Nondo azungumzia afya yake akiwa wodini

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema licha ya afya yake kuendelea kuimarika, lakini bado anasikia maumivu sehemu za uti wa mgongo na mabegani.

Maeneo mengine anayosikia maumivu ni mkono, magoti na miguu inayomuuma kwa nyakati tofauti kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa watu wanaodaiwa kumteka saa 10 alfajiri na kumtelekeza katika ufukwe wa Coco wilayani Kinondoni saa tano usiku.

Nondo anadaiwa kutekwa Desemba 1, 2024 nje ya Stendi ya Mabasi ya Magufuli, Mbezi Louis akitokea mkoani Kigoma, alikokuwa akishiriki shughuli za ujenzi wa chama hicho hasa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika Novemba 27, mwaka huu.

Baada ya tukio hilo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini David Misime alisema kuna mtu mmoja mwanaume amekamatwa kwa nguvu na kuchukuliwa na watu waliokuwa wakitumia gari nyeupe lenye usajili wa namba T 249 CMV Land Cruiser.

Nondo anayepatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, ameliambia Mwananchi leo Alhamisi Desemba 5, 2024 hali ya inaendelea kuimarika tofauti na Jumapili Desemba mosi, alipofikishwa hospitalini hapo.

“Naendelea vizuri Alhamdulilah, mabega, maeneo ya uti wa mgongo bado yananisumbua kwa sababu walinipiga sana, pia kwenye magoti nikikunja na kukunjua naumini sana. Mkono wa kushoto kuukunja wote siwezi una maumivu,” amesema.

“Bado kuna maumivu, lakini tofauti na hali ya jana na juzi, au nilivyoletwa siku ya Jumapili, lakini namshukuru tena hali yangu inaendelea kuimarika kadri siku zinavyozidi kusonga mbele, nina imani Mungu atanijaali,” amesema Nondo.

Mwanasiasa huyo anasema bado hajajua lini atapewa ruhusa kutoka hospitalini, akisema anasubiri ripoti ya madaktari wanaofuatilia kwa karibu mwenendo wa afya yake.

“Mimi kupata ruhusa hadi madaktari walijiridhishe na mwenendo wa hali yangu kama imetengemaa, bado hawajaniambia lini, lakini nikiimarika basi wataniambia sasa naweza kwenda nyumbani. Hata hivyo, nikiruhusiwa nitakuwa nakuja kwa ajili ya kliniki,” amesema Nondo.

Hivi karibuni akihojiwa na kituo kimoja cha redio, Nondo alisimulia mwanzo mwisho wa tukio la kutekwa na kuachiwa, akisema bado ana hofu na maisha yake kutokana na vitisho alivyokuwa akivipata kutoka kwa watu waliokuwa wanamshikilia.

Nondo alisema akiwa nje ya kituo hicho kutafuta usafiri, wakatokea vijana sita, waliomvamia na kumtaka kutopiga kelele.

“Waliniambia nitulie, awali nilihisi ni vibaka, lakini jambo lilikuwa ‘serious’ zaidi baada ya kuona gari nyeupe Hardtop likasogezwa na milango ya nyumba ilifunguliwa ili niingie ndani.

“Nilipiga kelele kuingia katika gari, kuhakikisha siingii, nilikuwa naomba msaada kwa watu waliokuwapo nikawaambia nisaidieni naitwa Abdul Nondo, maana kulikuwa na watu wa boda, wasafiri waliokuwa wanafika kutoka safarini  na wengine kwenda mikoani,” alisema Nondo.

Nondo alisema tukio la kutekwa kwake lilikuwa la ghafla, kwa kuwa hakuwa na wazo kama kuna watu wanamfuatilia ili akamatwe. Alisema ukatamaji ule haukuwa wa kawaida kwa sababu waliotekeleza tukio hilo hawakujitambulisha.

“Nilichosikia walikuwa wakilaumu pingu ziko wapi, baada kuzikosa pingu walinifunga kamba kwenye mikono tena kwa nguvu sana mikono ikiwekwa nyuma na usoni walinifunga kitambaa,” alisema.

Nondo anasema baada ya kuchukuliwa gari lilikwenda kwa kasi kisha kuingia sehemu na kuegeshwa na kumshusha mwanasiasa huyo, kwa kumuweka pembeni ya kibaraza na kuanza kumshushia kipigo cha magongo, kwenye unyayo, mabega na maungio ya miguu, magoti, mapaja na kumnining’iniza juu chini.

Hii ni mara ya pili kwa Nondo, kutekwa  mara ya kwanza ilikuwa Machi 2018 Nondo akiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alidaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na kutekelezwa wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Related Posts