Dodoma. Wabunge 16 wamejeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Shabby walilokuwa wamepanda kwenda kwenye michezo ya Afrika Mashariki, Mombasa nchini Kenya, kugongana na lori lililokuwa likitoa Morogoro kuelekea Dodoma.
Ajali hiyo imehusisha basi la Kampuni ya Shabiby ambalo lilikuwa limebeba wabunge na maofisa wabunge na lori hilo lilikuwa likitokea Morogoro kuelekea Dodoma.
Mbali na wabunge, maofisa wawili wa bunge na dereva wa basi wamejeruhiwa.
Akizungumza leo Desemba 6, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma George Katabazi amesema ajali hiyo imetokea leo saa 2:00 asubuhi katika barabara kuu ya Dodoma-Morogoro kwenye eneo la Mbande, wilayani Kongwa.
“Chanzo cha ajali hiyo ni kwamba dereva wa gari hilo la Shabiby ambalo lilikuwa limebeba wabunge na maofisa wabunge hakuchukua tahadhari wakati akitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake na hivyo kugongana na lori hilo,” amesema Katabazi.
Amesema ajali hiyo imesababisha majeruhi 19 na dereva wa basi anashikiliwa na polisi kwa sababu yeye ndiye aliyesababisha ajali hiyo kwa kutochukua tahadhari.
Amesema majeruhi wanaendelea vizuri na matibabu katika Hospitali za Benjamin Mkapa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Hospitali ya Uhuru.
Amesema katika Hospitali ya Mkapa wapo majeruhi wanane, kati yao wabunge ni sita na maofisa wawili wa Bunge.
“Wito wangu madereva wazingatie sheria za usalama wa barabarani ili kuepusha ajali kwa sababu mara nyingi husababisha vifo pamoja na majeruhi na uharibifu wa vyombo. Wasiendeshe kwa mazoea, bali wazingatie sheria za usalama wa barabarani,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma halitamfumbia macho mtu yeyote atakayeendesha gari au chombo chochote cha moto bila kuzingatia usalama barabarani,” amesema.