Siku ya Jumapili Desemba Mosi, 2024 ilikuwa ni siku ya Ukimwi duniani. Mwaka huu kaulimbiu inasema Chagua njia sahihi; Afya yangu, haki yangu.
Katika utafiti wa karibuni 2023 uliochapishwa katika Jarida la PLOS ONE, watafiti walichunguza uhusiano kati ya virusi vya Ukimwi (VVU) na vikundi vya damu vya ABO na Rhesus factor D (RhD).
Walifanya kwa kutumia taarifa kutoka katika vituo vya kukusanya damu katika majimbo manane kati ya tisa ya Afrika Kusini.
Kwa kawaida makundi ya damu yanapangwa kwa mfumo wa makundi ya ABO na Rhesus D. Ni aina ya vijichembe ambavyo vipo katika nyuso za seli nyekundu.
Aina ya damu ya kila mtu hutegemeana na chembe za antijeni zilizorithiwa kutoka kwa wazazi wao. Chembe za urithi yaani genes huchangia katika uwezekano wa mtu kuambukizwa VVU, kuenea kwa VVU hadi Ukimwi na kuwezesha ufanisi wa matibabu tofauti tofauti.
Kila mwaka mamilioni ya watu wanaingia katika hatari ya maambukizi ya VVU, lakini si kila mtu ataambukizwa. Ndiyo maana wapo wanaojamiiana bila kinga na waathirika lakini hawapati VVU. Watafiti wanakadiria chembe za urithi zinachukua asilimia 28 hadi 42 ya hatari ya mtu kuambukizwa VVU.
Antijeni za vikundi mbalimbali vya damu zimefanyiwa utafiti kuona kama chembe hizo zinaweza kukuza au kulinda mwili dhidi ya maambukizi ya VVU. Lakini hadi sasa, watafiti hawajapata uhusiano wowote wazi kati ya antijeni za aina ya damu na hatari ya kupata au kukabiliana na VVU.
Antijeni za kikundi cha damu ambazo zimechunguzwa kwa jukumu lao katika VVU ni pamoja na kundi la ABO lenye aina kama kundi O, A, AB na B.
Utafiti wa mapema wa VVU na Ukimwi uligundua wazi kwamba baadhi ya aina za damu huathirika zaidi na maambukizi ya VVU kuliko zingine.
Hata hivyo, nadharia hii haijathibitishwa na bado ina utata. Hapo awali, ilifikiriwa kuwa damu ya aina O iliongeza hatari ya VVU. Hii nayo ilipingwa na tafiti zingine ambazo ziligundua VVU ilikuwa ya kawaida zaidi kwa watu wenye damu ya aina ya AB au B. Hadi sasa, haijulikani ni kwa nini na kama ipo, jukumu la uchangiaji kundi la damu la mfumo wa ABO katika maambukizi ya VVU bado lina utata.
Protini za aina ya kundi la damu la mfumo wa Rhesus ziko kwenye uso wa seli nyekundu za damu. Nadharia ya awali ilikuwa Rh chanya kulindwa dhidi ya VVU na Rh hasi iliongeza hatari. Hata hivyo, utafiti haujaweza kuthibitisha uhusiano wowote kati ya aina ya kundi la Rh na hali ya maambukizi ya VVU. Ukiacha makundi ya damu, kuhusu chembe za urithi na VVU, kwa sasa DNA pia inatumika kutambua tiba mpya kwa ajili ya kuzuia na kutibu VVU.
Tafiti hizi za makundi ya damu na chembe za urithi, yaani genes zimechapishwa pia katika miaka ya karibuni katika majarida mbalimbali ya sayansi na tiba, ikiwamo JAMA, Science Today, The BMJ na Lancet.
Wanasayansi wana matumaini kwamba tafiti zilizofanywa na zitakazoendelea kufanywa kwa mapana zinaweza siku moja kasababisha tiba ya VVU na Ukimwi.
Nihitimishe kwa kusema kuwa mpaka sasa bado haijathibitika kisayansi kuwa moja kwa moja makundi ya damu na aina zake kuchangia au kupunguza uwezekano wa kuambukizwa VVU.