kanuni ya adhabu sura ya 16.
Amesema wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi saba na vielelezo kuthibitisha shtaka hilo wakati upande washtakiwa wao walijitetea kwa njia ya kiapo na walikana kuhusika na shtaka hilo, huku wengine wakiwasilisha mashahidi kwa ajili ya kuwatetea.
Hakimu Kiswaga amesema wenye jukumu la kuthibitisha mashtaka pasina kuacha shaka ni upande wa mashtaka na sio kuegemea wingi wa mashahidi.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Kiswaga amesema wenye jukumu la kuthibitisha mashtaka pasina kuacha shaka ni upande wa mashtaka na sheria zinaeleza hiyo.
Amesema tukio lilitokea Agosti 28, 2023 lakini mlalamikaji halikuripoti siku hiyo kituo cha Polisi na badala aliripoti Kituo Kikuu cha Polisi mwezi mmoja baadaye yaani Oktoba 29, 2023.
“Sasa katika mazingira hayo, je kitendo cha unyang’anyi kiliweza kufanyika? Alihoji hakimu Kiswaga na kuongeza.
“Unyang’anyi wa kutumia silaha unatokea pale wizi unafanyika na washtakiwa wanatumia silaha, lakini katika kesi hii…Fedha zilikuwa zinapelekwa katika eneo hilo la Kurasini wakati mlalamikaji akiendelea kuongea na washtakiwa bila kutishiwa na silaha” amesema hakimu.
Amesema katika mazingira hayo, mahakama imejiridhisha kuwa hakuna ushahidi wowote wa upande wa mashtaka uliyoonyesha kuwa fedha zilizotolewa zilikuwa ni Sh90 milioni kwa sababu hakuna uthibitisho uliopelekwa mahakamani hapo kuonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha kilichotolewa kilikuwa ni Dola za Kimarekani au la.
Sababu nyingine ya kushindwa kuwatia hatiani, Mahakama hiyo imesema hakuna uthibitisho wala nyaraka yoyote ilioonyesha kama fedha hizo zilitoka katika ofisi ya Matage.
“Pia, hakuna uthibitisho wowote ulitolewa mahakamani hapa, ambao unaonyesha kuwa washtakiwa walitambuliwa na kupelekwa polisi na kwamba ili mahakama iwatie hatiani washtakiwa hawa, lazima kuwe na ushahidi wa kujitosheleza,” amesema Kiswaga.
“Hisia hata ziwe na nguvu kiasi gani, haziwezi kuwa za msingi kuwatia hatiani washtakiwa kama upande wa mashtaka hawajathibitisha shtaka pasina kuacha shaka,” amesema Hakimu Kiswaga.
Amesema mahakama hiyo inajiuliza wakati unyang’anyi unafanyika ilikuwa ni mchana na baadhi ya mashahidi waliyotoa ushahidi walikuwepo eneo la tukio, lakini hakuna hata shahidi mmoja aliyekwenda kuripoti kituo cha polisi juu ya unyang’anyi huo.
“Kifungu walichoshtakiwa nacho washtakiwa kinaeleza kuwa iwapo watatiwa hatiani, adhabu yao ni kifungo cha miaka 30 kila mmoja, sasa hoja hapa ni moja tu, iwapo washtakiwa walitenda kosa hilo au la?
Alisema shahidi wa kwanza, wa pili, wa nne na wa tano waliieleza mahakama namna mshtakiwa Tarimo, Majid na Stella walivyoenda katika ofisi za mlalamikaji, huku shahidi wa kwanza na wa sita wakiieleza Mahakama kwa kirefu namna fedha zile zilivyochukuliwa na washtakiwa hao.
Vilevile shahidi wa watano katika kesi hiyo, aliieleza mahakama jinsi alivyotumwa na Matage kwenda kuchukua Dola ofisi kwake na kwenda kuzibadilisha katika duka la kubadilishia fedha za kigeni na kisha kuzipeleka Kurasini sehemu ambayo mlalamikaji huyo alikuwa ameshikiliwa na washtakiwa hao.
Hakimu Kiswaga alisema Mahakama hiyo inajiuliza huo unyang’anyi anaodaiwa kufanyiwa mlalamikaji uliweza kufanyikaje wakati mlalamikaji huyo alipewa nafasi ya kumpigia simu mfanyakazi wake na kumuelekeza apelekewe fedha hizo huko Kurasini.
Alisema mahakama pia inajiuliza alitoaje fedha na kuwakabidhi watu hao wakati hakutishiwa kwa silaha, bali sihala hiyo ilikuwa imevaliwa kiuno na katika maelezo ya moja ya mashahidi wa upande wa mashtaka alidai kuwa silaha hiyo ilivaliwa kiunoni na mmoja wa askari hao kwa lengo la kuimarisha ulinzi katika eneo hilo la Kurasini.
Alisema wakati watu hao wakisubiria fedha kutoka ofisi kwa Matage, kulikuwa kuna watu wengine ambao waliambatana na mlalamikaji huyo katika eneo hilo, lakini hakuna hata mmoja aliyekwenda kutoa taarifa polisi kuwa Matage amefanyiwa unyanga’anyi.
“Ni jukumu la upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka na siyo kuegemea wingi wa mashahidi au utetezi wa washtakiwa,” alisema Hakimu Kiswaga na kuongeza.
“Sasa bila kupoteza muda na baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi saba wa upande wa mashtaka ambao wametoa ushahidi wao mahakamani hapa, Mahakama inaona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hawa na hivyo inawaachia huru washtakiwa wote watano,” alisema Hakimu Kiswaga.
Ndugu waangua vilio ndani ya mahakama
Wakati Hakimu Kiwagwa akiendelea kusoma uamuzi huo, ndugu na jamaa wa washtakiwa hao walikuwa wamejaa ndani ya Mahakama ya wazi namba moja waliangua vilio vya furaha, hali iliyopelekea askari Polisi pamoja askari Magereza waliokuwepo ndani ya mahakama hiyo kutuliza hali hiyo.