WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, mipango na Uwekezaji nchini Tanzania Profesa Kitila Mkumbo amesema utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 utaenda sambamba na Mkakati maalumu wa uendelezaji wa Rasilimali watu ili kuhakikisha kuwa matarajio na malengo ya Dira hiyo mpya ya Taifa yanafikiwa kikamilifu na kwa wakati. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Waziri Kitila kadhalika amewaambia wanahabari kuwa ni muhimu kubadilisha mitazamo na fikra kwa wananchi na kwa Watumishi mbalimbali wa umma kwa kuwa na utamaduni wa matumizi sahihi ya muda, ili kuendana sawia na mipango na mikakati mbalimbali itakayotungwa, katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Prof. Kitila Mkumbo ameyasema hayo leo Ijumaa Disemba 06, 2024 wakati akizungumza na wahariri na wanahabari wa vyombo vya habari Jijini Dar es salaam, akihimiza umuhimu wa kuzingatiwa kikamilifu kwa maoni ya wananchi katika uandishi wa Dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 kama ilivyokuwa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
Katika maelezo yake, Kitila pia amewataka watanzania kutokujidharau kwa kuaminishwa kuwa Tanzania haipigia hatua za kimaendeleo na badala yake wasome na kufuatilia takwimu mbalimbali za ndani na nje ya nchi ambazo zote zimekuwa na viashiria vingi vya kuonesha kuwa Tanzania inapiga hatua za kuridhisha kwenye sekta mbalimbali za maendeleo.
“Mwaka 2000 pato la Taifa lilikuwa Dola Bilioni 13, leo hii tunazungumzia Dola za Marekani zaidi ya Bilioni 80. Pato la mtu mmoja mmoja mwaka 2000 lilikuwa Dola 384, leo hii tunazungumzia Dola za Marekani takribani 1210. Mwaka 2000 watoto chini ya asilimia 10 ndiyo waliokuwa wanapata nafasi ya kujiunga na elimu ya Sekondari, leo hii zaidi ya asilimia 70 ya watoto wanaomaliza elimu ya msingi wanajiunga na shule za Sekondari. Kwenye uchumi hivyo hivyo tunapiga hatua kwa mwendo mzuri,” amesema Mkumbo.
Akijibu Maswali ya wanahabari, Kitila pia amesema Dira 2050 itazingatia suala la uendelezaji wa vipaji na kukuza rasilimali watu kwa kuhakikisha elimu inaboreshwa zaidi pamoja na kutoa fursa katika ukuzaji wa sekta ya Viwanda ili kutoa ajira zaidi kwa vijana wanaoandamwa na changamoto ya kukosa ajira nchini.