Sababu watoto kuzaliwa bila njia ya haja kubwa

Dar es Salaam. Idadi ya watoto wanaozaliwa na changamoto kwenye njia ya haja kubwa, kitaalamu ‘anorectal malformation’ (ARM) imetajwa kuongezeka nchini.

Ili mfumo wa haja kubwa ukamilike unapaswa kuungana na utumbo mkubwa na kuwe na uwazi.

Katika uwazi huo ni lazima kuwe na valvu iliyosheheni mishipa ya fahamu ambayo kazi yake kubwa ni kuratibu shughuli zote za njia ya haja kubwa, ikiwemo kutoa hewa na kupata haja nyepesi na ngumu.

Kwa mujibu wa Daktari bingwa na mbobezi wa upasuaji wa watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaituni Bokhari, mtoto mchanga anapaswa kupata haja ndani ya saa 24 tangu kuzaliwa kwake, asipopata ni dalili mojawapo ya mtoto huyo kukosa njia ya haja kubwa.

Hali hii inadhihirika kwa mtoto ambaye hawezi kutoa haja kubwa kwa njia ya kawaida, huku nyingine zikiungana na njia ya mkojo na kisha haja hizo mbili kutokea sehemu moja.

Dk Zaituni, ambaye pia ni Mkuu wa kitengo cha upasuaji wa watoto, anasema hospitali hiyo inapokea watoto wawili mpaka watatu kwa siku wenye tatizo hilo.

Dk Zaituni anasema hiyo ni hali inayomtokea mtoto akiwa tumboni mapema baada ya yai kupevushwa kwa muda wa wiki sita mpaka nane za mwanzo.

“Baada ya wiki hizo, utumbo wa mtoto huanza kutengenezwa au kuumbwa, huku ukigawanyika na kufanya mifumo mbalimbali katika mwili. Huo ndio wakati ambao mfumo wa mkojo, kinyesi na mifumo mingine huundwa, huku kila mmoja ukifanya kazi yake.”

Mkanganyiko wa mifumo mbalimbali unapotokea, ndipo mtoto huzaliwa bila njia ya haja kubwa au inakuwa haijafunguka au njia hiyo imefunguka ila imefungukia sehemu isiyo sahihi,” anaeleza na kuongeza kuwa hali hii ya njia kufungukia sehemu isiyo sahihi, mara nyingi huwakumba watoto wa kike.

Anasema mara nyingi mfumo wa haja kubwa hujiunga kwenye kibofu cha mkojo na kufanya haja hizi kutokea sehemu moja au mfumo wa haja kubwa kujiunga kwenye mfuko wa uzazi (uterus) na kufanya haja hiyo kujaa kwenye mji wa uzazi badala ya kutoka nje ya mwili.

Dk Zaituni anasema baadhi ya dalili za mtoto kukosa njia ya haja kubwa ni pamoja na mtoto kukosa haja kwa saa 24 tangu kuzaliwa.

Tumbo kujaa gesi kutokana na kinyesi kujirundika tumboni, kukosa hamu ya kunyonya na kinyesi kuchanganyika kwenye njia ya mkojo ni dalili nyingine.

Kadhalika, anasema kwa miaka ya hivi karibuni uelewa umeongezeka kwa wazazi wengi kuwawahisha hospitali watoto wenye changamoto hiyo.

Anasema kutokana na uelewa huo, kila siku huwafanyia upasuaji watoto wawili mpaka watatu.

“Kila siku tunafanya upasuaji kwa watoto wawili mpaka watatu na kwa wiki tunawafanyia upasuaji watoto 21 na kwa mwezi hufikia watoto 84 na zaidi, huku kwa mwaka wakifikia watoto 1,008,” anasema daktari huyo.

Hata hivyo, anasema hawezi kuthibitisha kwamba tatizo hilo limekua kwa kiasi gani kwa sababu zamani uelewa ulikua mdogo kwa wazazi wengi kuficha watoto wenye matatizo kama haya kwa imani kuwa ni nuksi, laana au mkosi, kitu ambacho si cha kweli.

Dk Zaituni anasema hospitali hiyo inapokea watoto kutoka mikoa mbalimbali, huku baadhi yao wakitoka kwenye nchi za Kenya, Comoro na Uganda.

Anasema huduma ya kwanza kwa mtoto mwenye tatizo la kuzaliwa bila njia ya haja kubwa ni pamoja na kumwekea njia mbadala ya kutoa choo nje ambayo kitaalamu huitwa (temporary colostomy).

Dk Zaituni anaongeza kuwa njia pekee ya kumnusuru mtoto mwenye hali hiyo, ni kumfanyia upasuaji mara moja mpaka tatu, kulingana na tatizo lake linakuwa liko katika hatua gani.

Akizungumzia gharama, daktari huyo mbobezi wa upasuaji watoto, anasema hutegemeana na aina ya tatizo alilonalo mtoto.

Mtoto anapokuwa na tatizo la njia kuziba huku kukiwa na mbonyeo kwenye eneo la haja kubwa, mara nyingi hufanyiwa upasuaji mara moja.

“Upasuaji wa aina hii ya kwanza ni kuweka njia bila kufanya upasuaji wowote wa tumboni, upasuaji huu unagharimu Sh2.5 milioni na gharama nyingine za utanuaji wa sehemu hiyo ambao ni Sh400,000 mpaka Sh600,000,” anaeleza. Sambamba na hilo, Dk Zaituni anasema ikiwa mtoto ana tatizo la mifumo ya ndani na njia kuziba, ni lazima afanyiwe upasuaji mara tatu.

Upasuaji wa kwanza utakuwa wa kumwekea njia mbadala ya kutoa choo nje itakayogharimu Sh800,000 mpaka Sh1.2 milioni ambayo mara nyingi, hufanyika mara mtoto anapogundulika kuwa na tatizo hilo.

“Gharama nyingine ni ya mfuko mbadala wa kubebea choo anaowekewa mtoto, mfuko huu unauzwa Sh18,000 mpaka 20,000 kwa baadhi ya sehemu.

Aidha, mfumo huo unapaswa kubadilishwa kila baada ya siku tatu hadi saba kulingana na hali ya mtoto na aina ya mfuko,” anasema.

Anasema kutokana na gharama za mfuko huo maalumu wa kubebea choo, baadhi ya wazazi hujitengenezea mifuko kwa kushona vitambaa na kutumia pampas, ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza gharama hizo.

Upasuaji wa pili kwa aina hii ya high type ni kutengeneza njia ya kupata haja kubwa ambayo hugharimu Sh2.5 milioni.

Kadhalika anaongeza kuwa upasuaji wa kutengeneza njia hufanyika kwa mtoto mwenye umri wa miezi 6 na kuendelea, huku sababu ikiwa ni mtoto kushindwa kuhimili nguvu ya dawa zinazotumika wakati wa upasuaji.

Magdalena Joseph, mama wa mtoto mwenye changamoto hiyo, anasema kuwa moja kati ya changamoto anayopitia ni gharama za matibabu.

Anasema kila anapokwenda kliniki kwa ajili ya kutanuliwa njia anatakiwa kuwa na zaidi ya Sh300,000, hali inayomfanya ashindwe kukamilisha ratiba ya kumpeleka mtoto wake kliniki kupatiwa matibabu kama anavyoshauriwa na daktari.

Related Posts