Watumishi TRA wapigwa wakihusishwa na utekaji, Mwigulu, Polisi watoa onyo

 Dar es Salaam. Watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameshambuliwa wakiwa wakitaka kukamata gari linalodaiwa kuingizwa nchini kimagendo eneo la Tegeta kwa Ndevu jijini Dar es Salaam, wakihusishwa na utekaji.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Desemba 6, 2024, imesema tukio hilo limetokea usiku wa Desemba 5, 2024 wakati watumishi hao wa TRA wakiwa kwenye gari la Serikali.

Kufuatia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ameonya vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi.

“Wananchi watajiingiza kwenye matatizo. waache kujichukulia sheria mkononi,” amesema.

TRA kwenye taarifa yake imesema mkasa huo ulitokea wakati watumishi hao wakiwa kwenye majukumu yao ya udhibiti wa magendo na magari yaliyoingizwa nchini kinyume na utaratibu wa forodha.

Wakiwa kwenye utekelezaji wa jukumu hilo, watendaji hao wa TRA waliliona gari aina ya BMW X 6 lililoingizwa nchini bila kufuata utaratibu, hivyo wakaanza kulifuatilia kwa lengo la kulikamata ili liweze kulipa kodi takiwa.

“Wakati wanatimiza wajibu wao, walihusishwa na kitendo cha utekaji, kilichosababisha wao na gari kushambuliwa. Mamlaka ya Mapato Tanzania, inawapa pole watumishi wake waliojeruhiwa wakiwa wanatimiza wajibu wao, pamoja na wengine wote waliojeruhiwa katika kadhia hii, na kuwaombea wapone kwa haraka,” imeeleza taarifa hiyo.

TRA imewahakikishia wananchi kuwa itaendelea kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Kupitia mitandao wake X zamani Twitter, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba ameeleza kusikitishwa na tukio la kushambuliwa kwa watumishi hao.

“Nimesikitishwa na tukio la kushambuliwa kwa watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na gari lao (STL 9923) walipokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kisheria ya kudhibiti magendo na magari yaliyoingizwa nchini kinyume cha sheria, usiku wa tarehe 5 Desemba 2024, katika eneo la Tegeta kwa Ndevu, Dar es Salaam,” ameandika.

“Wizara ya Fedha inalaani vikali tukio hili na kuahidi kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika wa uhalifu huu. Aidha, TRA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa mujibu wa sheria,” ameandika.

Dk Mwigulu ametoa  wito kwa wananchi wote kushirikiana na Serikali kuhakikisha sheria za kodi zinatekelezwa ipasavyo kwa maendeleo ya Taifa, akisisitiza “Kodi Zetu ndiyo Maendeleo Yetu”.

Kupitia mitandao ya kijamii ilisambaa picha mjongeo ikionyesha gari aina ya LandCruiser Hardtop nyeupe likiwa limepasuliwa vioo likiwa na watu waliojitambulisha ni maofisa wa TRA. Walikuwa wamezuia gari BMW X6 wakimtaka dereva ashuke wanamuhitaji.

Hata hivyo, dereva huyo aligoma kushuka na  kufunga vioo huku akipiga kelele za kuomba msaada, kwamba anatekwa na watu asiowafahamu.

Baada ya kelele hizo, kulitokea msongamano wa magari na watu na wakaanza kulishambulia gari lenye watumishi hao kwa mawe.

Related Posts