Dar es Salaam. Hali ya utoaji wa huduma za afya nchini kwa mwaka 2024 imeendelea kuboreka kwa kiasi kikubwa, ingawa changamoto kadhaa bado zipo.
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, imewekeza katika kuboresha miundombinu, upatikanaji wa dawa na kuongeza rasilimali watu kwenye sekta ya afya.
Serikali imeendelea kujenga na kukarabati hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati ili kufanikisha huduma kwa maeneo ya vijijini.
Pamoja na hayo, kuna teknolojia ya matibabu kwa kuimarishwa upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi, ikiwemo kuanzishwa rasmi kwa kitengo cha upandikizaji mimba, yaani IVF kilichopo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Hata hivyo, eneo la rasilimali watu, mwaka 2024 Serikali imeongeza ajira kwa watumishi wa sekta ya afya, ikiwa ni pamoja na madaktari, wauguzi na wataalamu wa maabara.
Programu za mafunzo ya ndani na nje ya nchi zimeimarishwa ili kukuza ujuzi wa watumishi wa afya, hata hivyo changamoto bado zipo katika maeneo ya vijijini ambako kuna uhaba wa watumishi wenye ujuzi.
Kuhusu bima ya afya kwa wote, Wizara ya Afya kuanzia Januari hadi Juni 2024 imeendelea kukamilisha uandaaji wa sheria na hatua zinazoendelea sasa ni maandalizi ya kanuni.
Hatua inayoendelea sasa ni kukamilika kwa kanuni za sheria hiyo kutakakoiwezesha Serikali kutekeleza Sheria hiyo, ikiwa ni pamoja na ugharamiaji wa huduma kwa wasio na uwezo kwa kuanzisha mfuko maalumu kulisaidia kundi hilo.
Hata hivyo, kuna changamoto kadhaa za uhaba wa rasilimali fedha, ingawa bajeti ya afya imeongezeka bado kuna pengo katika kugharimia mahitaji yote ya sekta hii. Upatikanaji wa huduma bora za afya vijijini unahitaji maboresho zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya, kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka 9,366 vilivyokuwepo mwaka 2023 hadi kufikia vituo 9,826 Juni mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 4.9.
Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea anasema kati ya vituo hivyo, 7,366 sawa na asilimia 75 vinamilikiwa na Serikali na 1,006 vinamilikiwa na mashirika ya dini, vituo 79 vinamilikiwa na mashirika ya umma na 1,375 vikimilikiwa na watu binafsi.
Anasema katika kipindi hicho, idadi ya wagonjwa wa kulazwa iliongezeka kufikia 971,271 ikilinganishwa na wagonjwa 951,011 mwaka 2023, ongezeko lililochangiwa na kuongezwa kwa vitanda.
“Hadi kufikia Juni 2024 idadi ya vitanda vya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya imeongezeka kutoka 104,687 mwaka 2023 hadi 126,209, kwa mujibu wa viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kila watu 1000 uwiano ni vitanda 2.5, hivyo Tanzania imefikia uwiano wa 2.1 kwa kila watu 1,000,” anasema.
Anasema kuhusu huduma za uchunguzi wa magonjwa, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa vifaatiba na uchunguzi wa magonjwa ili kutoa tiba stahiki kulingana na ugonjwa.
Kwa mujibu wa Dk Nyembea, hadi kufikia Juni 2024 tayari kumenunuliwa na kusambazwa vifaa vya uchunguzi na jumla ya wagonjwa 531,861 walitumia vifaa hivyo katika kipindi cha Januari hadi Juni 2024.
Magonjwa yaliyotikisa 2024
Kuhusu magonjwa yaliyoongoza katika mahudhurio ya wagonjwa wa nje hospitalini ni maambukizi ya mfumo wa hewa, ukiathiri zaidi watoto chini ya miaka mitano na zaidi pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kwa wenye miaka mitano na kuendelea.
Kama ilivyo katika orodha iliyotolewa na Dk Nyembea, kundi la watoto chini ya miaka mitano, magonjwa yaliyoongoza kwa mahudhurio ya wagonjwa wa nje ni maambukizi ya mfumo wa hewa asilimia 40.9, malaria asilimia 9.9, kichomi kikali asilimia 7.7 na kuharisha pasipo kupungukiwa maji asilimia 7.6.
Anasema magonjwa mengine ni maambukizi ya njia ya mkojo asilimia 6.7, magonjwa ya ngozi asilimia 4.2, magonjwa ya kuambukiza asilimia 3.8, minyoo ya tumbo asilimia 2.9, ngozi asilimia 2.4, kuhara na upotevu wa maji asilimia 2.1, magonjwa yote yakiathiri kundi la watoto chini ya miaka mitano.
“Kwa wenye miaka mitano na kuendelea, magonjwa yaliyowaathiri zaidi ni maambukizi katika mfumo wa hewa asilimia 18.6, maambukizi katika njia ya mkojo asilimia 15.6.
“Mengine ni malaria asilimia 6.9, shinikizo la juu la damu asilimia 5.9, vidonda vya tumbo asilimia 3.9, magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza asilimia 3.5, kisukari asilimia 2.9 na kichomi kikali asilimia 2.6, minyoo ya tumbo asilimia 2.3, magonjwa ya viungo asilimia 2.2,” anasema.
Kwa upande wa wagonjwa wa kulazwa, Dk Nyembea anasema Januari hadi Juni kwa watoto chini ya miaka mitano malaria iliongoza kuwalaza kwa asilimia 16.3, kichomi kikali asilimia 33.0 na wenye miaka mitano na zaidi waliathiriwa zaidi na shinikizo la damu kwa asilimia 8.7 na kisukari asilimia 4.5.
“Ugonjwa wa kuharisha uliwaathiri watoto kwa asilimia 8.8, upungufu wa damu asilimia 8.8, kuzaliwa na uzito pungufu asilimia 5.7, maambukizi ya mfumo wa hewa asilimia 5.3, maambukizi ya njia ya mkojo asilimia 3.2, selimundu asilimia 1.3 na kuugua asilimia 1.2,” anasema.
Dk Nyembea anasema kwa wenye miaka mitano na kuendelea, magonjwa yaliyoongoza kuwalaza hospitali ni malaria asilimia 16.3, maambukizi ya njia ya mkojo asilimia 9.6, upungufu wa damu asilimia 9.3, shinikizo la damu asilimia 8.7 na kichomi kikali asilimia 6.3.
“Ugonjwa wa vidonda vya tumbo nako ilichukia asilimia 6.3, magonjwa ya akina mama asilimia 5.4, kisukari asilimia 4.5, kuvunjika mfupa asilimia 3.7 na maambukizi katika mfumo wa hewa asilimia 3.5,” anasema.
Hata hivyo, wadau wa masuala ya afya wamezungumzia hali ilivyokuwa kwa mwaka 2024, wakisema ulikuwa wa mifumo ya kukabiliana na majanga kama Marbug, Ebola, Mpox na nchi imefanikiwa kuvuka salama.
Akizungumza na Mwananchi, Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Mugisha Nkoronko anasema nchi imeendelea kutoa huduma za kibingwa na kibobezi, kupandikiza figo na kutibu mafua, maambukizi ya mfumo wa mkojo (UTI) na magonjwa ya ajali.
Dk Mugisha anasema mwaka huu nchi imekuwa na kitita cha bima ambacho kimeathiri utoaji wa huduma, kupata Waziri wa Afya mpya (Jenista Mhagama) baada ya kuondoka Ummy Mwalimu na nchi imefanikiwa kushinda kiti cha Uongozi wa WHO Afrika.
“Afya ya jamii, tumeona mikutano ya afya mikubwa na midogo, mahususi MATbscientific Conference, THS, hospitali zimepata viongozi wapya na mengine mengi. Zaidi ya wataalamu wa afya 3,000 wamehitimu masomo na 900 wameajiriwa,” anasema.
Hata hivyo, anasema nchi imepata shida za kitita kipya cha NHIF, hali ambayo huenda ilichangia kuondoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF (Bernard Konga) na kuletwa mpya Dk Irene Isaka.
Dk Mugisha anasema miongoni mwa mambo yaliyojirudia ambayo yanafaa kuangaliwa zaidi ni wagonjwa kuendelea kuchelewa kuwahi hospitalini, ajali na majeruhi kuongezeka na kwamba bado wanawake wanapoteza maisha wakati wa uzazi, watoto wanapoteza maisha wanapozaliwa.
“Upatikanaji wa dawa na huduma za msingi bado sio kwa watu wote, maradhi bado ni maadui wakubwa wa maendeleo yetu. Tunadhani Taifa lina kazi ya kufanya, kujenga mifumo imara ya afya inayojibu matatizo ya wapiga kura wa nchi hii, wananchi wa mijini na vijijini,” anasema.
Dk Mugisha anasema mifumo hiyo inategemea ukuaji wa uchumi, utengaji wa bajeti zaidi pengine tufike asilimia 10 badala ya 5.7 ya sasa.
“Tuendelee kuwawezesha wafanyakazi wachache waliopo, tuwawekee mazingira mazuri zaidi ya kufanya kazi zao kwa weledi na urahisi, tuwalipe stahiki zao kwa wakati na tuboreshe maslahi yao,” anasema.
Anashauri ni vema kuajiri wataalamu zaidi kukabiliana na upungufu wa asilimia 66 uliopo na kwamba ni muhimu kujenga mfumo wa elimu kwa umma ili kuzuia na kudhibiti maradhi.
Kuharakishwa kwa mapitio ya Sera Mpya ya Afya ni muhimu ili kuachana na ile ya mwaka 2007 ambayo kwa mujibu wa Dk Mugisha imepitwa na wakati.
“Tujenge mifumo ya afya inayoboresha mazingira ya ukuaji wa sekta binafsi (PPP). Tushirikishe wadau wote wa Afya kuongeza kasi ya uwekezaji kwenye sekta ya afya, viwanda vya kuzalisha vifaa tiba, dawa na vitendanishi vya maabara,” anasema.
Anasema ni muhimu kupunguza utegemezi kwa wadau wa maendeleo na kushirikiana nao kwenye vipaumbele vinavyodhibiti na kuzuia magonjwa.
“Nanukuu kauli ya Prof. Fathala kuwa watu wetu hawafi kwa magonjwa ambayo hatuwezi kuyatibu bali kwa maamuzi na mipango inayotekelezwa isiyoshirikishi na vipaumbele hafifu. Mwaka 2025 tuna nafasi ya kupiga hatua kubwa tena kwa haraka na kwa mbinu rahisi,” anasema Dk Mugisha.