Watu wanaoishi na kisukari hukutana na changamoto za kudhibiti kiwango cha sukari, jambo linaloweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya, kama vile magonjwa ya moyo, kiharusi, matatizo ya figo, upofu na vidonda visivyopona.
Hata hivyo, athari za kisukari siyo tu za kimwili, bali pia huweza kusababisha matatizo ya kisaikolojia.
Kwa watu wengi wenye kisukari hupitia hali ya wasiwasi, hofu na huzuni kubwa kuhusu maisha yao ya kila siku. Hali hii inaweza kuathiri ushirikiano wao katika matibabu, unaweza kuzorotesha maendeleo yao binafsi na maisha kwa jumla.
Hivyo, ushauri nasaha unakuwa na umuhimu kwao. Ushauri nasaha ni njia bora ya kuwasaidia kuhimili changamoto hizi za kisaikolojia na kimihemko.
Ushauri nasaha kwa wenye kisukari unahusisha kutoa msaada wa kisaikolojia na kimhemko ili kuwasaidia watu waelewe na kukubaliana na hali na namna ya kuishi.
Wataalamu wa ushauri nasaha wanatoa huduma ya kufundisha mbinu za kukabiliana na mafadhaiko, wasiwasi na huzuni. Hii ni muhimu, kwani mabadiliko katika mtindo wa maisha, pamoja na kurekebisha mlo, mazoezi na matumizi ya dawa, yanahitaji nguvu za ziada, akili na utayari wa hisia. Wengi hawawezi kukubaliana na mabadiliko haya bila msaada wa kisaikolojia.
Ushauri nasaha unasaidia kupunguza hatari ya matatizo ya ziada, kama vile shinikizo la damu na magonjwa ya moyo yanayoweza kutokea kutokana na wasiwasi na msongo wa mawazo.
Wenye kisukari wanaweza kuathiriwa na hali ya kujiona kana kwamba wako pekee yao duniani, hivyo kuwa na mtu wa kuwashauri na kuonesha kuwa wapo pamoja nao kunaweza kuleta nafuu kubwa.
Wataalamu wa ushauri nasaha pia wanaweza kusaidia watu hao katika kujenga mtazamo chanya kuhusu afya yao na kwa njia hii wanasaidia kupunguza athari za magonjwa ya kisukari kwa kuimarisha hali ya kiakili na hisia.
Ushauri nasaha unahakikisha kuwa watu wenye kisukari wanapata elimu kuhusu kisukari na namna bora ya kudhibiti kisukari. Wataalamu wa ushauri nasaha mara nyingi hushirikiana na madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa afya ili kutoa msaada wa kina kwa mgonjwa.
Elimu hii inahusisha namna ya kujitunza, mbinu za kupambana na msongo wa mawazo na umuhimu wa kufuata maelekezo ya matibabu.
Hii inawawezesha watu kuishi maisha bora na yenye afya, huku wakiepuka athari za kiafya zinazoweza kutokea kutokana na udhibiti mbovu wa kisukari.
Ushauri nasaha pia unaweza kusaidia kufuta hali ya kujinyanyapaa wenyewe kwa kujiweka mbali na jamii.