Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi
Mahmoud Thabit Kombo (Mb) ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha
Kwanza cha Mashauriano ya Kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kilichofanyika Makao Makuu
ya Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE mjini Abu Dhabi tarehe 05 Desemba 2024.
Kupitia
mazungumzo hayo ya kwanza na ya aina yake, Tanzania na UAE
zimehakikishiana dhamira zao za kuendelea kushirikiana kwa karibu
kuboresha uhusiano uliopo ili kuufikisha katika viwango vya juu kwa
manufaa ya nchi na wananchi wa pande zote mbili.
Aidha, Tanzania
na UAE zimeongelea pia umuhimu wa kushirikiana kiuchumi na kuwa na
ushirikiano wa kina uliojengwa juu ya msingi wa kuaminiana, ambao
umeyafanya mataifa haya kushirikiana kwa karibu katika kushughulikia
masuala mbalimbali ya pande mbili na ya kimataifa kwa maslahi ya pamoja
Pamoja
na mambo mengine kupitia mashauriano hayo Tanzania na UAE
zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo
biashara , uwekezaji, Kilimo, Mifugo na Uvuvi hususan kwenye mpango wa
Tanzania wa Build Better Tomorrow (BBT), Ujenzi na Usafirshaji, Nishati;
Afya na Uchumi wa Buluu.
Aidha, kwa upande wa Nishati UAE
imekubali ombi la Tanzania la kuunga mkono Agenda ya Nishati Safi ya
Kupikia (Clean Cooking Initiative) inayopewa msisitizo na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuungwa
mkono na Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika na Dunia kwa ujumla kwa
kuwa sio tu unamkomboa Mwanamke lakini pia inachangia katika agenda ya
Dunia ya utunzaji wa mazingira.
Katika kutekeleza makubaliano
tajwa pande zote mbili zimekubaliana kukamilisha na kusaini mikataba
mbalimbali ya ushirikiano hususan ya ya kiuchumi kwa maslahi ya wote.
Sambamba
na hilo, Tanzania na UAE zimekubaliana kuharakisha utekelezaji wa
mradi wa Upanuzi na Ukarabati wa Hospitali ya Wete, Pemba ambayo
inatekelezwa kwa ufadhali wa Mfuko wa Maendeleo ya Abu Dhabi kwa gharama
ya Dola za Marekani Milioni 10 pamoja na utekelezaji wa Mkataba kati ya
Mfuko wa Maendeleo wa Khalifa (Khalifa Fund) na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ya Msaada wa Dola za Marekani Milioni 10 kwa ajili ya Miradi
ya Wajasiliamali Wadogo na Wakati Zanzibar.
Akizungumza katika
majadiliano hayo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala
ya siasa wa UAE Mhe. Lana Nusseibeh alisema Tanzania ni moja ya wadau
wakubwa wa UAE barani Afrika na kuongeza kuwa hali hiyo imesababisha
kusainiwa kwa Mikataba ya Ushirikiano katika Sekta ya Anga na Kutotoza
Kodi Mara Mbili .
Kupitia mikataba hiyo Mashirika ya Ndege ya
Emirates, Etihad na FlyDubai pamoja na Air Tanzania yamepata kibali cha
safari za moja kwa moja kati ya nchi hizi mbili.
Kikao hicho
cha kwanza cha mashauriano ya kidiplomasia kimekuwa cha mafanikio na
kimefanyika wakati ambapo Tanzania na UAE zinaadhimisha miaka 50 ya
uhusiano wa kidiplomasia na sasa umejikita katika ushirikiano wa
kiuchumi kwa maslahi ya pande zote mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi
Mahmoud Thabit Kombo (Mb) akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Kikao cha
Kwanza cha Mashauriano ya Kidiplomasia kati ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kilichofanyika Makao Makuu
ya Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE mjini Abu Dhabi tarehe 05 Desemba 2024.Ujumbe
wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE )katika mashauriano hayo uliongozwa
na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulikia masuala ya siasa wa UAE
Mhe. Lana Nusseibeh