Na Oscar Assenga,TANGA
SERIKALI imesema kwamba itahakikisha uundwaji wa Bodi ya Wanajiolojia Tanzania (TGS) ili waweze kuwa na chombo ambacho kinaweza kuwaunganisha wataalamu hao kuweza kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta hiyo.
Hayo yalisemwa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Msafiri Mbibo wakati akifungua mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wataalamu wanajiolojia ulishirikisha wataalamu kutokana ndani na nje ya nchi wa siku mbili unaofanyika Jijini Tanga.
Hatua hiyo inatokana na kauli iliyotolewa kwenye mkutano huo na Rais wa Jumuiya wa Wanajiolojia Tanzania Dkt Elisante Mshiu ambapo alisema kwamba kama taasisi hiyo haitopata bodi basi kunaweza kuwa kikwazo katika mchango wao kuweza kutimiza maono ya 2030.
Alisema kwamba wamelipokea wapo pamoja na wataendelea kuwasiliana kuona jinsi ambavyo wanaweza kuharakisha uundwaji wa bodi hiyo ili kuchochea kasi ya ukuaji wa chombo chenu.
“Wizara ya madini imeendelea kutumia wanajiosayansi katika kufanya tafiti kwa lengo la kubaini uwepo wa madini nchini kupitia maono ya Vision 2030 madini ni maisha,madini ni utajiri ni lengo la wizara ya madini na maono ya mheshimiwa Waziri kuhakikisha kwamba maisha ya watanzania yanabadilishwa kutokana na rasilimali hizi ambazo ni za thamani sana zilizopo Nchini,”alibainisha Katibu Mkuu.
‘Ili kufanikisha maono haya wanajiosayansi wameendelea kutumia utaalamu wao kkatika kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa lengo la kutambua tabia za miamba utambuzi huu unatuwezesha kufanyika kwa tafiti nyingine za jiosayansi zenye kuwezesha kubaini aina mbalimbali za madini yanayopatikana nchini,”alisisitiza Katibu Mkuu huyo.
Kwa upande wake Rais wa jumuiya ya wanajiolojia Tanzania Dkt. Elisante Mshiu amesema kwamba wamekutana kwajili ya kujadiliana juu ya mabadiliko kutoka kwenye nishati chafuzi kwenda kwenye nishati salama ambazo zote ukiangalia ni malengo ya serikali.
Amewataka wanajiolijio kuelewa majukumu yao hususani katika kuelekea kwenye maono ya 2030 huku akieleza kwamba bila kuwa na bodi ya usajili ya wanajiosayansi maono ya 2030 yanaweza kuwa na changamoto hivyo ameendelea kusisitiza umuhimu wa uundwaji bodi hiyo.
“Kupitia Wizara ya madini tayari kuna juhudi kubwa zinafanyika na hatua hizo ziko mwishoni lakini ujumbe wetu kwa serikali ni kupeleka jambo hili kwa haraka ili liendane na kasi ya serikali kimaendeleo wito wangu kwa watanzania ni kwamba madini ni utajiri na nchi yetu ni tajiri kirasilimali tuko hapa hapa kuhakikisha tunaisaidia serikali kufikia malengo iliyojiwekea,”alisema Rais Mshiu.