FOUNTAIN Gate imeendelea na mchakato wa kuboresha kikosi chake kuelekea usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 15 mwaka huu baada ya kumalizana na Said Mbatty.
Mbatty alikuwa nahodha wa Tabora United, ikiwa daraja la chini hadi ilipopanda msimu huu anaungana na timu hiyo akiwa mchezaji huru na ataungana na mshambuliajia Yusuf Athuman ambaye pia amemalizana na timu hiyo.
Chanzo cha kuaminika kutoka Fountain maarufu kama FOG kimeliambia Mwanaspoti, mchezaji huyo tayari amemalizana na timu hiyo na muda wowote kuanzia sasa ataungana nayo tayari kwa ajili ya kujiweka sawa.
“Bado tunaendelea kuimarisha kikosi chetu, kuna wachezaji hawatakuwa sehemu ya timu yetu mara baada ya dirisha kufunguliwa, hivyo watapishana na hawa wapya,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Kuongeza wachezaji ni mpango wa benchi la ufundi na tuna imani kubwa na mapendekezo hayo ambayo tayari tumeanza kuyafanyia kazi na tunaendelea.”
Mtoa taarifa huyo aliongeza bado wanapambana na usajili mwingine wa mchezaji ambaye anacheza eneo la kiungo mkabaji ambaye hakutaka kuweka jina lake wazi, lakini Mwanaspoti linafahamu wapo katika mazungumzo na Nasoro Kapama wa Kagera Sugar.
Fauntain ipo nafasi ya saba katika msimamo baada ya kucheza mechi 12, wakikusanya pointi 17, wameshinda mechi tano sare mbili na vipigo vitano.